Weka haki za binadamu katika kitovu cha juhudi za kubadili mwelekeo wa leo wa uharibifu - Guterres

Weka haki za binadamu katika kitovu cha juhudi za kubadili mwelekeo wa leo wa uharibifu - Guterres
Ikiwa leo ni Siku ya Haki za Binadamu, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres kupitia ujumbe wake mahususi kwa ajili ya siku hii amesema, "Nyakati za majaribu" za leo zinaeleza hitaji la kujitolea tena kwa haki za binadamu, ambazo ni muhimu katika kutatua matatizo ya kimataifa.
Maadhimisho haya ya kila mwaka yanaadhimisha uamuzi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kupitisha Azimio la Kimataifa la Haki za Kibinadamu, tukio lililofanyika tarehe 10 Desemba 1948.
"Haki za binadamu ni msingi wa utu wa binadamu, na msingi wa jamii zenye amani, umoja, haki, usawa na ustawi." Amesema Bwana Guterres.
Changamoto zisizo na kifani zilizofungamana
Aidha Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesema dunia kwa sasa inakabiliwa na changamoto ambazo hazijawahi kushuhudiwa na zinazoingiliana kwa haki za binadamukama vile kuongezeka kwa njaa na umaskini, kupungua kwa nafasi za raia, na "kushuka kwa hatari" kwa uhuru wa vyombo vya habari na usalama wa waandishi wa habari.
Guterres ameongeza kusema kuwa wakati huo huo imani katika taasisi inazidi kupungua, hasa miongoni mwa vijana, wakati janga la COVID-19 limesababisha kuongezeka kwa viwango vya ukatili dhidi ya wanawake na wasichana.
Ubaguzi wa rangi, kutovumiliana na ubaguzi vimekithiri, Guterres ameendelea kusisitiza, “na changamoto mpya za haki za binadamu zinaibuka kutokana na kile alichokiita "majanga matatu ya ulimwengu" yaani mabadiliko ya tabianchi, upotevu wa viumbe hai na uchafuzi wa mazingira.
Rejesha upya dhamira ya kimataifa
"Na tunaanza kufahamu tishio linaloletwa kwa haki za binadamu na teknolojia mpya. Nyakati hizi za majaribu zinahitaji kufufuliwa kwa dhamira yetu kwa haki zote za binadamu - kiraia, kitamaduni, kiuchumi, kisiasa na kijamii." ameongeza.
Bwana Guterres amekumbushia kwamba miaka miwili iliyopita, alitoa Wito wa Kuchukua Hatua ambao unaweka haki za binadamu katikati ya suluhisho la changamoto zinazoikabili jumuiya ya kimataifa.
Miaka 75 ya Azimio la Haki za Binadamu
Vile vile Katibu Mkuu wa UN amesema maadhimisho ya miaka 75 ya Azimio la kihistoria la Haki za Binadamu mwaka ujao lazima iwe fursa ya kuchukua hatua.
"Ninaziomba Nchi Wanachama, mashirika ya kiraia, sekta ya kibinafsi na wengine kuweka haki za binadamu katika moyo wa juhudi za kubadilisha mwelekeo wa leo wa uharibifu. Katika Siku hii ya Haki za Kibinadamu, tunathibitisha usawa na kutogawanyika kwa haki zote, tunapotetea haki za binadamu kwa wote." Amesema Guterres.