Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uhuru wa kujieleza si tiketi ya kusambaza chuki dhidi ya watu wengine- Wataalamu

Kumekuwa na ongezeko kubwa la matumizi ya matamshi ya chuki kwenye Twitter
© Unsplash
Kumekuwa na ongezeko kubwa la matumizi ya matamshi ya chuki kwenye Twitter

Uhuru wa kujieleza si tiketi ya kusambaza chuki dhidi ya watu wengine- Wataalamu

Haki za binadamu

Ongezeko la matumizi ya neno la kibaguzi dhidi ya watu wenye asili ya Afrika kwenye mtandao wa Twitter kufuatia umiliki mpya wa kampuni hiyo unaibua hoja ya kampuni za mitandao ya kijamii kuwajibika zaidi kuhusu chuki inayoelekezwa dhidi ya watu hao, wamesema wataalamu wa Umoja wa Mataifa wa haki za binadamu. 

Kupitia taarifa yao waliyoitoa hii leo huko Geneva, Uswisi, wataalamu hao wamesema neno hilo la kiingereza linaloanza na herufi, “N” limezidi kutumika katika siku za karibuni kwenye mtandao huo. 

Serikali na makampuni ya intaneti wameshindwa kuzuia chuki mtandaoni
Unsplash/Priscilla du Preez
Serikali na makampuni ya intaneti wameshindwa kuzuia chuki mtandaoni

Kumekuweko na ongezeko la matumizi ya lugha ya chuki 

“Katika siku za mwanzo za umiliki mpya wa kampuni hiyo hivi karibuni, Mtandao wa Utafiti katika Chuo Kikuu cha Rutgers nchini Marekani umesema matumizi ya neno hilo yameongezeka kwa asilimia 500 ndani ya saa 12 ikilinganishwa na kipindi cha mmiliki aliyetangulia,” wamesema wataalamu hao. 

Wamesema ingawa Twitter ilidai kuwa takwimu hizo ziliongezeka kutokana na kampeni ya makusudi iliyoendeshwa na baadhi ya watu na kwamba hakuna fursa ya chuki, maelezo yoyote ya chuki dhidi ya watu wenye asili ya Afrika yanatia shaka kubwa na lazima hatua zichukuliwe kwa misingi ya haki za binadamu. 

Kampuni zinaruhusu matangazo ya chuki na nadharia potofu 

Wataalamu hao wamesema kauli za chuki, chuki kwa misingi ya uchechemuzi wa masuala ya uzawa, rangi na dini kwenye mitandao ya kijamii sio tu jambo linalotia hofu kwenye Twittter pekee bali pia majukwaa mengine makubwa ya mitandao ya kijamii kama vile Meta. Ingawa baadhi wanadai kutoruhusu kauli za chuki bado kuna pengo kati ya ahadi za kampuni na sera na usimamizi wake.” 

Wataalamu hao wamesema pengo hilo ni dhahiri kwani kinachoonekana ni kuthibitishwa kwa matangazo yenye uchochezi, taarifa za uongo kuhusu uchaguzi huko Facebook na maudhui yenye nadharia za kufikirika. 

Utafiti wa hivi karibuni kutoka taasisi ya Global Witness na SumOfUs umedhihirisha ni kwa vipi kampuni ya Meta inayoendesha Facebook inashindwa kuzuia matangazo ya aina hiyo. 

Wamesema licha ya Meta kuchukua hatua ya kuunda Bodi ya ufuatiliaji wa maudhui mwaka 2020, bado matokeo yake kwa sasa hayajaonekana pengine siku za usoni. 

Matamshi ya chuki, yawe ya mtandaoni au nje ya mtandao, ni tishio kwa demokrasia na haki za binadamu.
Unsplash/Dan Edge
Matamshi ya chuki, yawe ya mtandaoni au nje ya mtandao, ni tishio kwa demokrasia na haki za binadamu.

Uhuru wa kujieleza hukoma pale uhuru huo unapoibua chuki 

Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa haki za binadamu Volker Türk hivi karibuni aliandika barua ya wazi kwa Afisa Mtendaji Mkuu wa Twitter Elon Musk akisisitiza kuwa uhuru wa kujieleza si kibali cha kusambaza taarifa za uongo zenye madhara ambazo zinaleta madhara halisi duniani. 

“Alikumbusha kuwa sheria ya Haki za binadamu iko dhahiri – Uhuru wa kujieleza hukoma pale chuki inapochochea ubaguzi, uhasama au ghasia,” wamesema wataalamku hao wakiongeza kuwa mara kwa mara wanaona kusambaa kwa chuki na kauli za chuki dhidi ya watu wenye asili ya Afrika na makundi mengine sio tu vinadumaza haki zao bali pia vinajenga mipasuko mikubwa kwenye jamii. 

Wamesema kuruhusu au kuvumilia uchochezi huo kunazidi kutoa hamasa kwa watekelezaji na wakati huo huo kujenga kiwewe na shinikizo kwa jamii na watendewa. 

Wamesema mitandao ya kijamii lazima ichukue hatua kukabili machapisho na shughuli zinazochochea chuki, ubaguzi kwa mujibu wa kanuni za kimataifa za uhuru wa kujieleza. 

Maafisa watendaji wakuu wa majukwaa ya kijamii wajibikeni 

Wametoa wito kwa wakuu wa majukwa ya mitandao ya kijamii, Elon Musk, Mark Zuckerberg, Sundar Pichai, Tim Cook, na wengineo kuweka haki za binadamu, haki ya watu wa rangi mbalimbali, uwajibikaji, uwazi, uwajibikaji wa kijamii wa kampuni na maadili katika miundo yao ya biashara. 

“Tunawakumbusha kuwa uwajibikaji wa kampuni katika mfumo wa haki wa kila mtu na haki za binadamu ni wajibu mkuu wa kijamii. Kuheshimu haki za binadamu ni kwa ajili ya maslahi ya muda mrefu ya kampuni hizo na wamiliki wa hisa.” 

Wamerejelea nyaraka kama vile Mkataba wa Kimataifa wa kutokomeza aina zote za ubaguzi wa rangi, Mkataba wa kimataifa wa haki za kiraia na kisiasa na Mwongozo wa Umoja wa Mataifa wa kanuni kuhusu haki za biashara na kibinadamu wakisema zinatoa njia na mwongozo sahihi. 

“Tunasihi maafisa watendaji wakuu hao wa mitandao ya kijamii wawajibike kikamilifu na waheshimu haki za binadamu,” wametamatisha wataalamu huru hao wa Umoja wa Mataifa.