Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

EU-FAO kuhakikisha ahueni na maendeleo ya minyororo ya thamani ya kilimo Ukraine

Kwa wakulima wa Ukraine, vita vinavyoendelea vinamaanisha kutokuwa na uwezo wa kuuza nje mazao yao, na matarajio mabaya ya mavuno yao kuharibika katika banda.
© UNOCHA/Matteo Minasi
Kwa wakulima wa Ukraine, vita vinavyoendelea vinamaanisha kutokuwa na uwezo wa kuuza nje mazao yao, na matarajio mabaya ya mavuno yao kuharibika katika banda.

EU-FAO kuhakikisha ahueni na maendeleo ya minyororo ya thamani ya kilimo Ukraine

Amani na Usalama

Kaya za vijijini, wakulima wadogo na wafanyabiashara wadogo wa kilimo nchini Ukraine watanufaika na mradi wa dola milioni 15.5 unaofadhiliwa na Muungano  wa Ulaya (EU) na kutekelezwa na shirika la Umoja wa Mataifa la chakula na Kilimo (FAO) ili kusaidia utendakazi, uifuatiliaji na uimarishaji wa minyororo ya thamani katika kilimo, uvuvi na sekta ya misitu, na kukabiliana na hali ya wakati wa vita.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na FAO mradi huo utalenga kusaidia wazalishaji katika maeneo ya Lvivska, Ivano-Frankivska, Zakarpatska na sehemu za mkoa wa Chernivetska kwa ruzuku sawa kwa ajili ya uwekezaji wa mashambani na mnyororo wa thamani pamoja na msaada wa ugani na ushauri. 

Christian Ben Hell, meneja kwa ajili sekta ya kilimo kwenye ujumbe wa EU nchini Ukraine amesema "Fedha za EU kwa mradi huu wa FAO zinalenga kuanzisha tena au kuimarisha utendaji wa kiwango cha kabla ya vita wa minyororo ya thamani ya kilimo. Hili linahitajika ili kukidhi mahitaji ya chakula kwa wakazi wa eneo hilo na waliokimbia makazi yao magharibi mwa nchi na kushughulikia uhaba wa chakula mahali pengine nchini katika muda wa haraka na mfupi, na itakuwa muhimu katika kuepusha shida ya chakula mwaka 2023." 

Uhakika wa chakula unazidi kuzorota 

FAO inasema hali ya uhakika wa chakula nchini Ukraine imezorota kwa kasi kufuatia kuzuka kwa vita tarehe 24 Februari 2022, ambayo imesababisha uharibifu mkubwa wa mazao, kilimo na miundombinu mingine ya kiraia, na kutatiza minyororo ya usambazaji na thamani. 

Tathmini ya hivi karibuni ya FAO ya nchi nzima juu ya athari za vita kwenye kilimo na kaya za vijijini inaonyesha kuwa “mtu mmoja kati ya wanne miongoni mwa watu  5,200 waliohojiwa amepunguza au kusitisha uzalishaji wa kilimo kutokana na vita.” 

Kupitia mradi huu unaofadhiliwa na Muungano wa Ulaya, ambao ulianza Februari 2021 kwa awamu ya maandalizi lakini ukasitishwa kwa sababu ya vita sasa unarudishwa ili kukidhi mahitaji ya sasa.  

Mwezi Machi-Mei 2022 msaada wa dharura wa kilimo ulitolewa kwa zaidi ya kaya za vijijini 6,000.  

Msaada huu ulishughulikia hitaji la haraka la watu la pembejeo za kilimo, pesa taslimu, mbegu za mboga mboga na viazi ili kuendeleza uzalishaji wa chakula kwa matumizi ya kaya. 

Kuna haja ya haraka kurejesha uwezo wa familia kujikimu 

"Shuhuda za watu binafsi na familia nilizokutana nazo wakati wa ziara zangu katika maeneo mapya yanayofikika zinathibitisha hitaji la msaada wa haraka katika kurejesha uwezo wa kaya na kuepuka kutegemea misaada ya kibinadamu. Wakati huo huo, ni muhimu kwamba serikali inaungwa mkono katika juhudi zake za kuendeleza sekta ya kilimo na kuimarisha na kubadilisha minyororo ya thamani," amesema Pierre Vauthier, mkuu wa ofisi ya FAO nchini Ukraine . 

Ameongeza kuwa vita ikiendelea, nchini Ukraine washiriki wa soko ikiwa ni pamoja na idadi kubwa ya mashamba ya kaya na familia, wazalishaji binafsi, makampuni madogo, wafanyabiashara na wasindikaji wanapitia matatizo ya kupata pembejeo, fedha na uwekezaji ili kusaidia kuendelea na upanuzi wa shughuli za kilimo.  

FAO inasema matatizo makubwa yanayotarajiwa katika miezi michache ijayo kwa upande wa shughuli za uzalishaji wa mazao na mifugo ni faida ndogo kutokana na uuzaji wa bidhaa, vikwazo vya upatikanaji wa mbolea au viuatilifu, na mafuta au nishati ya umeme kwa vifaa vinavyotumia umeme.