Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mfumuko wa bei waporomosha kiwango cha ujira duniani

Mchuuzi wa matunda katika soko la Port Victoria nchini Seychelles
UN Women/Ryan Brown
Mchuuzi wa matunda katika soko la Port Victoria nchini Seychelles

Mfumuko wa bei waporomosha kiwango cha ujira duniani

Ukuaji wa Kiuchumi

Janga la mfumuko wa bei likichanganyika na kudorora kwa ukuaji wa uchumi duniani vikichochewa na vita nchini Ukraine na janga la nishati duniani kwa pamoja vinasababisha anguko la vivwango vya mishahara na ujira kwenye nchi nyingi duniani. 

Taarifa hizi ni kwa mujibu wa ripoti mpya ya shirika la Umoja wa Mataifa la kazi duniani, ILO ikiongeza kuwa janga hili linapunguza uwezo wa manunuzi wa watu wa vipato vya kati, huku kaya za kipato cha chini nazo zikiwa zimeathirika zaidi. 

Ripoti hiyo iliyotolewa leo jijini Geneva, Uswisi imepatiwa jina Ripoti ya Ujira duniani mwaka 2022-2023: Athari za mfumuko wa bei na COVID-19 kwenye ujira na uwezo wa  ununuzi. 

Kiwango kilishuka hadi hasi 

Ripoti inakadiria kuwa kiwango cha ujira duniani kimepungua kwa asilimia hasi 0.9 katika nusu ya kwanza ya mwaka huu wa 2022, ikiwa ni mara ya kwanza katika karne hii kiwango cha ujira kimekuwa hasi. 

Miongoni mwa wanachama wa kundi Tajiri la nchi 20, G20, ujira halisi ulipungua kwa asilimia hasi 2.2 (-2.2%) ilhali katika nchi 20 zinazoibuka kiuchumi, ujira halisi ulikua kwa asilimia 0.8 (0.8%) ikiwa ni pungufu kwa asilimia 2.6 (2.6%) ikilinganishwa na mwaka 2019, ambao ni mwaka mmoja kabla ya janga la COVID-19

Mfumuko wa bei umesababisha maandamano duniani 

Mkurugenzi Mkuu wa ILO Gilbert F. Houngbo anasema “majanga lukuki yanayokabili dunia yamechochea kuporomoka kwa ujira halisi. Hali hii imeweka makumi ya mamilioni ya wafanyakazi kwenye hali mbaya wakati huu wanakabiliwa na mustakabali wasiokuwa na uhakika nao.” 

Bwana Houngbo amesema ukosefu wa usawa kwenye kipato na umaskini vitaongezeka iwapo uwezo wa ununuzi kwa wale wanaopata kipato cha chini hautashughulikiwa.  

“Hii inaweza kuchochea zaidi mizozo ya kijamii duniani kote na kuporomosha lengo la kufanikisha ustawi na amani kwa wote,” amesema Mkuu huyo wa ILO. 

Vijana wa kike wakifungasha maharagwe kwenye shamba mjini Addis Ababa, Ethiopia.
© ILO/Sven Torfinn
Vijana wa kike wakifungasha maharagwe kwenye shamba mjini Addis Ababa, Ethiopia.

Mfumuko wa bei waathiri zaidi wale wa kipato cha chini 

Gharama ya maisha inaongeza shida kwa wafanyakazi waliopoteza ajira na familia zao wakati wa janga la COVID-19 na hii kwa nchi nyingi imekumba makundi ya vipato vya chini. 

Ripoti inaonesha kuwa ongezeko la mfumuko wa bei unaongeza gharama ya maisha kwa watu wa kipato cha chini. “Hii ni kwa sababu wanatumia fedha waliyonayo kugharimia huduma na bidhaa muhimu ambazo kwa kawaida huongezeka bei kuliko bidhaa zisizo za lazima.” 

Tofauti kikanda 

Ripoti hii inachambua takwimu kikanda na kitaifa ambapo kikanda inaonesha kuwa katika nusu ya kwanza yam waka 2022, mfumuko wa bei ulishamiri zaidi katika nchi za kipato cha juu kuliko nchi za kipato cha chini na kati. 

Mapendekezo kadhaa ikiwemo kuongeza kima cha chini cha mshahara 

Uchambuzi kwenye ripoti hiyo unapendekeza hatua za haraka za kisera kusaidia kuendeleza uwezo wa watu wa kipato cha chini kununua bidhaa halikadhalika kuhudumia familia zao. 

“Marekebisho ya viwango vya kima cha chini ya ujira au mshahara yanaweza kuwa mbinu Madhubuti, kwa kuzingatia kuwa asilimia 90 ya nchi wanachama wa ILO wana mfumo wa kima cha chini cha mshahara,” inapendekeza ripoti hiyo.  

Halikadhalika mazungumzo ya pande tatu: Mwajiri, mwajiriwa na vyama vya wafanyakazi, yanaweza kuweka uthabiti kwenye mjadala wa kuongeza mshahara na hivyo kufanikisha marekebisho kwenye janga laujira. 

Sera nyingine zinazoweza kulegeza madhara ya ongezeko la gharama ya maisha kwa kaya ni pamoja na zile zinazolenga makundi maalum kama vile kutoa vocha kwa kaya za kipato cha chini ili ziweze kununua bidhaa za msingi au muhimu, halikadhalika kupunguza kodi ya ongezeko la thamani, VAT, kwenye bidha hizo ili kupunguza mzigo wa mfumuko wa bei.