Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama limeombwa kuongeza muda wa makubaliano ya kufikisha misaada Syria

Machafuko yanayoendelea tangu Disemba 2018 yamewalazimisha maelfu ya watu kuzikimbia nyumba zao, miji na vijiji vyao wilayani Hajin Mashariki mwa Deir-ezZor, Syria. Familia zimefunga safari ndegu na dhiki kusaka usalama kwenye kambi ya Al-Hol
©UNICEF/ Syria 2019/ Delil Souleiman
Machafuko yanayoendelea tangu Disemba 2018 yamewalazimisha maelfu ya watu kuzikimbia nyumba zao, miji na vijiji vyao wilayani Hajin Mashariki mwa Deir-ezZor, Syria. Familia zimefunga safari ndegu na dhiki kusaka usalama kwenye kambi ya Al-Hol

Baraza la Usalama limeombwa kuongeza muda wa makubaliano ya kufikisha misaada Syria

Msaada wa Kibinadamu

Wakuu wa mashirika ya Umoja wa Mataifa leo wametoa wito kwa Baraza la Usalama kuongeza muda wa makubaliano ya kuhakikisha msaada wa kibinadamu unaendelea kuvuka mpaka kaskazini-magharibi mwa Syria, kwani muda wa makubaliano hayo unatarajiwa kumalizika baada ya siku nane zijazo.

Wito huo wa pamoja umetolewa na wakuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura OCHA, shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF, shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP, shirika la afya la Umoja wa Mataifa duniani WHO, shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu UNFPA na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR.

Taarifa hiyo ya pamoja imesisitiza kuwa “Iwapo Baraza litashindwa kuongeza muda wa azimio nambari 2642, matokeo yatakuwa mabaya kwa watu milioni 4.1 katika maeneo yasiyodhibitiwa na Serikali”.

Uwezo wa watu kuishi uko hatarini

Katika kilele cha msimu wa baridi na huku kukiwa na mlipuko mbaya wa kipindupindu, wanawake na watoto wanajumuisha watu wengi wanaohitaji msaada ili kuweza kuishi, imesema taarifa hiyo.

Na kuongeza kuwa "Bila ya oparesheni za kuweza kuvuka mpaka za Umoja wa Mataifa, mamilioni ya watu, hasa wale waliokimbia makazi yao kwa miaka na mara kadhaa, hawatapata chakula na malazi, kuwasaidia katika kukabiliana na hali mbaya ya baridi, kuwa na uwezo wa ufuatiliaji, matibabu na upimaji unaohitajika ili kudhibiti kipindupindu, huduma ya maji salama na kuwalinda dhidi ya ukatili wa kijinsia”.

Kushindwa kokote kwa Baraza kuongeza muda wa azimio kutamaanisha pia kuwa mfumo wa ufuatiliaji wa Umoja wa Mataifa (UNMM) kwa ajili ya usaidizi wa mpakani utakoma kufanya kazi, ambao unahakikisha kupitishwa kwa vifaa vya kibinadamu.

Mtoto akipatiwa chanjo katika kambi ya wakimbizi wa ndani ya Alhol Kaskazini mwa Syria
© UNICEF/ Delil Souleiman
Mtoto akipatiwa chanjo katika kambi ya wakimbizi wa ndani ya Alhol Kaskazini mwa Syria

Msimamo thabiti na wazi

Maafisa wa mashirika hayo wamesema "Msimamo wetu unabaki thabiti na wazi, msaada wa kibinadamu na huduma za ulinzi lazima ziruhusiwe kuwafikia wale wanaohitaji kupitia njia salama na ya moja kwa moja na yenye ufanisi".

Wameeleza kuwa mwaka 2022, pamoja na washirika, utoaji wa misaada kutoka mpaka wa Uturuki hadi Syria, ulifikia wastani wa watu milioni 2.7 kila mwezi  ikiwa ni pamoja na kujikwamua mapema na usaidizi wa kujikimu kimaisha ili kuimarisha jamii nchini kote.

"Tuliweza pia kuimarisha usaidizi ndani ya Syria kutoka maeneo yanayodhibitiwa na serikali katika mstari wa mbele hadi kaskazini-magharibi mwa nchi, kupeleka chakula, huduma za afya, elimu na vifaa vingine kwa maelfu ya watu wanaovihitaji", taarifa hiyo iliendelea kusema na kuongeza kuwa

"Tumedhamiria kudumisha na kupanua wigo wa usambazaji huu, na tunatoa wito kwa washikadau wote kuhakikisha ufikiaji wa misaada usiozuiliwa, endelevu na unaotabirika wa kibinadamu kuelekea kaskazini-magharibi mwa Syria kutoka maeneo yanayodhibitiwa na serikali".

Huduma inayoungwa mkono na UNICEF ya lori la kusambaza maji inatoa maji safi kwa watu walio hatarini Syria
© UNICEF/Delil Souleiman
Huduma inayoungwa mkono na UNICEF ya lori la kusambaza maji inatoa maji safi kwa watu walio hatarini Syria

 

Msaada wa kibinadamu ni muhimu

Ingawa njia za uwasilishaji wa sasa ni bora, lakini hauwezi kuendana na ukubwa na wigo wa shughuli za misaada za kuvuka mipaka ambazo zinahitajika, na zitaendelea kuwa za lazima wamesisitiza wakuu wa mashirika hayo.

Tofauti na maazimio ya awali, ambayo yaliongeza shughuli za misaada ya kuvuka mpaka kwa miezi 12, idhini ya hivi karibuni ya Baraza iliongeza muda kwa miezi sita tu.

Hii imesababisha changamoto za ziada za vifaa na uendeshaji, kuongezeka kwa gharama za uendeshaji, na kupunguza uwezo wa washirika wa kibinadamu kutoa misaada inayohitajika.

Taarifa hiyo imehitimisha kwa kusema kwamba "Mamilioni ya watu wanaotegemea njia ya kuvuka mpaka kwa ajili ya kuishi wanahitaji azimio hili kupitishwa upya na haraka bila kuchelewa".