Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Azimio dhidi ya Myanmar lisiwe maneno matupu; Mtaalamu wa UN aliambia Baraza la Usalama

Wasichana wadogo katika kambi ya wakimbizi wa ndani nchini Myanmar wanachota maji kutoka kwenye kisima.
UNOCHA/Z. Nurmukhambetova
Wasichana wadogo katika kambi ya wakimbizi wa ndani nchini Myanmar wanachota maji kutoka kwenye kisima.

Azimio dhidi ya Myanmar lisiwe maneno matupu; Mtaalamu wa UN aliambia Baraza la Usalama

Haki za binadamu

Siku moja baada  ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kupitisha azimio kuhusu Myamar kwenye mkutano wake uliojadili hali ya amani na usalama nchini humo, Mtaalamu Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya Myanmar Tom Andrews amesema azimio hilo la kusitisha uhasama na kurejesha utawala wa kidemokrasia halitakuwa na maana lisipotekelezwa kwa vitendo. 

Kupitia taarifa iliyotolewa leo na Ofisi ya Haki za binadamu ya Umoja wa mataifa, OHCHR, huko Geneva, Uswisi, Bwana Andrews amesema bila Baraza hilo kutumia Ibara ya 7 ya Mamlaka yake, utawala wa kijeshi wa Myanmar hautoacha kushambulia na kuharibu maisha ya watu milioni 54 wanaoshikiliwa mateka Myanmar. 

Nashukuru kwa azimio na utawala wa kijeshi uwajibishwe 

“Inatambuliwa kuwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepitisha azimio kuhusu Myanmar, ikiwa ni mara ya kwanza tangu jeshi lianze msako wa kikatili dhidi ya watu wa Myanmar miaka miwili iliyopita. Nashukuru juhudi hizi za Uingereza na wajumbe wa Baraza kuandaa na kusongesha azimio hili na kuepusha kura turufu,” amesema mtaalamu huyo akisema sasa kinachotakiwa ni vitendo. 

Lugha kidogo ni nyepesi lingalikuwa na hoja ya vikwazo 

Amesema vitendo ni muhimu kwa kuzingatia mifumo iliyowekwa na utawala wa kijeshi kukiuka haki za binadamu, vitendo vinavyoweza kuwa uhalifu dhidi ya binadamu, na vinatekelezwa kila siku na utawala huo ulio madaraki kinyume cha sheria. 

“Matakwa yaliyowekwa na azimio hilo ikiwemo kuacha mara moja aina zote za ghasia, kuachiliwa kwa wafungwa wa kisiasa na hitaji la kuheshimu haki za wanawake na watoto bila kusahamu kufikisha misaada kwa wahitaji bila vikwazo vyote, yote hayo ni muhimu lakini kinachokosekana ni hatua za kuchukuliwa iwapo utawala huo wa kijeshi utashindwa kutekeleza azimio hilo,” amesisitiza mtaalamu huyo. 

Anasema vikwazo na uwajibishwaji ni muhimu na hivyo “nakubaliana na wajumbe wa Baraza kutoka Norway, Falme za Kiarabu, Marekani, Iceland na Mexico ya kwamba azimio lilipaswa kuwa na lugha kali zaidi.”