Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yatenga dola milioni 3.1 kwa ajili ya ujenzi wa amani Zimbabwe

Bendera ya Zimbabwe
UN Photo/Loey Felipe
Bendera ya Zimbabwe

UN yatenga dola milioni 3.1 kwa ajili ya ujenzi wa amani Zimbabwe

Amani na Usalama

Umoja wa Mataifa na serikali ya Zimbabwe leo wametia saini mjini Harare makubaliano ya msaada wa dola milioni 3.1 zilizotengwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kuanzisha fuko la ujenzi wa amani kwa ajili ya Zimbabwe.

Makubaliano hayo yamesainiwa na mratibu mkazi wa Umoja wa Mataifa Bishow Parajuli kwa upande wa Umoja wa Mataifa na Dkt.Misheck JM Sibanda msaidizi wa Rais kwa niaba ya serikali.

Fedha hizi ni sehemu ya mikakati wa Katibu Mkuu Antonio Guterres ya amani na demokrasia kama chombo cha kuimarisha uratibu na kutoa fursa miongoni mwa wadau wa kitaifa kuhusu masuala ya Amani, maridhiano na mabadiliko ya kiutawala.

Akizungumza katika hafla hiyo Dkt. Sibanda maesema “Msaada huu kutoka fuko la Umoja wa Mataifa la ujenzi wa amani utawezesha kuanzishwa kwa jukwaa la kitaifa kwa ajili ya mazungumzo jumuishi ambayo yataiwezesha serikali, wananchi na wadau wa maendeleo kufanya kazi pamoja katika kuunga mkono Amani endelevu, kuzuia migogoro, ukuaji wa uchumi jumuishi na maendeleo.”

Baada ya kiutia saini makubaliano hayo mratibu mkazi wa Umoja wa Mataifa Bwana.Parajuli amesema “Napenda kuchukua fursa hii kusisitiza nia ya Umoja wa Mataifa ya kusaidia serikali kutekeleza mpango wa mpito wa kurejesha utulivu ili kupiga hatua katika masuala ya katiba, Amani, kuheshiimu utawala wa sheria , usawa wa kijinsia na kulinda haki za binadamu ambavyo vyote ni muhimu sana katika kuwezesha ukuaji jumuishi na maendeleo endelevu.”

Makubaliano hayo ya mfuko wa ujunzi wa amani pia yalitiwa saini na wawakilishi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa , lile la kuhudumia watoto UNICEF, la mpango wa maendeleo UNDP na linalohusika na masuala ya wanawake UN Women.

Mfuko huo wa ujenzi wa mani utajikita katika kuchagiza ushiriki wa wanawake na vijana katika majadiliano ya kitaifa ya Amani na maridhiano, kuboresha huduma za kutatua migogoro na ulinzi wa mifumo ya kijamii kwa ajili ya wale waliotengwa na jamii zilizoko hatarini, na kusongesha juhudi za kitaifa za maridhiano kupitia utekelezaji mpango wa miaka mitano wa kitaifa wa tume ya amani na maridhiano.