UN iko pamoja na waathirika wa tetemeko la ardhi Uturuki-Antonio Guterres

25 Januari 2020

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameeleza masikitiko yake kutokana na vifo na uharibifu wa mali kutokana na tetemeko la ardhi lililotokea katika jimbo la Elazig nchini Uturuki.

Kupitia  taarifa iliyotolewa na msemaji wake jumamosi jioni mjini New York Marekani, Katibu Mkuu Guterres ametuma salamu za rambirambi kwa familia za waathirika na kwa serikali na watu wa Uturuki.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anawatakia kupona haraka wale wote waliojeruhiwa.” Imeeleza taarifa hiyo.

Aidha salamu hizo za Bwana Guterres zimeeleza kuwa Umoja wa Mataifa uko pamoja na Uturuki na wako tayari kusaidia.

Vyombo mbalimbali vya Habari vya kimataifa vimeeleza kuwa takribani watu 29 wamefariki dunia na zaidi ya watu 1,400 wamejeruhiwa katika tetemeko hilo la ardhi lililotokea mashjariki mwa Uturuki.

Tetemeko hilo lenye ukubwa wa 6.8 vipimo vya richa, limepiga katika mji wa Sivrice jimboni Elazig na kusababisha majengo kuporoka na hivyo kuwafanya watu kukimbilia mitaani.

Duru zinadai kuwa watu 43 wameokolewa ingawa wengine kama 20 wanahofiwa kuendelea kukwama katika vifusi.

Tetemeko hili limetokea Ijumaa jioni majira ya saa mbili na dakika hamsini na tano saa za Uturuki.

Taarifa zinadai nguvu ya tetemeko hilo imetetemesha pia nchi za jirani kama Syria, Lebanon na Iran.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter