Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Balozi Mulamula miongoni mwa washauri 10 wa mfuko wa ujenzi wa amani wa UN

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres
UN Photo/Manuel Elías
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres

Balozi Mulamula miongoni mwa washauri 10 wa mfuko wa ujenzi wa amani wa UN

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres Alhamisi wiki hii ameteua na kutangaza jopo la wajumbe 10 watakaokuwa washauri wake wa mfuko wa ujenzi wa amani na miongoni mwao ni balozi mstaafu kutoka Tanzania.

 

Mfuko wa ujenzi wa amani wa Umoja wa Mataifa ni chombo cha kifedha cha shirika ambacho ni kimbilio la kwanza katika kuhakikisha amani endelevu katika nchi na hali zilizo hatarini au zilizoathirika na machafuko.

Kupitia taarifa iliyotolewa na msemaji wa Umoja wa Mataifa tangu mwaka 2006 hadi 2017 mfuko huo umeidhinisha jula ya dola milioni 772 zilizotolewa kwa nchi 41 na kuanzia mwaka 2017 hadi 2019 mfuko huo ulinyoosha mkono zaidi na kuidhinisha dola milioni 531 zilizogawanywa kwa nchi 51.

Wajumbe walioteuliwa

Kwa kuzingatia kanuni za mfuko huo wa ujenzi wa amani ulioptishwa na Baraza Kuu , Katibu Mkuu ameteua watu 10 watakaohudumu kwa kipindi cha miaka miwli akizingatia pia suala la jinsia na uwiano wa kikanda. Wajumbe hao hupendekezwa nan chi wanachama ikiwemo nchi wachangiaji wa mfuko huo.

Wajumbe hao walioteuliwa ni Bi. Anne Anderson , Balozi mstaafu kutoka Ireland, Profesa Emmanuel Asante, ambaye ni mwenyekiti wa baraza la kitaifa la amani nchini Ghana, Lise Filiatrault balozi mstaafu kutoka Canada, Bi Liberata Mulamula balozi mstaafu kutoka Tanzania.

Wengine ni Johannes Oljelund, mkurugenzi mkuu kwa ajili ya ushirikiano wa maendeleo ya kimataifa, kwenye wizara ya mambo ya nje ya Sweden, Bi Sara Pantuliano , mtendaji mkuu anayeshughulikia taasisi ya maendeleo ya nje nchini Uingereza, Bwana Stephane Rey, mkuu wa sera za amani , na naibu mkuu wa kitengo cha usalama wa binadamu kwenye idara ya serikali ya wizara ya mambo ya nje ya Uswis, Bwana Gert Rosenthal balozi msataafu kutoka Guatemala, Hanns Heinrich Shumaher balozi msataafu kutoka Ujerumani na Marriet Schuurman, mkurugenzi idara ya misaada ya kibinadamu na utulivu katika wizara ya mambo ya nje ya Uholanzi.

Janga la COVID-19

Taarifa hiyo imeongeza kuwa janga lisilotarajiwa na virusi vya corona au COVID-19 linahitaji uwekezaji endelevu katika ujenzi wa amani sasa kuliko wakati mwingine wowote .

Nchi ambazo zimeathirika na vita au zilizo katika hatari zinahitaji msaada wa kwenda sanjari na hali halisi ya mshtuko ambao unaweza kusababishwa na janga hilo .

Taarifa imeenda mbali zaidi na kusema bila amani na usalama fursa ya kupata huduma za afya na za kibinadamu itakuwa hatarini na hii ndio maana Katibu Mkuu ametoa wito wa usitishwaji wa uhasama kimataifa.

Mkakati wa mfuko huo wa ujenzi wa amani kwa mwaka 2020-2024 umeandaliwa ili kutunisha mfuko huo kwa lengo la kufikia dola bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa amani, ambalo ni lengo kubwa zaidi kwa mfuko huo hadi kufikia sasa.

Katibu Mkuu ameumia fursa hii kuwashukuru wajumbe ambao wamemaliza muda wao mwezi Machi mwaka huu kwa ushauri na msaada wao ambao umesaidia kuboresha wajibu wa mfuko huo kimataifa.