Ama hakika mikunde imenusuru vijana Tanzania

Theodosia Peter ambaye ni mnufaika wa mradi wa FAO huko Kigoma, Tanzania akikausha maharage  yake aliyovuna shambani.
FAO Tanzania
Theodosia Peter ambaye ni mnufaika wa mradi wa FAO huko Kigoma, Tanzania akikausha maharage yake aliyovuna shambani.

Ama hakika mikunde imenusuru vijana Tanzania

Ukuaji wa Kiuchumi

Kuelekea siku ya kimataifa ya mikunde kesho tarehe 10 ya mwezi Februari, tunafunga safari hadi Kigoma nchini Tanzania ambako huko Umoja wa Mataifa kupitia shirika lake la chakula na kilimo, FAO, umeanza kutekeleza kwa vitendo dhana ya kutumia mikunde siyo tu kwa ajili ya chakula bali pia kwa kilimo hai kisichoharibu udongo.
 

Maudhui ya mwaka huu ni “mikunde na uwezeshaji wa vijana katika kufanikisha mifumo endelevu ya kilimo.” Kwa umoja wa Mataifa, mifumo endelevu ya kilimo ni ile ambayo inakidhi mahitaji ya jamii, uchumi, na mazingira kwa kipindi kirefu bila kuharibu mazingira. 

Mathalani matumizi ya mikunde katika kuongeza rutuba ya ardhi badala ya kutumia mbolea zenye kemikali. Halikadhalika kupatia jamii kipato. Faida hizi tayari zimeanza kuonekana nchini Tanzania ambako shirika la Umoja wa Mataifa la chakula na kilimo FAO kupitia mradi wa pamoja wa Kigoma, KJP, limetoa mafunzo ya kilimo bora kwa vijana huko wilayani Kibondo na sasa vijana hao wanajivunia kwani mashambani wamevuna na vipato vinaingia mfukoni

Miongoni mwa vijana hao ni Isidory Germanus ambaye baada ya kupatiwa mafunzo na FAO, chini ya mradi wa pamoja wa Kigoma, KJP,  juu ya mbinu bora za kilimo ikiwemo matumizi ya mbegu bora, Isidori sasa amejikita katika kilimo cha maharage na hivi sasa ana heka kadhaa za zao la maharage.

“Maharage yanatupatia ajira sisi vijana maana tunajikita katika shughuli za Kilimo,” ameeleza Isidori Germanus. 

Wanawake wakipalilia kwenye moja ya mashamba darasa ya mahindi na maharagwe chini ya mpango wa pamoja mashirika ya Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Kigoma, KJP.
UN News/Assumpta Massoi
Wanawake wakipalilia kwenye moja ya mashamba darasa ya mahindi na maharagwe chini ya mpango wa pamoja mashirika ya Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Kigoma, KJP.

Aina za mikunde na mifumo endelevu ya kilimo

Umoja wa Mataifa unaweka bayana kuwa kuna aina mbalimbali za mikunde ikiwemo maharage, choroko, kunde zenyewe, njugu mawe, mbaazi na njegere.

Na mifumo endelevu ya kilimo ni ile ambayo huimarisha jamii, huinua uchumi na hulinda mazingira. 
Kwa lishe, mikunde ina virutubisho na kiwango cha juu cha protini na hivyo kuifanya kuwa chanzo kizuri cha protini hasa kwenye maeneo ambako protini ya nyama na maziwa si rahisi kupatikana.
Mikunde ina kiwango kidogo cha mafuta lakini ina kiwango cha juu cha makapimlo na hivoy kusaidia kudhibiti kiwango cha sukari mwilini.

Mikunde pia inatoa hakikisho la upatikanaji wa chakula kwa kuwa unaweza kuuza na pia kula na hivyo kuwezesha wakulima kuwa na chakula na wakati huo huo wanaweza kuuza na kujipatia kipato.

Mikunde na mazingira

Na faida nyingine ya mikunde ni katika mazingira kwa kuwa hurutubisha udongo na hivyo kuongeza muda wa matumizi ya shamba. Kwa kuchanganya mikunde na mazao mengine kama vile mahindi, mkiulma anaongeza bayonuai shambani na kufukuza wadudu waharibifu. Na kutokana na uwezo wake wa kurutubisha udongo, mikunde inapunguza utegemezi wa mbolea za madukani.

Faida zote hizo zilifungua fikra za Isidory na sasa ana heka kadhaa za zao la maharage na anaona amepata faida akisema, “kwanza kabisa kipato, mimi kama kijana nimeanz akupata kipato ingawa kuna changamoto kama  vile ukosefu wa soko la uhakika, visumbufu vya mazao. Lakini pia kwa upande wa maharage ya Jesca yana virutubisho vya kutosha kwa wazee, wajawazito na watoto, kwa hiyo watu wanapenda sana kuyanunua. Pia niwashauri vijana wenzangu tujikite kwa kulima kwa kutumia mbinu bora za kilimo, kwa sababu sisi ambao tumepata mafunzo tayari tunaweza kuwapatia wengine elimu kama  hii kwa sababu kipato kinaongezeka. Lakini nategemea kuongeza shamba, nashukuru sana FAO.”

Akifurahia kilimo cha maharage Shadrack Kipeya toka kijiji cha Kumkugwa wilayani Kibondo alikiri kwamba zao la maharage limempatia manufaa makubwa ikiwemo chakula na kipato akisema. “ kwa kweli mazao ya mikunde ni mazuri kwa sababu kwanza ni mazao  ya muda mfupi, miezi mitatu yanaweza kumkomboa kijana. Unaweza kulima mara mbili kwa mwaka. Kimsingi mazao haya yamenufaisha watu wengi, unaona wamejenga nyumba nzuri na yanaepusha watu kufanya mambo mabaya. Kwa ujumla mazao haya ni mazuri, unaweza kupanda na kuvuna na kuamua wakati wa kuuza au kuhifadhi.”

Mafunzo pia yaliwezesha vijana kujifunza sio tu uzalishaji bali pia uchambuaji wa zao la maharage kwa hali ya juu hivyo kumfikia mlaji likiwa na ubora na yeyé kujipatia kipato zaidi.
“Mbali na chakula, maharage pia hurutubisha ardhi pindi yanapovunwa kwani eneo lililotumika kuzalisha maharage huwa na rutuba zaidi kwa zao lingine hususani mahindi kwa msimu unaofuata,”alikiri Bwana Fulgency Dogo toka kijiji cha mvugwe aliyefika kujifunza zaidi kwa shemeji yake Shadrack akiongeza kuwa kando ya mbolea, anaweza kuuza hadi kibondo mjini na kupata faida.