Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tulinde ardhi oevu ili itusaidie kupambana na mabadiliko ya tabianchi

Picha kutoka angani ya Ardhioevu (Maktaba)
UNDP China
Picha kutoka angani ya Ardhioevu (Maktaba)

Tulinde ardhi oevu ili itusaidie kupambana na mabadiliko ya tabianchi

Tabianchi na mazingira

Leo ni siku ya ardhi oevu. Umoja wa Mataifa unapigia chepuo siku hii kama njia mojawapo ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi.

Siku hii inayoadhimishwa kila mwaka tarehe 2 Februari, inalenga kuongeza uelewa wa kimataifa kuhusu jukumu muhimu la ardhioevu kwa watu na sayari. Siku ya ardhi oevu pia inaadhimisha tarehe ya kupitishwa kwa mkataba wa ardhioevu tarehe 2 Februari 1971.

Umuhimu wa ardi oevu Ardhi oevu mara nyingi huonekana kama maeneo yenye majimaji ambayo hayafai kitu, lakini yana jukumu muhimu katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi kwani ardhi oevu hufanya kazi kama sponji ya asili, kunyonya hewa ukaa ikiwa ni mara nne zaidi ya misitu ya mvua.

Ardhi oevu pia hufyonza hewa ukaa mara 40 kwa kasi zaidi kuliko misitu ya mvua. Mkurugenzi wa Kituo cha ardhi oevu katika taasisi ya kitaifa ya ikolojia ya nchini Korea Bae-geun Lee anasema “Ardhi oevu ni nzuri sana katika kuhifadhi na kufyonza hewa ukaa na methane, kwa hivyo sasa tunakadiria kwamba uwepo wake, unasaidia kudhibiti takriban asilimia 35 ya kaboni iliyopo kwenye sayari.”

Kwa bahati mbaya, maeneo oevu yanatoweka kwa kasi ya kutisha ndio maana katika kuadhimisha siku hii Umoja wa Mataifa unahimiza kila mtu kuchukua hatua sasa ili kulinda mifumo hii muhimu ya ikolojia kabla hatujachelewa.

Mwanamke akipanda mikoko Timor Leste ili kufufua mfumo wa viumbe hai ulioharibiwa ufukweni mwa bahari
UNDP/Yuichi Ishida
Mwanamke akipanda mikoko Timor Leste ili kufufua mfumo wa viumbe hai ulioharibiwa ufukweni mwa bahari

Uharibifu wa ardhi oevu Ardhi oevu yenye mimea, kama vile vinamasi na mabwawa, ni baadhi ya mifumo ya ikolojia yenye utajiri mkubwa wa wanyamapori kwenye sayari.

Maji yao ya kina kifupi yana maisha tele ya mimea inayotegemea kila kitu kutoka kwa wadudu, bata hadi kongoni. Lakini maeneo haya oevu, pamoja na maziwa, mito na mazingira mengine yenye maji mengi duniani, yamo hatarini, na mengi yamechafuliwa au kuharibiwa kutokana na mabadiliko ya tabianchi na maendeleo ya binadamu.

Takriban asilimia 35 ya maeneo oevu duniani, ambayo pia hupunguza athari za mafuriko na kusafisha maji machafu, yalipotea kati ya 1970 na 2015. Na kiwango cha hasara kimekuwa kikiongezeka tangu 2000.

Kulingana na kupanda kwa kiwango cha kina cha bahari kunaosababishwa na changamoto za mabadiliko ya tabianchi, asilimia 20-90 ya ardhi oevu ya sasa ya pwani, ambayo inachukua kaboni hadi mara 55 kwa kasi zaidi kuliko misitu ya mvua ya kitropiki, inaweza kupotea mwishoni mwa karne hii.

Udhibiti unaendelea Nchi zote ulimwenguni sasa zimeanza kurejesha ardhi oevu. Mifano ya mipango ya uhifadhi wa ardhioevu ni pamoja na maendeleo ya miji inayochipukia ya sifongo nchini Uchina, na urejeshaji unaoungwa mkono na serikali wa Great North Bog ya Uingereza, ambalo ni eneo muhimu la kuhifadhi kaboni na maji.

Mkuu wa idara ya Majini na Maji Safi katika Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira UNEP Leticia Carvalho, amesema kulingana na na Muongo wa Umoja wa Mataifa wa Urejeshaji wa Mifumo ya ikolojia, ni lazima nchi zisitishe sera na ruzuku zinazochochea ukataji miti na uharibifu wa ardhi oevu kutoka chanzo hadi bahari na kuendeleza urejeshwaji wao wa haraka.

"Wakati huo huo, ni lazima tuongoze na kuendesha uwekezaji ili kulinda mifumo ya ikolojia inayopewa kipaumbele, kama vile peatlands, na kuhimiza sekta binafsi kujitolea katika kudhibiti ukataji wa miti pamoja na minyororo ya usambazaji isiyo na mifereji ya maji," amesema Bi.Carvalho.

Ardhi oevu ni vituo muhimu kwa ndege wanaohama, ambao pia wamepoteza viumbe hai zaidi kuliko mifumo mingine ya ikolojia ya nchi kavu na baharini.