Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Msichana mkimbizi aongoza kwa alama za juu KCPE kambini Dadaab Kenya

Kambi ya Dadaab nchini Kenya, ni moja ya kambi kubwa zaidi za wakimbizi duniani.
IOM/UNHCR/Brendan Bannon
Kambi ya Dadaab nchini Kenya, ni moja ya kambi kubwa zaidi za wakimbizi duniani.

Msichana mkimbizi aongoza kwa alama za juu KCPE kambini Dadaab Kenya

Wahamiaji na Wakimbizi

Maryan Mohamed, mkimbizi kutoka Somalia anayeishi kambini Daadab nchini Kenya ameongoza kwa kupata alama za juu kuliko wanafunzi wenzake kwenye mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi, KCPE, kwa mwaka huu wa 2018. 

Maryan mwenye umri wa miaka 14 alipata alama 396 kati ya alama 500 na kuwa miongoni mwa wanafunzi 228,414  nchini Kenya waliopata kuanzia alama 300 na kuendelea.

Akiwa miongoni mwa watoto 7 wa familia moja, Maryan alifika Hagadera, eneo mojawapo la kambi ya Dadaab akiwa na umri wa miaka 6 baada ya wazazi wake kukimbia mgogoro nchini Somalia.

Licha ya kuwa mkimbizi na pia msichana, wazazi wake walimsisitiza kusoma kwa bidii na wakimwelezea faida za elimu bora.

Maryan anasema, “kuwa msichana na pia mtoto wa mwisho kwa kuzaliwa haiji na matarajio kidogo. Nilifanya kazi kubwa kuwafanya wazazi wangu, walimu na jamii yangu wajivunie. Hisabati ni somo ninalolipenda zaidi. Nifurahi kukokotoa na maswali na kujifunza vitu vipya”

Fatuma Ibrahim, ambaye ni mama mzazi wa Maryan amefurahishwa sana na taarifa za bintiye kupata alama za juu katika masomo, akisema , “nilimuhamasisha asome kwa bidi lakini nashukuru kwamba yeye mwenyewe anajituma. Mara nyingi, anaweza kuamka alfajiri kujisomea hisabati na Kiswahili kabla hajaenda shule. Usiku anatutumia taa ndogo ya mwanga wa jua zinazotolewa na UNHCR na alikuwa akifanyia kazi mazoezi anayopewa shuleni. Akitoka shule angependa kusaidia katika kazi za nyumbani lakini nilikuwa nahakikisha dada zake wanafanya hizo kazi.”

Zaidi ya wanafunzi wakimbizi 3000 katika kambi ya Daadab walifanya mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi, KCPE ambao ulikamilika tarehe mosi ya mwezi Novemba mwaka huu wa 2018. Maryan alifanya mtihani wake kwenye shule ya msingi ya Upendo, moja ya shule chache katika kambi hiyo ya wakimbizi.

Mwalimu mkuu wa shule aliyokuwa anasoma Maryan, Hussein Maalim naye ameeleza furaha kuhusu mafanikio ya mwanafunzi wake na akapongeza kipaji chake na bidii yake ya kujifunza,“Maryan wakati wote amekuwa miongoni mwa wanafunzi wa kwanza katika shule ya upendo. Anajifunza haraka akiwapita wavulana na wasichana wote katika darasa lake.”

Ameongeza kuwa “baada ya shule alikuwa anashiriki katika makundi ya kujisomea na wenzake wakijiandaa na mitihani ya mwisho na klabu za kijamii za shule nyingine. Elimu kwa wasichana bado ni changamoto kambini Daadab. Baadhi ya wasichana wanaachwa nyumbani kwa ajili ya shughuli za nyumbani kama kupika, kufanya usafi, kuteka maji na hata wengine wameolewa. Kwa hivyo mafanikio ya Maryan ni makubwa hakika”

Lakini mafanikio ya Maryan yanakuja kukiwa na umuhimu wa kuboresha elimu katika kambi ya Daadab.

Kuna zaidi ya wanafunzi 3,600 kwenye shule ya msingi ya Upendo na hakuna rasilimali za kutosha mahitaji.

Wakimbizi wanategemea UNHCR na wadau wake kuweza kuipta elimu. Kutokana na kupungua kwa fedha, idadi ya walimu imeshuka kutoka 1,257 katika mwaka 2017 hadi 920 katika mwaka huu wa 2018. Kuna walimu 173 ambao wana vigezo vya kuwa walimu wa shule ya msingi, kati yao 32 ni raia wa Kenya na 141 ni walimu wakimbizi.

Suleiman Hassan, mmoja wa maafisa wa UNHCR wanaohusika na elimu anasema,“Watoto katika shule nyingi za Dadaab wanasoma katika mazingira mabovu wakiwa wamelundikana katika madarasa. Hii imesababisha kuwa na watoto wengi jambo ambalo pia linaathiri mazingira bora ya kujifunza na hivyo kusababisha watoto kuacha kuhudhuria shuleAnaongeza kwa kusema kuwa, ili kuboresha mazingira bora ya kupata elimu kuna uhitaji mkubwa wa madarasa zaidi, vyoo na walimu zaidi wenye ujuzi ili kuweza kuwahudumia wanafunzi wote”

Bwana Hassan anasema kuwa “kuna upungufu wa walimu wa kike na ni asilimia 15 tu ya walimu ni wa kike. Kwa msingi huo, wasichana wanakosa watu wa kuwatazama kama kioo chao” 

Kambi ya Dadaab ina wakimbizi na wasaka hifadhi 208,500, na ina makazi matatu ikiwemo ya Hagadera, Ifo na Dagahaley.

Zaidi ya wakazi 104,300 wa kambi hiyo kubwa ni wa umri wa kwenda shule yaani kati ya miaka mitatu na saba na wakichukua nusu ya wakazi wote.

UNHCR  inasema ni watoto 63,892 tu kati ya wale wanaotakiwa kwenda shule ambao wameandikishwa shuleni na kati yao, 45,245 wameandikishwa katika shule zamsingi zilizoko katika kambi ya Dadaab.

Tweet URL

 

Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa, tafadhali jisajili na pia unaweza kupakua apu ili kuweza kusikiliza wakati wowote popote ulipo.