Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mwanza Tanzania wavuvi wazipa kisogo karabai na kugeukia taa za sola ili kujilinda wao na mazingira

Taa za sola zinazotumiwa na wavuvi katika Ziwa Victoria Tanzania
UN NEWS/ Evarist Mapesa
Taa za sola zinazotumiwa na wavuvi katika Ziwa Victoria Tanzania

Mwanza Tanzania wavuvi wazipa kisogo karabai na kugeukia taa za sola ili kujilinda wao na mazingira

Tabianchi na mazingira

Mwaka huu wa 2022 ulitangazwa na Umoja wa Mataifa kuwa mwaka wa uvuvi wa kiwango kidogo ukilenga wavuvi wanaotumia teknolojia za kiwango cha chini, sababu ni kuwamulika na kufahamu changamoto zao na kisha kuwajengea uwezo ili uvuvi wao uwe endelevu, usioharibu mazingira na wakati huo huo wajipatie kipato. Nchini Tanzania tayari hilo linafanyika kwa ushirikiano na wadau.

Matumizi ya karabai sasa taratibu yanaanza kutoweka na badala yake taa za nishati ya jua au sola zinachukua nafasi. Je kulikoni? Na faida ni ipi hasa. Evarist Mapesa wa Radio Washirika SAUT FM ya Mwanza Tanzania amefuatilia na kuandaa mada hii.

Jijini Mwanza nchini Tanzania kando ya mwalo mkubwa zaidi wa ziwa Viktoria hapa, wavuvi wamekutana na wametoka maeneo mbalimbali ya mwambao wa ziwa hili. 

Kwa miaka mingi wavuvi hawa walitumia taa za karabai ambazo ni hatarishi kwa siyo tu maisha yao bali pia kwa viumbe hai  wanaoishi ndani ya maji,Sasa wanatumia taa za nishati ya jua ambazo ni rafiki kwao na viumbe hai

Japhet Kasibo mvuvi katika mwalo huu wa Mswahili, anaona taa za nishati ya jua zimewarahisishia katika matumizi ya kazi zao ukilinganisha na zama za matumizi ya karabai ambazo walikuwa wakizitumia kwa kipindi kirefu.

Taa za Sola
UN NEWS/ Evarist Mapesa
Taa za Sola

“hizi taa uzuri wake ni kuwa unapoenda nazo ziwani, zinamwanga ambao huwa siyo mkali sana tofauti na karabai ambayo ilikuwa na mwanga mkali, moshi na matatizo mengi, lakini hizi taa za nishati ya jua zinaturahisishia kazi”,alisema Kasibo.

“kwa karabai ulipokuwa ukitega ukimaliza lazima urudi kuishindilia lakini hizi taa ukishaziwasha zinawaka moja kwa moja mpaka muda wake ukiisha (masaa 12) ndipo zinazimika”,aliongeza Kasibo.

Taa hizi za nishati ya jua zililetwa kwa ajili ya majaribio mnamo mwaka 2015 kufuatia uhusiano wa karibu kati ya jiji la Mwanza na serikali ya Ujerumani ambayo iliona ni njia sahihi ya kupambana na uchafuzi wa mazingira hususani katika ziwa Victoria. 

Lakini haikuwa kazi rahisi kuwashawishi wavuvi hao kuachana na matumizi ya karabai ambayo yalikuwa yakichafua mazingira katika ziwa Victoria n ahata kuhatarisha afya za wavuvi waliokuwa wakifanya shughuli hiyo.

“baada ya kuzileta taa hizi,mimi mara ya kwanza niliziona hazifai lakini baadaye baada ya kuona wenzangu wakienda nazo wanaleta mboga, na mimi nikazichukua Kwenda kuzijaribu, nilipo jaribu nikaona ni nzuri, hata kama upepo unapiga, wewe una uwezo wa kurusha nanga, upepo ukitulia unaendelea na kazi yako na unaikuta taa yako ipo”,alisema Kisibo.

Taa za karabai zilimwaga mafuta kwenye maji ziwani na kuleta madhara makubwa kwa viumbe vya bahari, athari za mafuta kwenye viumbe hao wakiwemo dagaa zilikuwa ziliwaathiri walaji na hata wanunuzi wakagoma kununua. 

Lucas Kisibo ni mvuvi hapa Ziwa Viktoria aliyeifanya kazi hii kwa za zaidi  ya miaka 13 hadi sasa, anasema taa za karabai zilikuwa na athari nyingi kwao.

“karabai ilikuwa inaweza kuleta shida kwenye jeti ikilipuka inasababisha moto, na ule moto ukishika mtego kwenye mtumbwi ukichanganya na mafuta ya petrol ambayo yapo katika injini ya huo mtumbwi, lazima mpate athari ya kuripukiwa na moto, wengine wanarukia majini inapotokea hali hiyo na kupoteza maisha”,alisema Lucas.

Kwa sasa wavuvi katika katika mwalo huu wanaona faida ya ujio wa taa za nishati ya jua kwani umepunguza gharama za uendeshaji wa shughuli za uvuvi katika ziwa Victoria. 

Robert Mussa ni mvuvi na mwenyekiti wa wavuvi katika mwalo wa Mswahili anasema “ taa za solar (nishati ya jua) zimepunguza gharama za ununuzi wa mafuta ya taa ambayo tulikuwa tukitumia awali katika taa za karabai”.

“Taa za karabai zilikuwa na gharama kuliko taa za zinazotumia nishati ya jua, ambazo kwa sasa zimesaidia kupunguza gharama za matumizi kama ilivyokuwa awali wakati tunatumia karabai”,alisema Mussa.

Dagaa kutoka Ziwa Victoria
UN NEWS/ Evarist Mapesa
Dagaa kutoka Ziwa Victoria

Katibu mtendaji wa Taasisi ya Nishati Jadidifu (TAREA) kanda ya ziwa Jacob Ruhonyora amesema kuwa taa hizo za nishani jadidifu zimesaidia katka utunzaji wa mazingira kwa kudhibiti uzalishaji wa hewa ya ya ukaa iliyokuwa ikizaliswa katika ziwa Victoria.

“kulikuwa na tani 15000 za hewa carbon ambazo zilikuwa zinazalishwa katika ziwa Victoria kwa mwaka,hiyo ilikuwa ni kiasi kikubwa sana, lakini tangu kuanzishwa kwa taa hizi za nishati ya jua angalau tumepunguza kiasi hicho cha carbon katika ziwa Victoria”,amesema Ruhonyora.

“lakini pia kulikuwa na uchafuzi wa mazingira,mafuta yanamwagika ambayo yanaathiri kitoweo cha Samaki kwa walaji, na mengine yanamwagika kwenye ziwa na kuathiri mazalia ya Samaki kwasababu utakuta kuna utando wa mafuta, kwahiyo vitu vyote hivyo tumevipunguza baada ya kuanza matumizi ya taa za nishati ya jua” aliongeza Ruhonyora.