Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dola bilioni 1 zasakwa kusaidia Uturuki kwa miezi 3; UN yapaza sauti

Mtoto akiwa baba yake wakisubiri mgao wa msaada kwenye makazi ya muda kusini-mashariki mwa Uturuki
© UNICEF/Özgür Ölçer
Mtoto akiwa baba yake wakisubiri mgao wa msaada kwenye makazi ya muda kusini-mashariki mwa Uturuki

Dola bilioni 1 zasakwa kusaidia Uturuki kwa miezi 3; UN yapaza sauti

Msaada wa Kibinadamu

Hii leo Umoja wa Mataifa umezindua ombi la dola bilioni 1 kwa ajili ya usaizidi wa kibinadamu kwa wananchi wa Uturuki wanaokumbwa na machungu kufuatia tetemeko kubwa zaidi la ardhi kuwahi kukumba taifa hilo katika karne.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amesema fedha hizo zitakazotumika kwa kipindi cha miezi mitatu zitasaidia watu milioni 5.2 na kuwezesha mashirika ya misaada kuimarisha kasi ya usaidizi wao kwa juhudi za serikali za kupeleka misaada kwenye maeneo kadhaa ikiwemo misaada ya chakula, ulinzi, elimu, maji na malazi.

Wakati wa kurejesha fadhila kwa Uturuki

Taarifa iliyotolewa leo jijini New York, Marekani na msemaji wa Umoja wa Mataifa, imemnukuu Katibu Mkuu Guterres akisema “Uturuki ni nyumbani kwa wakimbizi wengi zaidi duniani na kwa miaka mingi imekuwa ikionesha ukarimu wa kipekee kwa majirani zao Syria. Sasa ni wakati wa dunia kusaidia wananchi wa Uturuki kama vile ambavyo wamekuwa wakishimana na wengine wanaosaka misaada.”

Mahitaji ni mengi

Tetemeko hilo la ardhi lililopiga Uturuki na Syria Jumatatu ya wiki iliyopita, limetokea wakati wa kilele cha majira ya baridi kali, na kuacha mamia ya maelfu ya watu wakiwemo watoto na wazee bila fursa ya malazi, chakula, maji, vipasha joto na huduma za afya.

Wavulana wawili wakipita kwenye mitaa iliyosambaratishwa kwa tetemeko la ardhi huko Kahramanmaraş nchini Urutuki
© UNICEF/Özgür Ölçer
Wavulana wawili wakipita kwenye mitaa iliyosambaratishwa kwa tetemeko la ardhi huko Kahramanmaraş nchini Urutuki

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya dharura, OCHA inasema majeño 47,000 yamesambaratishwa au kuharibiwa kiasi, na maelfu ya watu wamesaka hifadhi katika makazi ya muda nchini kote Uturuki.

Shule, hospitali na huduma nyingine za msingi zimevurugwa au kuharibiwa kabisa na tetemeko hilo laardhi huku familia nyingi zimetenganishwa, mamie ya watoto wamebakia yatima au hawawezi kuunganishwa na wazazi wao.

Jumuiya ya kimataifa fadhilini ombi kwa ukamilifu

Katibu Mkuu anasema, “mahitaji ni makubwa, watu wanapitia machungu na hakuna muda wa kupoteza. Nasihi jamii ya kimataifa iongeze juhudi na kufadhili kwa ukamilifu ombi hili ili kupatia jawabu janga kubwa zaidi la kiasili kuwahi kutokea katika zama zetu.”

OCHA imesema kwa mujibu wa takwimu za serikali ya Uturuki, zaidi ya watu milioni 9 nchini Uturuki wameathiriwa na tetemeko hilo la ardhi na hadi tarehe 15 mwezi huu wa Februari, zaidi ya watu 35,000 wamethibitishwa kufariki dunia kutokana na tetemeko hilo.