Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nyama ikiingia mezani, mikunde hunyanyapaliwa- FAO

Mkoani Njombe kusini mwa Tanzania, mapishi mbalimbali kutokana na matumizi ya mikunde. Hii inafuatia mafunzo yaliyowezeshwa na FAO na AgriConnect.
FAO Tanzania
Mkoani Njombe kusini mwa Tanzania, mapishi mbalimbali kutokana na matumizi ya mikunde. Hii inafuatia mafunzo yaliyowezeshwa na FAO na AgriConnect.

Nyama ikiingia mezani, mikunde hunyanyapaliwa- FAO

Afya

Jamii ya mikunde! Wengi wanaitambua zaidi kama ni kunde zenyewe, na maharagwe lakini ni zaidi ya hiyo. Kuna choroko, mbaazi, dengu, njegere na kadha wa kadha ambapo kutokana na umuhimu wake sio tu kiuchumi bali pia katika lishe ya binadamu, kurutubisha udongo na pia kuhimili mabadiliko ya tabianchi, ndio maana Umoja wa Mataifa unapigia chepuo.

Tweet URL

Mathalani nchini Tanzania, shirika la Umoja wa Mataifa la chakula na kilimo, FAO linafadhili mradi wa AgriConnect ambao pamoja na mambo mengine  unapatia wananchi; wanawake na wanaume stadi za mapishi sahihi ya jamii ya mikunde.

Tathmini ya ulaji wa mikunde Tanzania

Afisa lishe wa FAO nchini Tanzania Stella Kimambo amenukuliwa hivi karibuni huko mkoani Njombe nchini Tanzania akisema “vyakula vya jamii ya mikunde huondoka mezani pale nyama inapoonekana, vinanyanyapaliwa.”

Na kama hiyo haitoshi idadi kubwa ya watanzania hula zaidi maharage lakini mikunde kama vile mbaazi, dengu na choroko havipati nafasi mezani.

Ulaji uko chini lakini uuzaji mikunde nje ya nchi unashamiri

Bi. Kimambo anasema ingawa ulaji wa aina mbalimbali za mikunde uko chini, bado Tanzania ni mzalishaji muhimu wa mikunde na kwamba mwaka 2022 Tanzania iliuza nje ya nchi mazao ya jamii ya mikunde yenye thamani ya dola milioni 266 kutoka dola milioni 198 mwaka 2020. Takribani asilimia 85 ya mazao hayo yanaelekea India.

Magreth Natai  afisa lishe kutoka Wizara ya kilimo Tanzania anaelezea juu ya umuhimu wa mazao jamii ya mikunde akisema mazao ya mikunde kama njegere, mbaazi, choroko, kunde ni mazao ambayo yana umuhimu mkubwa kilishe, kiuchumi na kimazingira kwa maana tunajua mikunde inarutubisha udongo.”

Hivyo amesema wataendelea kushirikisha wananchi kutambua umuhimu huo ikiwemo kwa lishe.

Mikunde iliyozoeleka ni maharage lakini FAO inasema kuna aina nyingi ya mikunde kama ilivyo pichani kwa hiyo inataka mlo unaofika mezani uwe na jamii zote za mikunde.
FAO Tanzania
Mikunde iliyozoeleka ni maharage lakini FAO inasema kuna aina nyingi ya mikunde kama ilivyo pichani kwa hiyo inataka mlo unaofika mezani uwe na jamii zote za mikunde.

Harakati za kuchagiza ulaji wa mikunde

Ili kushamirisha ulaji wa mazao ya jamii ya mikunde hapa nchini, FAO inaunga mkono mradi wa AGRICONNECT, mradi unaochagiza sio tu kuongeza mnyororo wa thamani wa mazao hasa nyanda za juu za kusini mwa Tanzania ikiwemo mkoa wa Njombe, bali pia kuhakikisha kuna uhakika wa chakula na lishe.

Mashindano ya upishi wa mazao ya mikunde yalifanyika mkoani  Njombe kusini mwa Tanzania tarehe 10 mwezi Februari mwaka huu wakati wa maadhimisho ya siku ya mikunde duniani.

Nilipika keki kwa kutumia ndizi na maharage

Esther Lukasi mpishi na mama lishe  aliibuka mshindi wa pili na akihojiwa na John Kabambala wa Redio Washirika KidsTime FM nchini Tanzania amesema, alipatiwa zawadi ya mtungi wa gesi, vijiko vikubwa vya chakula pamoja na kisu.

“Nilipika mchanganyiko wa wali na choroko, pilau la maharage, ugali wa maharage au usuge, mboga za majani na keki kwa kutumia ndizi na maharage,” amesema Bi. Lukasi.

Esther Lukasi mmoja wa washindi wa mapishi ya kutumia jamii za mikunde .Mashidano yalifanyika huko Njombe, kusini mwa Tanzania wakati wa maadhimisho ya siku ya mikunde duniani, 2023 na yalifadhiliwa na FAO na AgriConnect.
FAO Tanzania
Esther Lukasi mmoja wa washindi wa mapishi ya kutumia jamii za mikunde .Mashidano yalifanyika huko Njombe, kusini mwa Tanzania wakati wa maadhimisho ya siku ya mikunde duniani, 2023 na yalifadhiliwa na FAO na AgriConnect.

Kwa mshindi huyu wa pili, mashindano hayo yalikuwa kitu kikubwa kwake kwani hawajahi kupika vitu kama hivyo na kwamba “ninashukuru FAO kwani wamekuja kutupa mafundisho ambayo hatukufahamu hapa. Na nina furaha sana sikutegemea kushinda na nimefurahi kuwa nitaweza kupika chakula kwa urahisi nyumbani kwangu.”

Katika soko la kuu la nafaka na matunda mkoani Njombe, mazao yamesheheni lakini cha ajabu ni changamoto ya lishe miongoni mwa watoto.

Sara Mtibike mchuuzi hapa sokoni anasema changamoto ya lishe licha ya kuweko kwa vyakula ni kwamba “tumeondokana na asili, zamani wazee wetu walipika kande, maboga lakini sisi tunaona uvivu kupika kwa muda mrefu. Hivyo ni vema turejee asili ili watoto wetu waweze kuwa na lishe bora.”