Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nchi 6 zaibuka na mpango mkubwa zaidi duniani wa kurejesha mito, maziwa na maeneo oevu

Mabwawa  ya samaki huko Yangambi, karibu na Kisangani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo
CIFOR/Alex Fassio
Mabwawa ya samaki huko Yangambi, karibu na Kisangani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo

Nchi 6 zaibuka na mpango mkubwa zaidi duniani wa kurejesha mito, maziwa na maeneo oevu

Tabianchi na mazingira

Hii leo jijini New York, Marekani wakati mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu maji ukiendelea, Colombia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Ecuador, Gabon, Mexico na Zambia zimezindua changamoto ya kurejesha hali ya mito, maziwa na maeneo oevu ambayo yameharibiwa kutokana na mabadiliko ya tabianchi.

Taarifa iliyotolewa na shirika la Umoja wa Mataifa la mazingira duniani, UNEP jijini New York, Marekani imesema mpango huo unaonekana kuwa hatua hiyo ni  muhimu kwa mito, maziwa na maeneo oevu kutokana na umuhimu wao mkubwa katika kutatua majanga ya maji, tabianchi na mazingira yanayoshamiri kila uchao.

Lengo ni kwamba ifikapo mwaka 2030 kilometa 300,000 za mito, sawa na kuzunguka dunia mara 7, halikadhalika ekari milioni 350 za maeneo oevu, ukubwa ambao ni zaidi ya eneo la India ziwe zimerejeshwa.

Faida za mito, maziwa na maeneo oevu

Taarifa hiyo inasema pamoja na kuwa vyanzo vya maji, mifumo anuai ya maji iliyo na afya ina faida lukuki kwa watu na mazingira na ni muhimu katika kupunguza athari na kuhimili mabadiliko ya tabianchi, na zaidi ya yote kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu, SDGs.

Licha ya umuhimu huo, theluthi moja ya maeneo oevu duniani imetoweka katika kipindi cha miaka 50 iliyoptia na bado na bado inaendelea kutoweka kwa kasi kubwa kuliko hata misitu inavyotoweka.

Mito na maziwa nayo ndio imeharibiwa zaidi duniani huku idadi ya samaki ambao wanategemewa zaidi katika uhakika wa chakula ikiwa hatarini kutoweka.

Mkulima akipanda mboga kwenye moja ya maeneo oevu nchini Guinea-Bissau
UN News/Alexandre Soares
Mkulima akipanda mboga kwenye moja ya maeneo oevu nchini Guinea-Bissau

Sasa serikali zifanye nini?

Mpango huu unataka serikali zote ziweka ahadi zenye malengo ya wazi katika mikakati yao ya kitaifa ya bayonuai, michango ya kitaifa ya kukabili mabadiliko ya tabianchi, NDCs na mikakati ya kitaifa ya utekelezaji wa SDGs ili hatimaye kurejesna maji yaliyo safi kwenye mito, maziwa.

Inger Andersen, Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP amesema “mito, maziwa na maeneo oevu yenye afya ni msingi wa jamii na uchumi, lakini mara nyingi hupuuzwa na thamani haionekani. Na hii ndio inafanya mpango huu wa serikali za Colombia, DRC,  Ecuador, Gabon, Mexico na Zambia kuwa wa muhimu sana. Wakati nchi zimeahidi kurejesha ekari bilioni 1 ya ardhi, Changamoto hii ya kurejesha mito na maziwa na maeneo oevu ni hatua ya kwanza muhimu ya kurejesha tena mifumo anuai ya maji hayo yasiyo na chumvi.”

Maeneo yapi yatapatiwa kipaumbele?

Mpango huu utajikita katika kupatia ushahidi unaotakiwa nan chi ili kubuni kwa ufanisi na kutekeleza mikakati ya kurejesha mito, maziwa na maeneo oevu, halikadhalika kubaini maeneo ya kipaumbele ya kurejesha na wakati huo huo kuweka taarifa mpya kwenye mipango ya kitaifa huku zikimasisha uchangishaji fedha na kutekeleza mipango yao.

Wafadhali ni pamoja na Muongo wa UN wa urejeshaji wa mifumo anuai, Sekretarieti ya Mkataba wa kimataifa wa maeneo oevu, WWF, IUCN, Uhifadhi wa Mazingira au The Nature Conservancy, Wetlands International na ABinBev.