Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tunataka kuwafikia waathirika wote japo kuna kikwazo cha usalama katika baadhi ya maeneo - WFP Syria

Chakula kinasambazwa kwa watu waliokimbia makazi yao baada ya tetemeko la ardhi huko Aleppo, Syria.
© Al-Ihsan Charity
Chakula kinasambazwa kwa watu waliokimbia makazi yao baada ya tetemeko la ardhi huko Aleppo, Syria.

Tunataka kuwafikia waathirika wote japo kuna kikwazo cha usalama katika baadhi ya maeneo - WFP Syria

Msaada wa Kibinadamu

Mashirika ya Umoja wa Mataifa yanaendelea kupeleka na kusambaza misaada nchini Uturuki na Syria ili kusaidia walioathiriwa na matetemeko makubwa ya ardhi yaliyotokea Jumatatu wiki hii na kujeruhi, kuua maelfu na kuharibu miundombinu. Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) lina lengo la kuwafikia watu nusu milioni katika nchi zote mbili ijapokuwa kuna changamoto za kiusalama katika baadhi ya maeneo.

Si Jindires, si Allepo, kote ni milio ya magari ya wagonjwa, majengo yameporoka, ni magofu, vilio, buludoza, harakati za uokozi na juhudi za kusambaza misaada zikiendelea.  

WFP inaharakisha msaada muhimu wa chakula kwa familia nchini Syria zilizoathiriwa na tetemeko kubwa la ardhi.
© Al-Ihsan Charity
WFP inaharakisha msaada muhimu wa chakula kwa familia nchini Syria zilizoathiriwa na tetemeko kubwa la ardhi.

WFP inasema kufikia mwishoni mwa wiki hii itakuwa imewapa wadau wake chakula cha kutosha wiki nzima kwa watu 125,000. Hali hii ya matetemeko imeikuta WFP tayari ikiwa na mzigo wa kuwahudumia  watu milioni 1.4 kila mwezi Kaskazini Magharibi mwa Syria pekee. Kenny Crossley, ni Mkurugenzi wa WFP nchini Syria, akiwa katika mji mkuu wa Syria, Damascus anasema, "Siku chache zilizopita, tetemeko la ardhi la kutisha lilitokea hapa nchini Syria na Uturuki. Mamia pengine maelfu ya waliokufa, maelfu kujeruhiwa, makumi, pengine maelfu ya watu waliokimbia makazi yao, kupoteza makazi yao, watu hawawezi kurejea katika maeneo ambayo huwa wanalala, sasa wanalala mitaani wakijibana kwenye vibanda. Kwa WFP bila shaka, kwetu ni muhimu, kwamba watu lazima wale. Saa chache tu baada ya tetemeko la ardhi, tulikuwa tukifanya kazi na wadau wetu wa eneo hilo watu walikuwa wakila chakula cha moto katika makazi ya muda waliyokuwa wakiishi.” 

Pamoja na juhudi za WFP, shirika hilo la Umoja wa Mataifa linasema matetemeko ya ardhi yamezidisha ugumu uliopo wa kufika Kaskazini Magharibi mwa Syria kutokana na migogoro na hivyo kusababisha uhitaji zaidi kama anavyofafanua Kenny Crosseley, "Moja ya changamoto zetu kubwa kwa sasa sio usafiri, sio chakula, ni ufikiaji wa maeneo. Baadhi ya watu ambao ni vigumu kuwafikia wako katika maeneo ambayo kuna migogoro inayoendelea. Tunahitaji kuwa na uwezo wa kufikia watu ambao wako katika maeneo haya ambayo kuna migogoro inayoendelea." 

Mjini Aleppo, WFP kwa haraka kupitia majiko ya wadau wake imetoa chakula cha moto kwa watu 4,000 walioathirika katika makazi ya muda. Usaidizi utaendelea hadi kesho tarehe 11 mwezi huu Februari, kulingana na tathmini zinazoendelea za mahitaji. WFP pia kupitia wadau inasambaza milo iliyo tayari kuliwa inayotosha watu 5,000 walioathirika.