Skip to main content

Azimio la kuwatendea haki wazee lakaribishwa na mtaalam huru

Wazee wakisaka huduma ya afya nchini Tanzania.(Picha/Idhaa ya kiswahili/Tumaini Anatory)

Azimio la kuwatendea haki wazee lakaribishwa na mtaalam huru

Haki za binadamu

Mtaalam huru wa Umoja wa Mataifa kuhusu kufurahia haki za binadamu za wazee, Rosa Kornfeld-Matte, amepongeza kupitishwa kwa azimio la Vienna kuhusu haki za binadamu za wazee wakati wa mkutano wa kimataifa uliofanyika tarehe 12 na 13 Novemba 2018 mjini Vienna.

Ameipongeza pia serikali ya Austria na wizara ya kazi na ustawi wa jamii ya nchi hiyo kwa uongozi bora na hatua ya kuitisha mkutano huo uliojikita katika haki za wazee.

Azimio hilo ni sehemu ya juhudi za kimataifa zinazoendelea za kuimarisha haki za wazee wakati huu kukiwa na mabadiliko makubwa katika kanda mbalimbali duniani.

Azimio hilo lilipitishwa bila kupingwa na wadau wote wakijumuisha wawakilishi wa mamlaka za serikali, jumuiya ya wanazuoni na asasi za kiraia , lakini vilevile wadau wengine wanaohusika na haki za wazee.

Rosa amesema “Azimio la Vienna ni hatua muhimu katika kuelekea kutimiza lengo la kulinda haki zaidi kwa watu wasioonekana na wasio na sauti miongoni mwa jamii ya wazee. Ni mchango mkubwa katika majadiliano yanayoendelea kuhusu masuala muhimu na ya kawaida kwa kikosi kazi cha Umoja wa Mataifa kihusucho masuala ya uzee”

Ameongeza kuwa azimio hilo pia limetambua athari za teknolojia mpya kwa wazee.Masuala ya kidijitali na nyenzo za teknolojia vinaweza kutumika kama fursa ya kuwasaidia kushikilia au kuimarisha uwezo wao na kuwawezesha kuishi kwa uhuru, kujitegemea na maisha ya utu.

Hata hivyo amesema ni lazima kuhakikisha kwamba fursa hizo hazigeuki na kuwa changamoto , lakini pia kuhakikisha kwamba wazee wote wanaweza kufaidika na teknolojia hizo mpya. Na kwa mantiki hiyo amesema ni lazima wazee wote wahusishwe katika muundo, mchakato na ufuatiliaji wa matumizi ya teknolojia hizo kwa manufaa yao.