Kampeni ya Amani na Afya ya TANZBATT 9 nchini DRC yahitimishwa kwa kukabidhi jengo

Kamanda wa kikosi cha TANZBATT 9 akikata utepe kuashiria ufunguzi wa Jengo la eneo la chakula lililokabidhiwa na walinda amani wa kikosi cha 9 kutoka Tanzania, TANZBATT 9 kwa Zahanati ya Mavivi, mjini Beni, Jimboni Kivu kaskazini mashariki mwa jamhuri ya…
TANZBATT 9 / Private Sosper Msafiri
Kamanda wa kikosi cha TANZBATT 9 akikata utepe kuashiria ufunguzi wa Jengo la eneo la chakula lililokabidhiwa na walinda amani wa kikosi cha 9 kutoka Tanzania, TANZBATT 9 kwa Zahanati ya Mavivi, mjini Beni, Jimboni Kivu kaskazini mashariki mwa jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC. (Januari 16, 2023).

Kampeni ya Amani na Afya ya TANZBATT 9 nchini DRC yahitimishwa kwa kukabidhi jengo

Amani na Usalama

Kikosi cha 9 cha walinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Tanzania wanaohudumu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC kupitia Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini humo - MONUSCO wamehitimisha kampeni yao ya Afya na Amani iliyoanza tarehe 3 mwezi huu wa January ambapo  wamekabidhi jengo kwa ajili ya mahali pa wagonjwa na wahudumu wa afya kula chakula katika Kituo cha Afya cha Mavivi, mjini Beni, Jimboni Kivu Kaskazini mashariki mwa DRC.

Akikabidhi jengo hilo Kamanda wa kikosi cha tisa cha Ulinzi wa Amani kutoka Tanzania Luteni Kanali Barakael Mley amesema jengo hilo litabaki kuwa kumbukumbu ya uhusiano mzuri baina ya walinda Amani wa kikundi cha 9 na wananchi wa maeneo ya Mavivi na maeneo jirani,“katika vipaumbele ambavyo tulikuwa tumeviweka cha kwanza kabisa ilikuwa ni kuwasaidia wenzetu dawa ambalo tumeshalifanya tangu wiki iliyopita. Kingine ilikuwa ni kuhakikisha tunajenga hi nyumba. Na mengine ambayo tutayaweza kwa kadri Mungu atakavyotujalia tutaendelea kupunguza.”

Jengo kwa ajili ya eneo la chakula lililokabidhiwa na walinda amani wa kikosi cha 9 kutoka Tanzania, TANZBATT 9 kwa Zahanati ya Mavivi, mjini Beni, Jimboni Kivu kaskazini mashariki mwa jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC. (Januari 16, 2023).
TANZBATT 9 / Private Sosper Msafiri
Jengo kwa ajili ya eneo la chakula lililokabidhiwa na walinda amani wa kikosi cha 9 kutoka Tanzania, TANZBATT 9 kwa Zahanati ya Mavivi, mjini Beni, Jimboni Kivu kaskazini mashariki mwa jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC. (Januari 16, 2023).

Dkt Kasereka Nsara kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Kituo cha Afya cha Mavivi anashukuru akisema, “lilikuwa hitaji kubwa sana kwani tangu kuanzishwa kwa kituo hiki hatukuwa na mahali pa kuweka watu wakati wa kula. Hivyo walikuwa wanakula ndani ya vyumba vyao nah ii si nzuri kiafya kula chakula ambamo mgonjwa amelazwa.”

Kwa upande wake Afisa Uhusiano wa kikosi cha tisa cha Ulinzi wa amani kutoka Tanzania Kapteni Paul Mwesongo amebainisha kuwa hali ya uhusiano baina ya wananchi na walinda amani hao,“Ujenzi huu ni kuongeza chachu ya uhusiano mzuri na ushirikiano kati ya raia tunaowalinda katika maeneo ya uwajibikaji.” 

Naye Bi Kavathama Clarice, mwenyekiti wa kamati ya Afya katika kituo cha afya cha Mavivi amesema, “tukipokea wageni kutoka kutoka kambi ya MONUSCO upande wa watanzania. Wametuletea msaada kutujengea mahali pa kulia chakula. Tunashukuru waendelee wasichoke kutenda mema.”