Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatua Madhubuti zahitajika kuusaidia Ulimwengu unaozeeka - Ripoti ya UN

Wazee wawili wakiwa wamekaa katika benchi.
Photo: World Bank/Celine Ferre
Wazee wawili wakiwa wamekaa katika benchi.

Hatua Madhubuti zahitajika kuusaidia Ulimwengu unaozeeka - Ripoti ya UN

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Kote duniani idadi ya watu wenye umri wa miaka 65 na zaidi inatarajiwa kuongezeka Zaidi ya mara mbili kutoka watu milioni 761 mwaka 2021 hadi kufikia watu bilioni 1.6 mwaka 2050 kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa ya mwasula ya kijamii duniani mwaka 2023 iliyotolewa leo na idara ya kiuchumi na masuala ya kijamii DESA. 

Ripoti hiyo imesisitiza kwamba wakati dunia ikiendelea kushughiulikia changamoto kubwa ikiwemo kupanda kwa gharama za maisha , haki za wazee na ustawi wao lazima uwe kitovu cha juhudi za kufikia mustakbali bora kwa wote. 

Maisha marefu na yenye afya huleta fursa za maendeleo 

Ripoti ya dunia ya masuala ya kijamii iliyopewa jina: “Kutomwacha mtu nyuma katika ulimwengu wa kuzeeka” inasema kwamba kuzeeka kwa idadi ya watu duniani ndio mwelekeo wa ulimwengu wa wakati wetu.  

Imeongeza kuwa duniani kote, mtoto aliyezaliwa mwaka 2021 anaweza kutarajia kuishi kwa wastani karibu miaka 25 zaidi ya mtoto mchanga aliyezaliwa mwaka 1950 na kuweza kufikia miaka 71, huku wanawake wakiishi Zaidi ya wanaume kwa wastani wa miaka mitano.  

Afŕika Kaskazini, Asia ya Maghaŕibi na Afŕika Kusini mwa Jangwa la Sahaŕa kunataŕajiwa kuwa na ongezeko la kasi zaidi la idadi ya wazee katika miongo mitatu ijayo, wakati Ulaya na Ameŕika Kaskazini kwa pamoja sasa zina idadi kubwa zaidi ya wazee.  

Kulingana na ripoti hiyo, kuboreshwa kwa huduma za afya na matibabu, upatikanaji mkubwa wa fursa za elimu na kupungua kwa uzazi kumesababisha mabadiliko haya. 

Kote duniani idadi ya watu wenye umri wa miaka 65 na zaidi inatarajiwa kuongezeka Zaidi ya mara mbili kutoka watu milioni 761 mwaka 2021 hadi kufikia watu bilioni 1.6 mwaka 2050
© UNFPA China
Kote duniani idadi ya watu wenye umri wa miaka 65 na zaidi inatarajiwa kuongezeka Zaidi ya mara mbili kutoka watu milioni 761 mwaka 2021 hadi kufikia watu bilioni 1.6 mwaka 2050

Pengo la usawa katika kuzeeka 

Li Junhua, msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya kiuchumi na kijamii amesema "Pamoja, tunaweza kushughulikia kukosekana kwa usawa leo kwa manufaa ya vizazi vya kesho, kudhibiti changamoto na kutumia fursa ambazo zinaletwa na kuzeeka kwa idadi ya watu." 

Ameongeza kuwa sio kila mtu amefaidika kwa usawa kutokana na maboresho ya afya na elimu ambayo yamechangia kuzeeka kwa idadi ya watu.  

“Ingawa wazee wengi wana afya bora au wanafanya kazi zinazochangia kiuchumi, wengine wanaishi na magonjwa au umaskini. Katika kanda zilizoendelea zaidi, mifumo ya umma, ikiwa ni pamoja na pensheni au malipo ya uzeeni na huduma za afya, hutoa zaidi ya theluthi mbili ya matumizi ya wazee. Hata hivyo, katika maeneo yenye maendeleo duni, wazee huwa na tabia ya kufanya kazi kwa muda mrefu na kutegemea zaidi mali iliyokusanywa au usaidizi wa familia.”Ameongeza bwana Junhua. 

Zaidi ya hayo, amesema matumizi ya umma katika nchi nyingi hayajatosha kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya matunzo ya muda mrefu. 

Kama ripoti inavyoonyesha, umri wa kuishi huathiriwa sana na mapato, elimu, jinsia, kabila na mahali pa kuishi, miongoni mwa mambo mengine mengi.  

Baadhi ya michanganyiko ya mambo haya ripoti inasema mara nyingi imesababisha hasara ya kimfumo ambayo huanza mapema maishani. 

Kwa mantiki hiyo ripoti inasema bila sera za kuzizuia hasara za kimfumo pengo la usawa linakuwa katika maisha yote ya watu, na hivyo kusababisha tofauti tya Maisha katika uzee, na matokeo mabaya kwa maendeleo kuelekea kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu SDG’s, ikiwa ni pamoja na SDG 10 la kuhusu kupunguza ukosefu wa usawa. 

Katia (kushoto) mwenye umri wa miaka 97 na Zoia (86), walitelekezwa na ndugu zao. Wanaishi katika nyumba ya kibinafsi ya zamani huko Stanytsia Luhanska. (Maktaba)
OCHA/Maks Levin
Katia (kushoto) mwenye umri wa miaka 97 na Zoia (86), walitelekezwa na ndugu zao. Wanaishi katika nyumba ya kibinafsi ya zamani huko Stanytsia Luhanska. (Maktaba)

Njia ya kuganga yajayo 

Kwa mujibu wa ripoti mabadiliko haya ya idadi ya watu lazima yatimizwe na kufikiria upya sera na mazoea ya muda mrefu yanayohusiana na maisha na kazi. Katika ripoti yake kuhusu “Ajenda Yetu ya Pamoja,” Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres alitoa wito wa kuwepo kwa mipango ya muda mrefu ambayo inaongeza fursa za upatikanaji wa elimu bora, huduma za afya na kazi zenye staha katika maisha yote kwa wote. 

Nchi nyingi tayari zinaanzisha fursa za muda mrefu za kujifunza, kuimarisha na kukumbatia faida ya nguvu kazi ya vizazi na vizazi, na kuanzisha mabadiliko katika umri wa kustaafu ili kushughulikia changamoto mbalimbali binafsi na mapendeleo ya kibinafsi. 

Serikali zinaweza kusawazisha bajeti huku zikiziba pengo la usawa 

Kufikiria upya mifumo ya ulinzi wa kijamii, ikijumuisha miradi ya malipo ya uzeeni muhimu imesema ripoti.  

Na kuongeza kuwa changamoto moja kuu ni kuhakikisha uendelevu wa kifedha wa mifumo yamalipo ya uzeeni ya umma wakati huo huo kuhakikisha usalama wa mapato kwa wazee wote, pamoja na wafanyikazi katika sekta ya ajira isiyo rasmi. 

Ripoti pia inasema “kupanua wigo wa nafasi za kazi zenye staha kwa wanawake na makundi mengine ambayo kijadi yametengwa na soko rasmi la ajira, huku pia tukitambua mchango mkubwa wa sekta ya isiyo rasmi ya huduma kwa uchumi rasmi, ni mambo muhimu zaidi ya kuhakikisha ukuaji endelevu na shirikishi wa uchumi katika ulimwengu unaozeeka.”