Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wiki chache zijazo ni muhimu sana kwa msaada Msumbiji-WHO

Mwanamke akitembea katika moja ya nyumba 2000 zilizoharibiwa na kimbunga idai kilichopiga kambi ya  Tongogara kusini mashariki mwa Zimbabwe.
UNHCR/Zinyange Auntony
Mwanamke akitembea katika moja ya nyumba 2000 zilizoharibiwa na kimbunga idai kilichopiga kambi ya Tongogara kusini mashariki mwa Zimbabwe.

Wiki chache zijazo ni muhimu sana kwa msaada Msumbiji-WHO

Msaada wa Kibinadamu

Mkurugenzi wa shirika la afya ulimwenguni WHO kanda ya Afrika Dkt. Matshidiso Moeti, leo ameshuhudia juhudi za misaada ya kuokoa misha katika kukabiliana na athari za kimbunga Idai kwenye mji wa Beira nchini msumbiji.

Akizungumza baada ya kuzuru jamii zilizoathirika na kimbunga Idai na kujionea hali halisi ya uharibifu kwenye vituo vya afya Dkt. Moeti amesema “Wiki chache zijazo ni muhimu sana na kasi inahitajika haraka endapo tunataka kuokoa maisha na kupunguza madhila kwa waathirika “

Ili kupanua wigo wa huduma za dharura WHO imepeleka wataalam ikiwemo wa magonjwa mbalimbali, wa kiufundi na wa kuzuia magonjwa ili kujenga timu imara ya watu 40.

Dkt. Moeto amesisitiza kuwa kurejesha huduma za kawaida za afya ni suala muhimu hasa kwa kuzia magonjwa ya kuambukiza kama kipindupindu na mengine ya mlipuko. “Nimeshguhudia wodi ya Watoto ya kituo cha afya cha Pontagera ikiwa imesambaratishwa kabisa , paa limeezuliwa na vifaa vyote vimeharibiwa na maji. Ni lazima tufanye kila liwezekanalo ili kuwalinda watu wa Msumbiji dhidi ya milipuko ya magonjwa au matatizo mengine ya kiafya yanayosababishwa na ukosefu wa huduma muhimu.”

Juhudi zinazofanyika

Ameongeza kuwa WHO hivi sasa inasaidia kurejesha huduma za msingi ili vituo vya afya vilivyoathirika nchini Msumbiji viweze kutoa huduma za kawaida na muhimu kwa watu wake ikiwemo chanjo, matibabu ya magonjwa yaliyozoeleka, tiba ya utapiamlo na magonjwa ya akili, huku ikihakikisha kwamba dawa zinaendelea kuttolewa kwa watu wanaoishi na virusi vya ukiwmi VVU, kifua kikuu au kisukari.

Pia suala lingine linalotia hofu kwa mujibu wa Dkt. Moeti ni wahudumu wa afya, familia zao na nyumba zao ambavyo vimeathirika vibaya. WHO inajitahidi kuwasaidia katika majukumu yao kama wahudumu wa afya lakini pia katika kukarabati vituo hivyoi ambako wanafanya kazi.

Karika ziara hiyo Dkt. Moeti amezuru pia hospitali kuu ya Beira, kituo cha afya cha jumla, kituo cha kutibu kipindupindu nba hospital zingine mbili zilizoandaliwa kwa ajili ya dharura  na na timu ya madaktari kutoa Italia na Ureno. Ametembelea pia kituo cha afya cha makazi ya muda ambako watu 1000 walioathirika na kimbunga Idai wanaishi.

Machi 24 mwaka 2019 nchini Msumbiji, mvulana akiwa amesimama karibu na nyumba iliyoharibiwa kufuatia mafuriko yaliyotokana na kimbunga idai mji wa Beira.
UNICEF/Prinsloo
Machi 24 mwaka 2019 nchini Msumbiji, mvulana akiwa amesimama karibu na nyumba iliyoharibiwa kufuatia mafuriko yaliyotokana na kimbunga idai mji wa Beira.

Msaada kutoka wadau wengine

Shirika la kimataifa la chama cha msalaba mwekundu , Madaktari wasio na mipaka (MSF) na shirika la Save the Children wanafanyakazi usiku na mchana ili kuanza kampeni ya chanjo kesho Jumatano Aprili 3. Karibu dozi 900,000 za chanjo zimeshawasili Beira kwa ajili ya zoezi hilo  kwa msaada wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF na WHO na zimefadhiliwa na muungano wa chanjo duniani GAVI.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na wizara ya afya ya Msumbiji hadi kufikia Aprili Mosi visa vya kipindupindu ni 1052 na visa zaidi vinatarajiwa kutokana na kuongezeka idadi ya watu wanaokuja vituo vya afya  wakiwa wanahara kupita kiasi. WHO inasema watu zaidi ya 128,000 wanaoishi katika makazi ya muda wako katika hatari kubwa ya kupata kipindupindu , kuhara damu na magonjwa mengine ya kuharisha kutokana na maji machafu na huduma duni za usafi, na sasa WHO inajiandaa na kuongezeka kwa visa vya malaria. Vyandarua vyenye dawa za mbu vipatavyo 750,000viko njiani kwenda kugawiwa kwenye maeneo yaliyoathirika. Shirika hilo limesema katika miezi mitatu ijayo dola milioni 40 zinahitajika ili kukidhi mahitaji ya dharura ya kiafya.

Huduma muhimu kwa waathirika

WFP nalo shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP linafanya kila juhudi kuwafikia watu milioni 1.2 wiki hii kwa msaada wa chakula hasa kwa kuwa barabara sasa zinafunguliwa kwenye maeneo ya vijijini katika majimbo manne yaliyoathirika zaidi ya Sofala, Manica, tete na Zambezia baada ya kutoa msaada wa chakula kwa watu 350,000 walioathirika.

Waathirika hao wanapata mgao wa chakula wa nafaka na maharagwe, vyakula vya makopo na mafuta ya kupikia vitakavyowatosheleza kwa siku 15.

Lengo la WFP ni kuwafikia watu milioni 1.7 kati ya milioni 1.8 wananchi wa Msumbiji wanaohitaji msaada wa dharura wa chakula wengi wao wamepoteza kila kitu , nyumba zao, vitu vyao, mazao yao na hata maisha . Kwas asa shirika hilo linasema kuna uhaba wa chakula masokoni na bei zinapanda kwa kasi. Nyanya kwa mfano zinagharibu mara 3 hadi 4 ya ilivyokuwa wiki moja iliyopita. Hivi sasa ndege zisizo na rubani za WFP au Drones zinatumika kufanya tathimini ya uharibifu wa miundombinu, ikiwemo shule, hospital, madaraja, vituo vya afya, barabara na hospital, na pia inaangalia maeneo ya mabondeni na yasiyofaa kwa waathirika kurejea.

Kwa upande wake WFP inahitaji dola milioni 133 kwa ajili ya kuendelea kusambaza msaada wa chakula , wa kiufundi na mawasiliano ya dharura kwa miezi mitatu ijayo.