Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Manyanyaso na ukatili dhidi ya wazee vikome

Wazee ni waathirka zaid wa vita vinavyoendelea Ukraine Mashariki. Picha: IOM/UN/Volodymyr Shuvayev

Manyanyaso na ukatili dhidi ya wazee vikome

Masuala ya UM

Leo ni siku ya kimataifa ya kuelimisha umma kuhusu ukatili wanaofanyiwa wazee.

Baraza kuu la Umoja wa Mataifa lilitenga siku hii ya tarehe 15 mwezi Juni kila mwaka ili kupaza sauti za kupinga manyanyaso yanayowakuta  wazee.

Umoja wa Mataifa kupitia idara yake ya masuala ya kiuchumi na kijamii, UNDESA unasema kuwa dhuluma dhidi ya wazee huathiri haki za kiafya na za kibinadamu  za mamilioni ya wazee na hivyo basi suala hili ni lazima lipatiwe nafasi kimataifa.

Image
Kichapisho cha siku ya wazee duniani. (Picha:WHO)

 

Kwa nini suala hili linavaliwa njuga

UNDESA inasema sababu ni kwamba mataifa yote  yanatarajiwa kuona ongezeko la wazee kati ya mwaka wa 2015 na 2030 na kasi ya ongezeko itakuwa kubwa zaidi katika nchi zinazoendelea. Kwa hiyo hofu ni kwamba kwa kuwa idadi inaongezeka, vivyo hivyo idadi ya wazee wanaokumbwa na madhila na ukatili.

Je dhuluma dhidi ya wazee ni nini?

Ni tukio moja au mengi yanayoweza kumdhalilisha mzee. Vitu hivyo vinaweza kuwa kama kutochukua hatua yoyote kumhusu  mzee na hivyo kuleta kutoaminiana na ukosefu wa uaminifu huo humletea mzee maumivu au msongo wa mawazo.

UNDESA inaongeza kuwa dhuluma inaweza kuwa ya kisaikolojia, kimawazo au kimwili na wakati mwingine inaweza kuwa  ya kingono au kifedha bila kusahau kumpuuza tu mzee kwa makusudi.

Idara hiyo hiyo inasema katika baadhi ya nchi kupuuzwa huko huenda mbali zaidi na kutowajali wazee.

Ukatili kwa wazee hufanyika katika nchi zinazoinukia kiuchumi na zile zilizoendelea. Katika jamii fulani hususan barani Afrika mjane mzee wakati mwingine hulazimishwa kuolewa kwa nguvu na mtu mwingine na katika baadhi ya makabila wazee hutengwa na kushtumiwa kuwa wachawi.

 

Image
Wazee wakisaka huduma ya afya nchini Tanzania.(Picha/Idhaa ya kiswahili/Tumaini Anatory)

Ukimya juu ya ukatili dhidi ya wazee huleta shida zaidi

 Umoja wa Mataifa unasema jamii imekuwa kimya juu ya dhuluma kwa wazee na katu suala hilo limekuwa halizungumzi hadharani hadi siku za karibuni.

Ndio maana  baraza kuu la Umoja wa Mataifa, kupitia azimio nambari 66/127, likatenga siku hii ya 15 Juni kuwa siku ya kuhamasisha ulimwengu dhidi ya dhuluma kwa wazee.