Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mwanamke aliyefungwa mirija ya uzazi kisa ana UKIMWI ashinda kesi nchini Kenya

Mwanamke mjamzito mwenye umri wa miaka ishirini aliyezaliwa na virusi vya Ukimwi, hutumia dawa kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.
© UNICEF/UN0640796/Dejongh
Mwanamke mjamzito mwenye umri wa miaka ishirini aliyezaliwa na virusi vya Ukimwi, hutumia dawa kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.

Mwanamke aliyefungwa mirija ya uzazi kisa ana UKIMWI ashinda kesi nchini Kenya

Haki za binadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na harakati za kutokomeza UKIMWI, UNAIDS limekaribisha uamuzi wa Mahakama Kuu ya Kenya huko Nairobi wa kutambua kwamba kulazimishwa kufunga kizazi kwa wanawake wanaoishi na VVU ni ukiukaji wa haki zao za kibinadamu.

Taarifa iliyotolewa leo na UNAIDS kutoka Geneva Uswisi imeeleza kuwa hukumu hiyo inafuatia kesi iliyowasilishwa mwaka wa 2014 na mwanamke Mkenya anayeishi na virusi vya UKIMWI ambaye alilazimishwa na wataalamu katika kituo cha afya kufanyia operesheni ya kufungwa mishipa wa mirija ya uzazi hivyo kumwondolea uwezo wa kupata watoto.

Mahakama Kuu iligundua kwamba utendakazi wa operesheni hii bila kibali ni sawa na ukiukaji wa haki zake za kutobaguliwa, utu, afya na familia.

“Uamuzi huu ni hatua muhimu katika kulinda afya ya ngono na uzazi na haki za wanawake wanaoishi na VVU,” amesema Winnie Byanyima, Mkurugenzi Mtendaji wa UNAIDS na kuongeza kuwa “UNAIDS iko tayari kufanya kazi na serikali zote kuhakikisha vitendo kama hivyo vinakomeshwa kabisa na kwamba wanawake wanaoishi na VVU wanaweza kupata huduma za afya bila unyanyapaa au ubaguzi.”

Katika kesi hiyo mlalamikaji alieleza kuwa “Hii (Tukio ya kufanyia operesheni) haikuwa kamwe kuhusu pesa. Nilitaka kupigania haki kwa ajili yangu na wanawake wote ambao wamepata zahma kama hizi, na kuhakikisha hili halifanyiki kwa wanawake wengine wanaoishi na VVU ambao wanahitaji kupata huduma za afya ya uzazi.”

Mchango wa UNAIDS katika kesi hii

UNAIDS iliingilia kati kesi hii kama rafiki wa mahakama amicus curiae na kuitaarifu Mahakama Kuu ya Kenya kuhusu miongozo ya afya na viwango vya haki za binadamu ambavyo kila nchi inapaswa kufuata ili kuheshimu, kulinda na kudhamini haki za binadamu za watu wanaoishi na VVU, na athari ambazo vitendo hivyo vya kujitolea vinaweza kuwa na mwitikio wa VVU.

Mtandao wa Masuala ya Kisheria na Maadili ya Kenya kuhusu VVU/UKIMWI (KELIN) na Asasi ya Afrika ya Jinsia na Vyombo vya Habari (GEM) pia walikuwa walalamikaji katika kesi hii.

Allan Maleche, Mkurugenzi Mtendaji wa KELIN amesema “Tunakaribisha uamuzi wa mahakama na ingawa ulichukua muda mrefu, tunafurahi kwamba mahakama imeona haki za mteja zimekiukwa, na hasa kupatikana kwa ubaguzi kwa misingi ya jinsia na VVU.”

Naye Mkurugenzi wa UNAIDS nchini Kenya, Medhin Tsehaiu amesema UKIMWI ukiwa kama tishio la afya ya umma utamalizwa kupitia njia ya haki za binadamu pekee na si vinginevyo.

"Kesi hii ni wakati muhimu kwa haki ya uzazi na vuguvugu la wanawake. Kulazimishwa kufunga uzazi kwa wanawake wanaoishi na VVU ni ukiukaji wa haki za kimsingi za wanawake na kudhoofisha mwitikio mzuri wa VVU.” Asema Tsehaiu

Hakuna nafasi ya ubaguzi

Mkakati wa Kimataifa wa UKIMWI 2021–2026: “Komesha Ukosefu wa Usawa, Komesha UKIMWI” unajumuisha jukumu kuu la kukuza haki za binadamu, usawa wa kijinsia na utu, usio na unyanyapaa na ubaguzi kwa watu wote wanaoishi na VVU na walioathiriwa na VVU.

UNAIDS ina maono ya masuala yahusianayo na usawa wa kijinsia na kutambua haki za binadamu, ikiwa ni pamoja na haki ya afya, wito kwa washirika na wadau wote katika mwitikio wa VVU katika nchi zote kubadilisha kanuni zisizo sawa za kijinsia na kukomesha unyanyapaa na ubaguzi.

Mtazamo wa kukabiliana na UKIMWI unaozingatia haki ni pamoja na haki ya kuanzisha familia na kupata watoto, haki ya kuamua idadi na nafasi ya watoto wao, haki ya uhuru wa uzazi na haki ya kupata huduma bora ili kusaidia uchaguzi wao wa afya ya uzazi, kulingana na wao.

kibali cha kutoa habari, kuhakikisha usalama na kwa hiari. Hizi ni haki za kimsingi za binadamu ambazo ni za wanawake wote, bila kujali hali ya VVU, na zimehakikishwa katika mikataba ya kimataifa na kikanda.