Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tulinde maeneo oevu kwani yana manufaa kiuchumi na kijamii- Urrego

Mkulima akipanda mboga kwenye moja ya maeneo oevu nchini Guinea-Bissau
UN News/Alexandre Soares
Mkulima akipanda mboga kwenye moja ya maeneo oevu nchini Guinea-Bissau

Tulinde maeneo oevu kwani yana manufaa kiuchumi na kijamii- Urrego

Tabianchi na mazingira

Leo ni siku ya kimataifa ya maeneo oevu ambapo Katibu Mkuu wa Mkataba wa Kimataifa wa maeneo oevu uitwao RAMSAR, Martha Rojas Urrego amesema maeneo oevu yanasalia kuwa ni maeneo muhimu ya kufanikisha ajenda ya pamoja kuhusu bayonuai, mabadiliko ya tabianchi na maendeleo endelevu.
 

Katika ujumbe wake wa siku hii ambayo ni ni mara ya kwanza kuadhimishwa tangu Baraza Kuu lipitishe azimio mwezi Agosti mwaka jana, Bi. Urrego amesema, “toleo maalum lililozinduliwa hivi karibuni kuhusu hali ya maeneo oevu duniani linaonesha dhahiri fursa za aina yake zitokanazo na maeneo oevu iwapo maeneo hayo yatalindwa kwa hatua sahihi.”

Amesema ni dhahiri kuwa maeneo oevu ni mifumo ya anuwai iliyo thabiti zaidi katika kukabili hatari za mabadiliko ya tabianchi. Ametolea mfano wa maeneo ambako mikoko inaoteshwa akisema ni fanisi zaidi katika kufyonza hewa ya ukaa. “maeneo kama hayo huhifadhi mara mbili zaidi ya hewa ya ukaa kuliko ile inayofyonzwa na misitu.”

Ametolea mfano wa nchi kama vile Seychelles, Costa Rica, Indonesia na Uingereza ambako amesema tayari zinaonesha njia kwa kujumuisha maeneo oevu katika michango yao ya kitaifa ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Maeneo oevu pia yana mchango kiuchumi, afya na ustawi wa binadamu

Bi. Urrego amesema maeneo oevu kama vile maziwa, mito na vijito hupatia binadamu vyanzo vya maji safi sambamba na kufanikisha shughuli za uchumi na pia kuendeleza ubora wa maji. “Kwa kufyonza na kuhifadhi maji, maeneo oevu pia yanasaidia kupunguza uwezekano wa mafuriko iwapo kuna mvua kubwa na pia wakati wa majira ya ukame huwa vyanzo vya maji na kuepusha ukame.”

Amegusia pia bahari safi na ukanda oevu wa pwani kama vile miamba ya matumbawe, na maeneo oevu kulikopandwa mikoko akisema husaidia kuepusha jamii za pwani kukumbwa na vimbunga na hali za kupitiliza za hewa.

Ametoa mfano wa Senegal amnako hatua zinaendelea hivi saa kurejesha eka 45, 000 za mikoko ambazo zitalinda jamii dhidi ya vimbunga, sambamba na kupata tani hadi 18,000 za samaki kwa mwaka na kufyonza tani 500,000 za hewa ya ukaa katika kipindi cha miaka 20 ijayo.

Mkataba wa Ramsar ulipitishwa nchini Iran katika mji wa Ramsar mwaka 1971.