Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Theluthi moja ya wafungwa barani Ulaya wana matatizo ya afya ya akili - WHO

Uzio wa senyenge unaozunguka kituo cha mahabusu.
Unsplash/Hédi Benyounes
Uzio wa senyenge unaozunguka kituo cha mahabusu.

Theluthi moja ya wafungwa barani Ulaya wana matatizo ya afya ya akili - WHO

Afya

Mfungwa mmoja kati ya watatu barani Ulaya ana matatizo ya afya ya akili, ripoti mpya ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Ulimwenguni (WHO) imeeleza.

Ripoti hiyo ya WHO inaeleza kuwa wakati magereza ya Ulaya yalisimamia vizuri udhibiti wa janga la COVID-19 kwa wafungwa, wasiwasi unabaki kuhusu huduma duni za afya ya akili, msongamano na viwango vya kujiua. 

"Magereza yamejumuika katika jamii na uwekezaji unaofanywa katika afya ya watu walio gerezani unakuwa faida ya jamii. Kifungo hakipaswi kamwe kuwa hukumu kwa afya duni. Raia wote wana haki ya kupata huduma bora za afya bila kujali hali zao za kisheria." Anasema Dkt. Hans Henri P. Kluge, Mkurugenzi wa kanda wa ofisi ya kanda ya WHO ya Ulaya. 

Kufuatilia wafungwa 600,000 

Ripoti ya pili ya WHO kuhusu hali ya afya ya magereza katika kanda ya Ulaya ya shirika hilo inatoa muhtasari wa utendakazi wa magereza katika eneo hilo kulingana na data ya uchunguzi kutoka nchi 36, ambapo zaidi ya watu 600,000 wamefungwa. 

Matokeo yameonesha kuwa hali iliyoenea zaidi miongoni mwa watu gerezani ni shida ya afya ya akili, inayoathiri asilimia 32.8 ya wafungwa. 

Ikiwa imeazishwa mwaka 2016 ili kushughulikia pengo la taarifa kuhusu afya ya magereza katika eneo hilo, Kanzidata ya WHO ya Afya katika Magereza ya Ulaya inabainisha maeneo ambayo yanahitaji kuzingatiwa. Pia inafuatilia afya za watu walio gerezani kwa nia ya kutathmini mifumo ya afya ya taasisi, kuingizwa katika huduma za afya kwa ujumla. 

Dkt. Kluge anaonya akisema, "wakati magereza yanapotengwa katika mfumo wa afya kwa ujumla, jamii za maeneo hayo zinaweza kuathirika zaidi."  

Kujiua, msongamano wa watu 

Ripoti hiyo imeangazia maeneo kadhaa yanayoleta mashaka, ikiwa ni pamoja na msongamano wa watu na ukosefu wa huduma za afya ya akili, ambayo inawakilisha hitaji kubwa la afya miongoni mwa watu walio jela katika eneo lote la ulaya. 

Utafiti huo ulifanywa mnamo mwaka 2021 na ulichukua taarifa pia za mwaka 2020, wakati ulimwengu ulikuwa unapambana na mwanzo wa janga la COVID-19. Sababu ya kawaida ya kifo katika magereza ilikuwa kujiua, ikiwa na kiwango cha juu zaidi kuliko katika jamii pana. 

Zaidi, matokeo ya utafiti yalionesha kuwa moja kati ya Mataifa matano Wanachama yaliripoti msongamano wa magereza, ambao una matokeo mabaya kwa afya. Ripoti hiyo inapendekeza kuwa hatua mbadala zisizo za kizuizini huzingatiwa kwa makosa ambayo hayaleti hatari kubwa kwa jamii na ambapo kuna hatua madhubuti zaidi, kama vile kugeukia matibabu kwa matatizo ya matumizi ya dawa za kulevya. 

Njia mbadala zinahitajika 

Mshauri wa WHO wa kanda ya Ulaya kuhusu masuala ya pombe, dawa za kulevya na afya ya magereza, Carina Ferreira-Borges amesema kusaidia watu walioachiwa kutoka gerezani kujumuika katika jamii na kupata huduma za afya, kunaweza kupunguza uwezekano wa kufanya makosa tena. 

Programu ya kipekee 

WHO inahamasisha ushiriki zaidi wa wizara za afya katika utoaji wa huduma za afya katika magereza kote kanda. 

Ofisi ya kanda ya WHO barani Ulaya imekuwa ikifanya kazi kuhusu afya ya magereza tangu mwaka 1995, ikianzisha programu pekee ya afya katika magereza duniani, ambayo inalenga kufuatilia na kutoa ushahidi ili kufahamisha maendeleo ya sera na mifumo ya sheria inayohusiana.