Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Guterres ataka sitisho la mapigano Syria huku Kamishna Mkuu wa haki za binadamu akisikitishwa na madhila dhidi ya raia

Mtoto akitembea kwenye theluji katika makazi ya muda ambayo yanawahifadhi wakimbizi wanaokimbia machafuko kusini mwa Idlib na Aleppo vijijini, Syria.
© UNICEF/Baker Kasem
Mtoto akitembea kwenye theluji katika makazi ya muda ambayo yanawahifadhi wakimbizi wanaokimbia machafuko kusini mwa Idlib na Aleppo vijijini, Syria.

Guterres ataka sitisho la mapigano Syria huku Kamishna Mkuu wa haki za binadamu akisikitishwa na madhila dhidi ya raia

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ametoa wito kwa sitisho la haraka la mapigano nchini Syria, wakati huu ambapo zaidi ya watu 900,000 wamekimbia makazi yao tangu mapema mwezi Desemba mwaka jana.

 

Kupitia taarifa iliyotolewa leo na msemaji wake mjini New York, Marekani, Bwana Guterres amesema, “chuki hivi sasa zimefikia kiwango cha juu katika maeneo ya makazi ya raia wengi. Baridi kali ikiendelea, watu wanahaha kusaka maeneo ambamo angalau watapata hifadhi lakini hiyo inakuwa ni ngumu.”

Huku akitaka sitisho la mapigano, Katibu Mkuu ametaka sheria za kimataifa za kibinadamu zizingatiwe na kwamba, “hakuna suluhisho la kijeshi. Njia pekee ya utulivu ni suluhu jumuishi na la dhati linaloongozwa na Umoja wa Mataifa kupitia azimio namba 2254 la mwaka 2015.”

Azimio hilo lilipitishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa likiridhia mwelekeo wa mchakato wa amani Syria.

Hakuna makazi yaliyo salama

Wakati wakikabiliwa na msimu wa baridi kali na mabomu, zaidi ya raia 900,000 kaskazini-magharibi mwa Syria wamelazimika kukimbia katika maeneo madogo zaidi kutafuta usalama, amesema Kamishna Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa, Michelle Bachelet.

Akizungumza na waandishi wa habari hii leo mjini Geneva Uswisi, msemji wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya haki za binadamu, OHCHR, Rupert Colville amemnukuu Bi Bachelet akisema, "hakuna makazi salama sasa. Wakati shughuli za vikosi vya serikali vinavyozidi kupamba moto, watu wanalazimika kusaka hifadhi katika maeneo madogo na anahofia watu wengi zaidi watauawa."

Tangu Januari mosi mwaka huu, OHCHR imethibitisha vifo vya raia 299 huko Idlib, wakati serikali ya Syria inaendelea na shughuli za kijeshi kuchukua tena eneo la mwisho linaloshikiliwa na upinzani nchini.

Bwana Colville amesema, "karibu asilimia 93 ya vifo hivyo vilisababishwa na serikali ya Syria na washirika wake.” Asilimia saba  ya vifo vilitokana na vikundi visivyo vya kiserikali.

Zaidi ya asilimia 80 ya vifo vitokanavyo na shughuli za vikosi vya serikali na washirika wao ni 246 kati ya 299 kufuatia mashambulizi ya anga.

Kamishna ameeleza kushtushwa na hali wakati mzozo ukiendelea

Katika taarifa yake, Kamishna Mkuu ameelezea kushtushwa kwake kufuatia wigo wa mzozo.

Amesema "hali ni mbaya kiasi cha kutoaminika,” na kwamba wanawake na watoto wengi wanaoishi kwenye mahema ya plastiki walikuwa wakishambuliwa. Ameongeza kwamba wale waliokuwa wakikimbia machafuko walilazimika kukimbia maeneo ambayo yanatokomea kwa kila saa na kwamba hawana sehemu ya kukimbilia.

Madai ya uhalifu wa kivita

Akijibu swali la mwandishi wa habari, Bwana Colville amesema, "idadi kubwa ya mashambulio kwenye hospitali, vifaa vya matibabu, shule, vinaashiria kuwa yote hayawezi kuwa ni kwa bahati mbaya.” Ameongeza kwamba, "kwa kiwango cha chini, hata ikiwa ni bahati mbaya, inaonyesha ukosefu wa usawa, tahadhari na kadhalika, ambayo inaweza kuchangia kwa kitu kinachoweza kuwa ni uhalifu wa kivita."

Kwa upande wake shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limeonya kwamba kati ya watu milioni nne wanaoishi kaskazini-magharibi, zaidi ya milioni mbili ni watoto.

UNICEF imesema watoto milioni 1.8 kati yao, wanahitaji msaada wa kibinadamu.

UNICEF imeongeza kuwa kati ya watu takriban 900,000 waliolazimika kukimbia vurugu zinazoendelea, watoto zaidi ya nusu milioni - 525,000 wamelazimika kuhama kwa lazima kaskazini-magharibi mwa Syria tangu tarehe 1 disemba mwaka jana. 

Kuhusu vifo, takribani watoto 77 waliuawa au kujeruhiwa mwezi uliopita wa Januari pekee, ambapo watoto 28 waliuawa, na watoto 49 walijeruhiwa.

UNICEF imesisistiza wito wake wa kutaka kusitishwa kwa mapigano.