Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mlipuko waua watu kanisani DRC, Katibu Mkuu UN asisitiza wahusika wawajibishwe

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akizungumza na waandishi wa habari New York, Marekani
UN /Eskinder Debebe
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akizungumza na waandishi wa habari New York, Marekani

Mlipuko waua watu kanisani DRC, Katibu Mkuu UN asisitiza wahusika wawajibishwe

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amelaani vikali shambulio lililotokea jana mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC wakati wa ibada ya Jumapili katika kanisa moja huko Kasindi, jimboni Kivu Kaskazini. Selina Jerobon anaarifu zaidi.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ameanza kwa kutoa pole kwa familia zilizofiwa, watu wa DRC na serikali yao na akawatakia ahueni ya haraka waliojeruhiwa katika shambulio hilo la kilipuzi kilicholipuka katikati ya misa ya jumapili.

Na kisha “Katibu Mkuu anasisitiza haja ya kuwawajibisha wahusika wa shambulio hili na anabainisha kuwa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya huduma za kutegua mabomu ya kutegwa ardhini UNMAS inasaidia mamlaka ya DRC katika kufanya uchunguzi wa mazingira ya tukio hilo.” Imeeleza taarifa hiyo iliyotolewa jijini New York, Marekani usiku wa kuamkia leo Jumatatu na Stéphane Dujarric ambaye ni Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. 

Aidha Bwana Guterres akasisitiza kwamba Umoja wa Mataifa kupitia Mwakilishi wake Maalumu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, “utaendelea kuiunga mkono Serikali ya DRC na wananchi katika juhudi zao za kuleta amani na utulivu mashariki mwa nchi hiyo.”

Kwa mjibu wa ripoti za awali, takriban raia 12 wameuawa, na wengine 50 kujeruhiwa katika shambulio hilo.


Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa Kulinda Amani nchini humo DRC, (MONUSCO) wamefanya unatoa uokoaji wa matibabu kwa waliojeruhiwa, kwa ksuhirikiana na chini ya uratibu na mamlaka ya DRC.