Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mikunde jawabu la tabianchi na ukosefu wa chakula- FAO

Theodosia Peter ambaye ni mnufaika wa mradi wa FAO huko Kigoma, Tanzania akikausha maharage  yake aliyovuna shambani.
FAO Tanzania
Theodosia Peter ambaye ni mnufaika wa mradi wa FAO huko Kigoma, Tanzania akikausha maharage yake aliyovuna shambani.

Mikunde jawabu la tabianchi na ukosefu wa chakula- FAO

Afya

Hii leo ikiwa ni siku ya mikunde duniani, shirika la Umoja wa Mataifa la chakula na kilimo FAO linapatia msisitizo umuhimmu wa zao hilo katika sio tu kuhimili mabadiliko ya tabianchi kwa kustahimili ukame, bila pia nafasi yake katika kuimarisha lishe kwa walaji.

Taarifa ya FAO iliyotolewa Roma, Italia, makao makuu ya shirika hilo inasema ujumbe wa mwaka huu ni Mikunde kwa Mustakabali Endelevu, na inataja mikunde kuwa ni pamoja na maharage, kunde, mbaazi, njegere na njugumawe.

“Mimea ya jamii ya mikunde inachangia kwa njia mbali mbali marekebisho ya mifumo ya uzalishaji chakula na inatusaidia kutatua majanga mengi ya dunia,” amesema QU Dongyu Mkurugenzi Mkuu wa FAO.

Amesema ni dhahiri kuwa wakati huu ambapo dunia inakabiliwa na changamoto kubwa za chakula na uhakika wa kupata lishe, mathalani kutokana na magugu, wadudu waharibifu wa mazao na madhara ya mabadiliko ya tabianchi, mimea ya mikunde inaweza kuwa jawabu bora kwa kuwa ni rahisi kupata, ina lishe ya kutosha na inaweza kuhifadhiwa kwa muda mrefu.

Faida za mikunde

Mimea ya mikunde inajenga fursa kwa wakulima wadogo kwa kuwa ina faida kubwa kuliko nafaka.

“Inasaidia kurutubisha udongo kwa kufyonza hewa ya nitrojeni kutoka angani na  kupunguza matumizi ya mbolea za viwandani na wakati huo huo kuhimili ukame au mvua,” imesema FAO.

Shirika hilo linaongeza kuwa pindi nafaka zinapandwa baada ya mzunguko wa mikunde, mavuno yanaweza kuwa tani moja na nusu zaidi kuliko pale ambapo zao moja linalimwa hilo hilo miaka nenda miaka rudi.

Halikadhalika inasaidia kukabili mabadiliko ya tabianchi kwa kuongeza uwezo wa udongo kuhifadhi hewa ya ukaa na kurejesha udongo uliomomonyolewa.

Hapa ni Tanzania ambako maharagwe yamepandwa kwenye shamba la mahindi kama njia ya kilimo hifadhi na kutunza unyevunyevu na rutuba ya udongo.
FAO Tanzania
Hapa ni Tanzania ambako maharagwe yamepandwa kwenye shamba la mahindi kama njia ya kilimo hifadhi na kutunza unyevunyevu na rutuba ya udongo.

FAO na kilimo cha mikunde shuleni Tanzania

Nchini Tanzania, FAO inatekeleza mradi wa kilimo cha bustani za mikunde na mboga mboga shuleni ambapo wanafunzi wanaweza kupata mlo kutokana na mazao hayo.

Katika maadhimisho ya mwaka huu ya siku ya mikunde duniani, nchini Tanzania kitaifa yamefanyika mkoa wa Njombe kusini mwa taifa hilo la AFrika Mashariki ambako FAO imefika kujionea maendeleo ya mradi huo.

Idhaa ya Kiswahili ilipata fursa ya kuzungumza na baadhi ya wanufaka wakiwemo wanafunzi na walimu ambao walielezea manufaa kuwa ni pamoja na lishe na vile vile kupunguza utoro shuleni kwani watoto wanapata chakula badala ya kwenda shuleni.

Mathalani katika shule ya msingi ya Itipingi katika halmashauri ya wilaya ya Njombe, wanafunzi wamesema mpango wa bustani za mboga na mikunde ni mkombozi kwani sasa wanakula shuleni badala ya kupoteza muda wa mchana kwenda kula nyumbani.