Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baada ya kukimbia njaa na ghasia Somalia, sasa hofu ni ukatili wa kijinsia kambini Daadab.

Afisa mwandamizi wa Kamati ya Kimataifa ya uokozi, IRC Jane Ambale akikabidhi kikasha cha kujisafi kwa mmoja wa wakazi wa kambi ya Hagadera wakati wa tukio la uchunguzi kwa wakimbizi wapya kambini.
UNFPA Kenya
Afisa mwandamizi wa Kamati ya Kimataifa ya uokozi, IRC Jane Ambale akikabidhi kikasha cha kujisafi kwa mmoja wa wakazi wa kambi ya Hagadera wakati wa tukio la uchunguzi kwa wakimbizi wapya kambini.

Baada ya kukimbia njaa na ghasia Somalia, sasa hofu ni ukatili wa kijinsia kambini Daadab.

Wanawake

Wakati wa msimu wa krismasi mwaka jana, Rukia Yaroow Ali mwenye umri wa miaka 38, aliwasili kambi ya wakimbizi ya Hagadera iliyoko Daadab kaskazini mwa Kenya. Njaa na ukosefu wa usalama vilimlazimu akimbie kijiji chake cha Jilib nchini Somalia, akisafiri kwa punda na watoto wake 9.

Ukame ulisababisha mume wangu akimbie familia

Makala ya iliyochapishwa kwenye wavuti wa shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya watu na Afya ya uzazi  inamnukuu Rukia akisema “mume wangu alikuwa mkulima mwenye mafanikio makubwa, lakini ukame ulipobisha hodi, hakuweza tena kuendelea kulima mazao ya chakula.”

Mzigo wa kulea familia ulikuwa mzito mno, na kusababisha mvutano na mizonano kati yake na mumewe, “siku moja aliniambia anakwenda kutafuta kazi na katu hakurejea tena.”

Ukame unaoendelea katika Pembe ya Afrika umeweka shinikizo kubwa katika familia. Kama ilivyo kwa janga lolote linalosababishwa na tabianchi, wanawake na watoto wa kike wanabeba mzigo mkubwa zaidi za madhara. Wengi wanafanya safari za kutisha Kwenda kusaka chakula na maji, au Kwenda katika kambi za wakimbizi ambako huko wanaweza kupata misaada ya kiutu, ikiwemo huduma za afya kwa watoto wao.

Mwanaume aliyetusafirisha ananidai dola 33 sijui nitalipaje

“Nimefika hapa nikiwa sina chochote, na sikuweza kupata hata malazi au chakula kwa watoto wangu,” anasema Rukia akiongeza kuwa bado nina deni la dola 33 kwa mwanaume mmoja ambaye alitusafirisha hadi hapa, na sijui nitamlipa vipi.”

Kwa sasa, wanaishi kwenye makazi ya muda yaliyojengwa kwa fito na kufunikwa na sandarusi katika kambi ya Hagadera, akiwa na wengine wanaowasili kutoka Somalia. Miongoni mwao ni kaka yake na familia yake ambao waliwasili miezi michache kabla yake.

Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi duniani, UNHCR, mwaka 2022, takribani watu 45,000 walikimbia Somalia kutokana na ukame na kungia kambi za wakimbizi zilizoko eneo la Daadab lililoko kaskazini mwa Kenya. Kambi  hizo ni Hagadera, Ifo na Dagahaley.

Kambi ya Hagadera imejaa kuliko idadi yake

“Katika kambi ya Hagadera, tumekuwa na takribani ya ongezeko la asilimia 20 ya wakimbizi tangu mwezi Mei mwaka 2022, na hivyo kuweka shinikizo kubwa la rasilimali tulizo nazo kwa ajili ya wahitaji,” anasema Jane Ambale, Afisa mwandamizi wa ulinzi wa wanawake kutoka shirika la kimataifa la uokozi, IRC.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya watu duniani, na afya ya uzazi, UNFP linasaidia, IRC kuchunguza suala la ukatili wa kijinsia miongoni mwa wakimbizi wapya wanaowasili eneo hili, wengi wao hawajasajiliwa na hivyo inakuwa vigumu kupata huduma kambini.

Lengo letu ni kutambua wanawake na wasichana ambao ni manusura wa ukatili au wako hatarini kukumbwa na ukatili wa kijinsia na kisha tunawapatia taarifa muhimu na hutuma wanazohitaji,” anasema Bi. Ambale.

Kitendo cha wakimbizi wasiosajiliwa kukosa makazi na mgao wa chakula, kinaongeza maradufu hatari yao ya kukumbwa na ukatili wa kingono na wa kijinsia kwa kuwa mara nyingi hutegemea watu wengine ili kukidhi mahitaji yao ya msingi.

Ukame na ukosefu wa usalama nchini Somalia umemfurusha Rukia Yaarow Ali na watoto wake 9 na sasa anaishi ukimbizi nchini Kenya. Mume amemkimbia kwa sababu ya ukame na hawezi tena kutunza familia.
UNFPA Kenya

 ‘Chui waliovaa ngozi ya kondoo’ kambini Hagadera

“Mwezi Agosti mwaka 2022, mwanamke mmoja alifik akatika kituo cha IRC kambini Hagadera akisaka msaada baada ya kubakwa na mtu anayedaiwa kuwa msamaria mwema, mtu huyo alikuwa amejitolea kumpatia makazi mwanamke huyo na watoto wake mara tu baada ya kuwasili,” amesema Bi. Ambale.

IRC inaendesha kituo cha msaada kwa manusura wa ukatili wa kingono, kituo ambacho ni kama eneo salama kwa wanawake na wasichana kambini Hagadera.

Hapo wanapatiwa usaidizi wa kisaikolojia, matibabu na pia kuelekezwa vituo zaidi vya juu vya afya ili wapate huduma bora ya afya.

Kati ya mwezi Mei na Desemba mwaka jana, kituo hicho kimehudumia wanawake 2,000 wakiwemo 400 waliowasili wakiwapatia vikasha vya kujisafi ili kukidhi mahitaji yao wakiwa kambini.

UNHCR na IRC wanajitahidi kuepusha ukatili wa kingono na kijinsia

Kituo hicho mara kwa mara huwa na matukio ya kijamii mashinani, na kila wiki hutoa fursa ya kusikiliza sauti za wanawake ambao hukusanyika na kujadili mahitaji yao ya kupatiwa ulinzi na usalama.

“Mara nyingi manusura hawafahamu wapi wapate msaada, au wanahofia kuzungumza kwa wasiwasi pengine jamii itawatenga na hivyo kukosa msaada. Katika matukio yetu ya mashinani tunajitahidi kufikia wageni kwa kadri inavyowezekana na kuwafahamisha ya kwamba kuna msaada wakati wowote wanapohotaji,” anasisitiza Bi. Ambale.

UNHCR yahitaji dola milioni 114 kwa operesheni zake Pembe ya Afrika

Wakati jamii zinatafakari ukame mbaya zaidi kuwahi kukumba Somalia katika kipindi cha miaka 40, ukosefu wa usawa na ukosefu wa kupatia kipaumbele huduma za afya uzazi vinaongeza ‘chumvi kwenye kidonda’ na hivyo kuweka maisha ya maelfu ya wanawake na wasichana hatarini.

UNFPA inaimarisha harakati zake za kutoa huduma za kuokoa masiha za afya ya uzazi na ulinzi ili kukidhi mahitaji na imezindua ombi lake la dola milioni 114 la kusaidia operesheni zake kukabili ukame katika Pembe ya Afrika kwa mwaka 2022-2023.