Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tafsiri ya Facebook ya ugaidi ni pana sana: Mtaalam wa UN

Mtandao wa mawasiliano. (Picha:ITU)

Tafsiri ya Facebook ya ugaidi ni pana sana: Mtaalam wa UN

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Mtaalam huru aliyeteuliwa na  baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa amemuandikia waraka mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya FaceBook, Mark Zuckerberg, kumuelezea wasiwasi wake  kuhusu tafsiri ya ugaidi iliyotolewa na kampuni ya Facebook.

Taarifa iliyotolewa leo mjini Geneva Uswisi na ofisi ya tume ya haki za binadamu,inasema  mtaalam huyo, anaehusika na kuchagiza  na kulinda haki za binadamu na haki za msingi za uhuru wakati wa kukabiliana na ugaidi, Fionnuala Ni Aolain, anaona  tafsiriya Facebook kuhusu ugaidi ni pana sana na inakosa  mtazamo wa kina wa haki za binadamu katika será za fursa na  matumizi ya mtandao huo.

Mtaalamu huyo anasema tafsiri ya Facebook inayajumuisha makundi yote yasiyo ya kiserikali kwamba , "yanatumia ghasia kutimiza malengo yake au kutumbukia katika masuala ya kigaidi.”

Matumizi ya tafsiri pana na isiyo bayana kama msingi wa kudhibiti fursa na matumizi ya mtandao wa Facebook kunaweza kusababisha utekelezaji wa kibaguzi, udhibiti wa kupindukia na kuwanyima fursa  na matumizi ya huduma za Facebook amesema Ni Aolain.

Facebook inatafsiri vyombo vya ugaidi kuwa ni “mashirika yoyote yasiyo ya kiserikali ambayo yanajihusisha katika vitendo vilivyopangwa vya ghasia dhidi ya watu au mali, kuwatishia raia, serikali au shirika la kimataifa ili kufikia malengo ya kisiasa, dini au imani.”

Sera za kampuni zinazuia magaidi kutumia huduma za Facebook, na inatumia teknolojia kuwabaini ,pia inaajiri timu inayoendelea kukua ya wafuatiliaji wanaosaidiwa na timu ya watu 200 kusaka na kuondoa taarifa zinazohusiana na ugaidi katika mtandao wake.

Aolain ameongeza kuwa “matumizi ya tafsiri hiyo ya jumla yanatia hofu hasa wakati huu ambapo serikali nyingi zinataka kunyanyasa na kukandamiza upinzani iwe kwa njia ya amani au mabavu kama magaidi.

Amesisitiza kwamba “Tafsiri hiyo inakwenda kinyume na sheria ya kimataifa ya haki za binadamu kwa kuyafanya makundi yote yaliyojihami kwa silaha ambayo si ya kiserikali na yasiyohusiana na mashirika ya kimatifa katika migogoro ni magaidi hata kama makundi hayo yanazingatia sheria za kimataifa za kibinadamu.”