Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN: Jamii nzima ikishirikiana itafanikiwa kukomesha kauli za chuki

UNESCO inasema kauli za chuki zinaongezeka duniani kote
Unsplash/Jon Tyson
UNESCO inasema kauli za chuki zinaongezeka duniani kote

UN: Jamii nzima ikishirikiana itafanikiwa kukomesha kauli za chuki

Haki za binadamu

Wakati chuki ikieneza kwa kasi ya umeme kwenye mitandao ya kijamii na "waenezaji wakubwa" wakitumia matamshi ya kuwagawanya maelfu ya watu, Umoja wa Mataifa unatoa wito kwa juhudi za pamoja za kimataifa kupambana na kauli za chuki.

Kauli za chuki huimarisha ubaguzi na unyanyapaa na mara nyingi huwalenga wanawake, wakimbizi na wahamiaji, na kundi la watu wachache katika jamii. Kauli hiziz zikiachwa bila kudhibitiwa, zinaweza hata kudhuru amani na maendeleo, kwani zinaweka misingi ya migogoro, mivutano na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.

Ili kukabiliana na wimbi la chuki linaloongezeka, Umoja wa Mataifa unaadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kukabiliana na kauli za Chuki kwa kutoa wito kwa kila mtu kufanya kazi pamoja ili kujenga ulimwengu wenye heshima na kiraia zaidi, na kuchukua hatua madhubuti kukomesha hali hii yenye sumu na uharibifu.

Suluhu ya aina yoyote lazima ilinde uhuru wa kujieleza

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres katika ujumbe wake kwa siku hii ameonya kwamba majibu potofu na ya utata kwa kauli za chuki - ikiwa ni pamoja na kupiga marufuku na kuzima mitandao - pia inaweza kukiuka haki za binadamu kwa kuzuia uhuru wa kujieleza.

Naye Kamishna Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Türk, amesema kuenea kwa sheria zinazohusiana na kauli za chuki zinazotumiwa vibaya dhidi ya waandishi wa habari na watetezi wa haki za binadamu ni karibu sawa na kuenea kwa kauli ya chuki yenyewe.

Katika ujumbe wake kuhusu Siku hiyo, Türk amesisitiza kwamba sheria pana - ambazo zinaruhusu Mataifa kudhibiti hotuba wanazoziona hazifurahishi na kutishia au kuwaweka kizuizini wale wanaohoji sera za Serikali au kuwakosoa maafisa - zinakiuka haki na kuhatarisha mijadala muhimu ya umma.

“Badala ya kuharamisha mijadalaa ambayo ni haki yao, tunahitaji Mataifa na makampuni kuchukua hatua za haraka kushughulikia uchochezi wa chuki na vurugu,” ameeleza Kamisha Türk.

Walinda amani wa UN kutoka Burundi wanaohudumu MINUSCA nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR wakielimisha jamii kuhusu jinsi ya kukabili kauli za chuki
MINUSCA
Walinda amani wa UN kutoka Burundi wanaohudumu MINUSCA nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR wakielimisha jamii kuhusu jinsi ya kukabili kauli za chuki

Hamasisheni kauli zinazopinga chuki 

Katibu Mkuu Guterres amesema katika mapambano dhidi ya kauli za chuki jamii inanguvu kubwa na “tunaweza na lazima tutoe ufahamu kuhusu hatari zake, na tufanye kazi kuzuia na kukomesha kwa namna zote za chuki”.

Ametaka utekelezaji wa Mkakati na Mpango wa Umoja wa Mataifa kuhusu Kauli za Chuki kama mfumo mpana wa shirika hilo wa kushughulikia visababishi na athari za kauli za chuki, na amebainisha kuwa ofisi na timu za shirika hilo duniani kote zinakabiliana na kauli za chuki kwa kutekeleza mipango ya utekelezaji wa ndani inayozingatia mkakati huu.

“Umoja wa Mataifa unashauriana na serikali, makampuni ya teknolojia na wengine kuhusu Kanuni za Maadili za hiari kwa uadilifu wa taarifa kwenye majukwaa ya kidijitali, yenye lengo la kupunguza kuenea kwa taarifa potofu na kauli za chuki, huku ikilinda uhuru wa kujieleza,”amesema Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa.

Akiunga mkonos suala hilo Kamishna Türk ametoa wito wa kuchukua hatua mbalimbali kuanzia kwenye mipango ya elimu na kuwekeza katika programu za kusoma na kuandika kwa dijiti hadi kusikiliza zile zenye ufanisi zaidi kwa ajili ya kukabiliana na kauli za chuki na kuyahimiza makampuni kutimiza wajibu wao wa haki za binadamu.

“Mengi zaidi yanapaswa kufanywa ili kushughulikia waenezaji wakubwa - wale maafisa na washawishi ambao sauti zao zina athari kubwa na ambao mifano yao inahamasisha maelfu ya wengine,” alisema kamishna Türk huku akihitimisha kwa kusema “Lazima tujenge mitandao na kukuza sauti zinazoweza kupunguza chuki.”