Amani ndio muhimili wa kila kitu: LAJCAK

23 Aprili 2018

Masuala ya amani na usalama  ni muhimu mno kwa ajili ya maendeleo na suluhu ya pamoja. Kwa muktada huo Umoja wa Mataifa utajadili kwa kina masuala hayo kuanzia kesho Jumanne kwenye mkutano utakaofanyika makao makuu ya Umoja huo mjini New York Marekani.

Mkutano huo wa siku mbili  unalenga kujadilia mbinu za kuzuia kuzuka kwa vita badala ya hali  ya sasa ya kusughulikia kuzima vita ambavyo vimeshaanza kwa mujibu wa rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Miroslav Lajcak, ambae ndie ameitisha mkutano huo.

(SAUTI YA LAJCAK)

“Kwa sababu amani ni kitu muhimu.hakuna maendeleo yoyote au ulinzi wa haki za binadamu unaowezekana bila amani, na tunahijika kumulika suala la amani na pia uzuiaji wa migogoro kwa sababu Umoja wa Mataifa uliundwa  kwa misingi ya amani, na kipengele cha kwanza cha katiba ya Umoja wa mataifa kinagusia suala la kuokoa kizazi kijacho dhidi ya madhila ya vita.”

Mkutano huu unatarajiwa kuwa mkutano mkubwa kuwahi kufanyika wa viongozi wa mataifa na serikali pamoja na mawaziri katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa tangu mjadala mkuu wa septemba mwaka wa 2017.

Lajcak ametaja ujenzi wa amani na kudumisha amani kama mkakati wa mkutano huo. Miongoni mwa malengo ni kutathmini juhudi zilizochukuliwa  pamoja na nafasi za kuimarisha kazi za Umoja wa Mataifa kuhusu ujenzi wa amani na pia kudumisha amani hiyo.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter