Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

COVID-19 yaengua zaidi watoto wakimbizi kwenye elimu, lakini heko kwa wabunifu waliohakikisha watoto hao wanasoma

Mkimbizi kutoka DRC, Henriette Kiwele kiyambi akiandaa apu yake ya urembo katika karakana ya kuandaa apu kwenye kambi  ya wakimbizi ya Dzeleka nchini Malawi, ikiwa ni sehemu ya mradi wa kuunganisha wakimbizi na intaneti unaofadhiliwa na UNHCR na Microsoft
UNHCR/Tina Ghelli
Mkimbizi kutoka DRC, Henriette Kiwele kiyambi akiandaa apu yake ya urembo katika karakana ya kuandaa apu kwenye kambi ya wakimbizi ya Dzeleka nchini Malawi, ikiwa ni sehemu ya mradi wa kuunganisha wakimbizi na intaneti unaofadhiliwa na UNHCR na Microsoft

COVID-19 yaengua zaidi watoto wakimbizi kwenye elimu, lakini heko kwa wabunifu waliohakikisha watoto hao wanasoma

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR limesema janga la ugonjwa wa Corona, au COVID-19 ni tishio kubwa kwa elimu ya wakimbizi duniani kote.

Hofu hiyo ya UNHCR ni kwa mujibu wa ripoti yake iliyotolewa leo ikipatiwa jina, Kushirikiana kwa ajili ya elimu ya wakimbizi, ripoti ambayo inasema kuwa “nusu ya watoto wote wakimbizi hawako shuleni na hivyo kutoa wito kwa jamii ya kimataifa kuchukua maamuzi magumu ili kukabiliana na athari hiyo itokanayo na virusi vya Corona.”

Akizungumzia ripoti hiyo, Kamishna Mkuu wa UNHCR, Filippo Grandi amesema kuwa, “katu hatuwezi kupora mustakabali wa watoto hao. Nusu ya watoto wakimbizi tayari walikuwa hawako shuleni, sasa baada ya kuvumilia kila kitu, hatuwezi kuwakosesha elimu yao hii leo. Licha ya changamoto zote zitokanazo na COVID-19, pamoja na msaada wa jamii ya kimataifa kwa wakimbizi na jamii enyeji, tunaweza kuongeza mbinu zetu bunifu za kulinda manufaa yaliyokwishapatikana kwenye elimu ya wakimbizi katika miaka iliyopita.”

Ripoti inabainisha kuwa wakati watoto katika kila nchi wanahaha na janga la Corona, watoto wakimbizi hali ni mbaya zaidi. 

Takwimu zinaonesha kuwa wanafunzi bilioni 1.6 duniani kote wakiwemo mamilioni ya watoto wakimbizi elimu yao imevurugwa.

Shefuka, mwenye umri wa miaka 9 akijisomea nyumbani kwa msaada wa mama na mwalimu wake, wakati huu ambapo kituo cha kujisomea kwenye kambi ya wakimbizi warohingya kimefungwa.
© UNICEF
Shefuka, mwenye umri wa miaka 9 akijisomea nyumbani kwa msaada wa mama na mwalimu wake, wakati huu ambapo kituo cha kujisomea kwenye kambi ya wakimbizi warohingya kimefungwa.

“Kabla ya janga, mtoto mkimbizi alikuwa na nafasi ya mara mbili zaidi kutokuwepo shuleni kuliko mtoto asiye mkimbizi,”  imesema ripoti hiyo ikiongeza kuwa hali inaweza kuwa mbaya zaidi  kwa kuwa wengi wao hawatakuwa na fursa ya kurejea masomoni kutokana na shule kufungwa, ugumu wa kulipa karo za shule, kununua sare za shule na vitabu, ukosefu wa teknolojia ya kusomea mtandaoni au kwa sababu wanatakiwa kufanya kazi ili kusaidia familia zao.

Heko wale walioibuka na mbinu bunifu ili watoto wakimbizi waendelee kusoma

Hata hivyo ripoti hiyo imeangazia pia mifano bora ya jinsi wakimbizi vijana na walimu wao wanaendelea kung’ara katikati ya janga la COVID-19.
“Kuanzia wakimbizi na wenyeji wao, hadi walimu, sekta binafsi, wadau, mamlaka za kitaifa na kimaeneo, wabunifu na mashirika ya kiutu, woete wamesaka mbinu bunifu za kuhakikisha elimu inaendelea kwa wakimbizi wakati huu wa corona,” imesema ripoti hiyo.

Bwana Grandi amesema kuwa anadhani kimekuwa ni kipindi cha kuonesha ubia, ukarimu na ubunifu kutoka kwa mamilioni ya vijana.

Amesema wakati wa vizuizi kutokana na  COVID-19, UNHCR, serikali na wadau walikuja na mbinu za kipekee, “kuanzia Misri kuhamishia mtaala mzima mtandaoni hai kambi ya wakimbizi ya Daadab nchini Kenya ambako matangazo ya shule kupitia redioni yalifanyika. Madarasa ya kuhamahama huko Bolivia, mbinu mpya za kufundisha kati ya wazazi na walimu huko Chad na jukwaa jipya la kujifunzia nchini Uganda, wote wakitumia mbinu za kuvuka kikwazo cha ukosefu wa mitandao ya intaneti au intaneti isiyo na nguvu.”