Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Muda wa kazi unaoendana na mazingira ya mtumishi unaweza kuwa na tija kwa mwajiri na mwajiriwa- ILO

Baba akimlea mtoto wake mdogo huku akiendelea kufanya kazi kutokea nyumbani huko Madagascar.
World Bank/Henitsoa Rafalia
Baba akimlea mtoto wake mdogo huku akiendelea kufanya kazi kutokea nyumbani huko Madagascar.

Muda wa kazi unaoendana na mazingira ya mtumishi unaweza kuwa na tija kwa mwajiri na mwajiriwa- ILO

Ukuaji wa Kiuchumi

Ripoti mpya ya shirika la Umoja wa Mataifa la kazi duniani, ILO imepigia chepuo mipango bunifu ya ufanyaji kazi kama ile iliyoanza kutumika kufuatia mlipuko wa janga la COVID-19 ikisema inaweza kuleta manufaa kwa uchumi, biashara na wafanyakazi. 

Ikipatiwa jina Mizania kati ya saa kazi na saa za kufurahia maisha duniani kote, ripoti imesema mipango hiyo inaweza kuongeza tija zaidi na mizania ya kazi na maisha yenye afya kwa mtumishi. 

Mizania kati ya kazi na maisha 

Ripoti inamulika mambo makuu mawili ambayo ni muda wa kazi ikiwa ni saa za kufanya kazi na mipango ya ufanyaji wa hizo kazi na mizania zaidi kati ya ufanyaji kazi au ratiba za kazi na upande wa pili athari ya mambo hayo kwenye utendaji wa biashara husika na jinsi mtumishi anaweza kuweka mizania kati ya kazi na maisha yake. 

Mipango ya utendaji kazi iliyochambuliwa kwenye ripoti hiyo na athari zake kwenye utendaji kazi na maisha ya mtumishi ni pamoja na kufanya kazi kwa zamu, kufanya kazi kwa saa nyingi mfululizo na kisha mapumziko, halikadhalika kusubiri kuitwa endapo mtumishi atahitajika. 

Ripoti ina takwimu mpya zaidi saa za kazi kabla na wakati wa janga la coronavirus">COVID-19 ambapo utafiti uliozalisha ripoti hiyo umebaini kuwa idadi kubwa ya watu wanafanya kazi kwa saa nyingi au kidogo ikilinganishwa na muda unaotakiwa kisheria wa saa 8 kwa siku au saa 40 kwa wiki. 

Zaidi ya theluthi moja ya wafanyakazi walikuwa wanafanya kazi zaidi ya saa 48 kwa wiki, ilhali mfanyakazi 1 kati ya 5 duniani kote anafanya kazi ya kibarua ya chini ya saa 35 kwa wiki. Ripoti inasema wafanyakazi kwenye sekta isiyo rasmi wako katika nafasi ya kufanya kazi kwa muda mrefu au mfupi zaidi. 

Mfanyakazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kazi duniani, ILO Susan Hayter amekuwa akifanyia kazi nyumbani kutokana na janga la Corona
ILO
Mfanyakazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kazi duniani, ILO Susan Hayter amekuwa akifanyia kazi nyumbani kutokana na janga la Corona

Mfayanyakazi akipewa chaguo anafanya kazi kwa tija zaidi 

Ripoti imeonesha ushahidi ya kwamba kumpatia mfanyakazi chaguo la jinsi ya kufanya kazi, wapi afanyie kazi na wakati gani afanya kazi kunaweza kuleta tija kwa mtumishi na mwajiri, na kwamba kudhibiti mazingira hayo kunaweza kuongeza gharama ikiwemo watumishi kuacha kazi. 

 “Kuna ushahidi wa kutosha kwamba sera zinazoweka mizania kati ya kazi na maisha ya mtumishi zina manufaa makubwa kwa kampuni na mtumishi,” imesema ripoti hiyo. 

Mwandishi kiongozi wa ripoti hiyo Jon Messenger amesema kitendo cha watumishi wengi kuamua kwa hiari kuacha kazi kimeweka mbele hoja ya mizania ya kazi na maisha kwenye masuala ya jamii na soko la ajira baada ya janga la COVID-19. 

Amesema “iwapo tutatumia baadhi ya kile tulichojifunza kutokana na janga la COVID-19 na kuangalia vyema mpangilio wa saa za kazi na urefu wake, tunaweza kuwa na mazingira ya kazi yenye maslahi kwa pande zote, kuimarisha utendaji wa kampuni na mizania ya kazi na maisha kwa mtumishi.” 

Mapendekezo ni yapi sasa ili hali iwe bora zaidi? 

ILO ina mapendekezo matano ikiwemo kutambua kuwa sheria za saa za kazi na kanuni kuhusu kiwango cha juu cha saa za kazi na likizo ni mafanikio yanayochangia kwa afya na ustawi wa jamii na hivyo visiwekwe hatarini. 

Ripoti inatanabaisha kuwa saa nyingi za kazi zinasababisha tija kidogo ilhali saa chache za kazi zinachangia tija kubwa. 

Kisha nchi zitumie uzoefu wao wakati wa kupunguza saa za kazi wakati wa janga la COVID-19 ikiwemo saa za kazi kulingana na mazingira ya mtumishi. 

Halikadhalika ripoti pia inapendekeza mpango wa mtumishi kufanya kazi kutoka eneo lolote duniani kwani unasaidia kuendeleza ajira ya mtumishi na kujenga mazingira ya mtumishi kujisimamia. Hata hivyo imeonya umakini katika mfumo huu kwa kuweka sera za kuainisha ni wakati gani mtumishi ana haki ya kutofanya kazi wakati wa saa za kazi. 

Ripoti kamili inapatikana hapa