Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ujumuishi na uwekezaji kwenye ujenzi wa amani ni muarobaini wa amani ya kudumu

Wanafunzi hushiriki katika shughuli ya kuongeza ufahamu kuhusu ujenzi wa amani, kwa msaada kutoka kwa mpango wa Kujifunza kwa Amani wa UNICEF.
© UNICEF
Wanafunzi hushiriki katika shughuli ya kuongeza ufahamu kuhusu ujenzi wa amani, kwa msaada kutoka kwa mpango wa Kujifunza kwa Amani wa UNICEF.

Ujumuishi na uwekezaji kwenye ujenzi wa amani ni muarobaini wa amani ya kudumu

Amani na Usalama

Hii leo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limekuwa na mjadala wa wazi kuhusu Ujenzi wa amani na Uendelevu wa amani  hususan kuwekeza katika watu ili kujenga mnepo dhidi ya changamoto kubwa ambapo Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina J. Mohammed amependekeza kwa Baraza hilo mambo manne ya kuwezesha kujenga na kuendeleza amani kwa misingi ya ujumuishi na maendeleo endelevu. 

Akihutubia Baraza hilo Bi. Mohammed ametaja mambo hayo kuwa ni; mosi, uelewa wa pamoja wa amani na njia zake; pili, ujumuishi; tatu matumizi ya mifumo ya UN ya  ujenzi wa amani na nne uwekezaji katika ujenzi wa amani. 

Mambo manne ya kujenga amani na kudumu

Amesema mambo hayo manne ni muhimu kwa kuzingatia kuwa amani ambalo ni msingi wa uwepo wa Umoja wa Mataifa hivi sasa inayoyoma, wakazi wa dunia wakiwa wanakumbwa na mizozo huku wananchi katika nchi 6 kati ya 7 wakiwa wana hofu kuhusu usalama wao. 

“Dunia inakabiliwa na idadi kubwa ya mizozo ya vita kuwahi kushuhudiwa tangu Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Watu bilioni 2, sawa na robo ya wakazi wote bilioni 8 duniani wanaishi kwenye maeneo yenye mizozo. Hii inasababisha machungu ya binadamu iwe moja kwa moja au la na kuongeza umaskini na ukosefu wa uhakika wa chakula na kupunguza huduma za elimu na afya,” amesema hali hiyo inaweka shinikizo kwa uwezo wa watu kufikia ustawi wao na kuchangia kwenye  jamii. 

Naibu Katibu Mkuu amerejelea maneno ya Katibu Mkuu Antonio Guterres kuwa “dunia iko katika kipindi chenye kiza katika historia,” na hivyo kufikiria upya juhudi za kuelekea katika maendeleo endelevu ni jambo muhimu zaidi.  

Amesema kuna njia moja pekee kuelekea amani ya kudummu, amani ambayo inahimili na kukabili majanga ya zama za sasa na amani hiyo ni maendeleo endelevu. 

Uelewa wa pamoja kuhusu amani na mwelekeo wake 

Juhudi za kufanikisha amani lazima zizingatie uelewa wa pamoja kuhusu amani nan jia zake, amesema Naibu Katibu Mkuu akikumbusha kuwa mashauriano ya Ripoti ya Ajenda yetu ya Pamoja ya Katibu Mkuu yanayofanyika mwaka huu wa 2023 wakati wa maandalizi ya mkutano wa viongozi kuhusu Malengo ya Maendeleo Endelevu, SDGs na ule wa viongozi kuhusu mustakabali ujao inafungua fursa ya kubadilisha zaidi mawazo ya uelew wa mbinu au njia za kufanikisha amani. 

Amesema Ajenda Mpya ya Amani itatoa fursa ya kipekee ya kuumba dira ya pamoja ya jinsi nchi wanachama zinashirikiana kushughulikia changamoto na kutekeleza ahadi yao wakati wa azimio la miaka 75 ya UN ya kwamba “Tutasongesha amani na kuepusha mizozo.” 

Amekumbusha kuwa hakuna nchi iliyo na kinga dhidi ya ghasia na hivyo kila serikali lazima ijiandae kuchukua hatua kushughulikia changamoto na kuepusha ghasia. 

Wanawake wakihudhuria masomo ya kujifunza kusoma na kuandika huko Umm al Khairat nchiin Sudan
PBF Secretariat in Sudan
Wanawake wakihudhuria masomo ya kujifunza kusoma na kuandika huko Umm al Khairat nchiin Sudan

Ujumuishaji katika harakati za ujenzi wa amani 

Naibu Katibu Mkuu amesema kuwekeza katika ujumuishaji sio tu ni haki bali pia ni jambo la busara.

“Ujumuishaji unafanikisha pia umma kuunga mkono Zaidi harakati na pia harakati husika kupata uhalali. Kunaimarisha mnepo wa  jamii na kutatua ukosefu wa usawa mambo ambayo ni vichocheo vikubwa vya mizozo yenye mapigano.” 

Amesisitiza kuwa ujumuishi unatatua ukosefu wa usawa kwenye jinsia akitolea mfano huko Afghanistan ambako amesema wakati wa ziara yake alipatia mamlaka zilizojisimika zenyewe uongozi ya kwamba “jamii iliyojengwa kwa misingi ya uenguaji wengine na ukandamizaji katu haiwezi kustawi.” 

Ni kwa mantiki hiyo amesema  ujumuishaji wanawake pamoja na vijana kwenye ujenzi wa amani ni suala la msingi akirejelea azimio namba 2250 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linalotambua nafasi ya vijana katika kusongesha amani, ulinzi na utulivu duniani. 

“Uzuiaji na  utatuzi wa mizozo lazima ufanyike kupitia michakato jumuishi inayohusisha uongozi wa wanawake na vijana na kuakisi vipaumbele vyao.” 

Mifumo ya UN ya ujenzi wa amani 

Katika kipengele hiki cha tatu, Bi. Mohammed amegusia umuhimu wa kuchambua mifumo ya ujenzi wa amani ya Umoja wa Mataifa, hasa kwa Baraza kuangalia ni vipi linaweza kutumia vema ushauri kutoka Kamisheni ya UN ya Ujenzi wa Amani. 

“Kamisheni ya UN ya Ujenzi wa Amani inajenga ubia muhimu na majawabu ya pamoja dhidi ya vitisho vya amani na usalama, ikiwa inaweka mizani ya dhima muhimu ya kazi ile inayofanywa na Baraza. Halikadhalika inatoa mahitaji mahsusi ya kitaifa na kikanda ikiwemo Jamhuri ya Afrika ya Kati, Colombia, Ukanda wa Maziwa Makuu, Afrika Magharibi na Sahel.” 

Amesihi Baraza litumie vyema Kamisheni hiyo ili kujumuisha vema mikakati yake ya kuzuia na kujenga amani kupitia kazi ya Kamisheni. 

Mfuko wa Ujenzi wa Amani unasaidia shughuli za kuzuia unyanyasaji unaohusiana na uchaguzi na kisiasa, hasa dhidi ya wanawake, nchini Haiti.
© UNICEF/Roger LeMoyne
Mfuko wa Ujenzi wa Amani unasaidia shughuli za kuzuia unyanyasaji unaohusiana na uchaguzi na kisiasa, hasa dhidi ya wanawake, nchini Haiti.

Uwekezaji katika ujenzi wa amani 

Ametaja kipengele cha nne kuwa ni uwekezaji katika ujenzi wa amani akisema “mafanikio ya jitihada zetu za pamoja za kusongesha amani endelevu duniani yatategemea uwekezaji wa kutosha katika ujenzi wa amani.” 

Amesema anatiwa moyo sana na hatua ya Baraza Kuu la UN kupitisha kwa kauli moja mwezi Septemba mwaka jana wa 2022 azimio la Ufadhili wa ujenzi wa amani, azimio ambalo linasisitiza umuhimu wa uwekezaji wa kifedha, kisiasa na kiutendaji ili kuzuia na kujenga amani na hatimaye aman iwe ya kudumu. 

Amesisitiza kuwa mfuko huo wa Katibu Mkuu unasalia kuwa mbinu ongozi katika kuwekeza kwenye ujenzi wa amani na uzuiaji wa mizozo kwa ubia na mfumo  mzima wa Umoja wa Mataifa na mamlaka za kitaifa kwa hiyo, “hatuwezi kuruhusu majanga ambayo ni mengi, yatusababishe tuelekeze fedha huko badala ya kuelekeza kwenye juhudi zetu hizi za msingi za kuyazuia.”