Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Janga la COVID-19 halikuyumbisha vita dhidi ya malaria 2021: WHO Ripoti

Mwanamke akipokea dawa za kumtibu binti yake mwenye umri wa miaka minne ambaye anaugua malaria katika Jimbo la Jonglei, Sudan Kusini.
© UNICEF/Mark Naftalin
Mwanamke akipokea dawa za kumtibu binti yake mwenye umri wa miaka minne ambaye anaugua malaria katika Jimbo la Jonglei, Sudan Kusini.

Janga la COVID-19 halikuyumbisha vita dhidi ya malaria 2021: WHO Ripoti

Afya

Takwimu mpya zilizotolewa leo na ripoti ya shirika la afya la Umoja wa Mataifa duniani WHO kuhusu malaria, zinaonyesha kwamba nchi kote duniani zilisimama kidete kwa kiasi kikubwa dhidi ya vikwazo zaidi kwa huduma za kuzuia, kupima na matibabu ya malaria mwaka 2021.

Kulingana na ripoti hiyo ya mwaka 2022 ya ugonjwa wa malaria, kulikuwa na vifo vya malaria vinavyokadiriwa kufikia 619,000 duniani kote mwaka 2021 ikilinganishwa na vifo 625,000 katika mwaka wa kwanza wa janga la coronavirus">COVID-19. Mwaka 2019, kabla ya janga hilo kutokea, idadi ya vifo ilikuwa 568,000. 

Ipoti hiyo inasema wagonjwa wa malaria waliendelea kuongezeka kati ya mwaka 2020 na 2021, lakini kwa kiwango cha polepole kuliko kipindi cha mwaka 2019 hadi 2020.  

Idadi ya wagonjwa wa malaria duniani kote ilifikia watu milioni 247 mwaka 2021, ikilinganishwa na watu milioni 245 mwaka 2020 na watu milioni 232 mwaka 2019. 

Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus, mkurugenzi mkuu wa WHO amesema "Kufuatia ongezeko kubwa la wagonjwa wa malaria na vifo katika mwaka wa kwanza wa janga la COVID-19, nchi zilizoathiriwa na ugonjwa wa malaria ziliongeza juhudi zao na kuweza kupunguza athari mbaya zaidi za usumbufu unaohusiana na COVID-19 kwa huduma za malaria. Tunakabiliwa na changamoto nyingi, lakini kuna sababu nyingi za matumaini. Kwa kuimarisha hatua, uelewa na kupunguza hatari, kujenga mnepo na kuharakisha utafiti, kuna kila sababu ya kuwa na ndoto ya mustakabali usio na malaria.” 

Kuweka neti kitandani kumeendelea kuwa njia mojawapo muhimu ya kujikinga na mbu waenezao Malaria
© UNICEF/Frank Dejongh
Kuweka neti kitandani kumeendelea kuwa njia mojawapo muhimu ya kujikinga na mbu waenezao Malaria

Juhudi za kitaifa ni chahu ya mafanikio 

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya WHO vyandarua vilizotiwa dawa  au (ITNs) ndio nyenzo kuu ya kudhibiti vidudu vya malaria inayotumika katika nchi nyingi zenye malaria na, mwaka 2020, nchi zilisambaza vyandarua zaidi kuliko mwaka wowote uliowahi kurekodiwa.  

Mwaka 2021, usambazaji wa ITN ulikuwa thabiti na kwa kiasi kikubwa kwa jumla na katika viwango sawa na miaka ya kabla ya janga la COVID-19. 

Vyandarua vyenye dawa milioni 171 vilivyopangwa kusambazwa, milioni 128 au asilimia (75%) kati ya vyanadarua hivyo vilishasambazwa. 

Hata hivyo WHO inasema nchi nane ambazo ni Benin, Eritrea, Indonesia, Nigeria, Visiwa vya Solomon, Thailand, Uganda na Vanuatu zilisambaza chini ya asilimia 60% ya idadi ya vyandarua vyao, na nchi saba  za Botswana, Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR, Chad, Haiti, India, Pakistan na Sierra Leone hazikusambaza vyandarua vyovyote vyenye dawa. 

Uzuiaji malaria kwa msimu ni muhimu 

Ripoti imeendelea kusema kwamba uzuiaji wa malaria kwa msimu (SMC) unapendekezwa ili kuzuia ugonjwa huo miongoni mwa watoto wanaoishi katika maeneo yenye maambukizi ya malaria ya msimu mwingi barani Afrika.  

Mwaka 2021, upanuzi zaidi wa juhudi za uingiliaji kati huu ulifikia karibu watoto milioni 45 kwa kila mzunguko wa SMC katika nchi 15 za Afrika, ikiwa ni ongezeko kubwa kutoka watoto milioni 33.4 mwaka 2020 na watoto milioni 22.1 mwaka 2019. 

Wakati huo huo, ripiti imesema nchi nyingi zilifanikiwa kudumisha upimaji na matibabu ya malaria wakati wa janga la COVID-19.  

“Licha ya changamoto za ugavi na vifaa wakati wa janga hili, nchi zenye ugonjwa wa malaria zilisambaza idadi iliyovunja rekodi ya vipimo vya haraka vya uchunguzi (RDTs) kwa vituo vya afya mwaka 2020. Mwaka 2021, nchi zilisambaza RDT milioni 223, kiwango sawa na kilichoripotiwa kabla ya janga hilo la COVID-19.” Imesema ripoti 

Imeongeza kuwa tiba mseto yenye msingi wa Artemisinin (ACTs) ndiyo tiba bora zaidi kwa ugonjwa huo. 

Pia ripoti imeongeza kuwa nchi zenye ugonjwa wa malaria ziliwasilisha wastani wa ACT milioni 242 duniani kote mwaka 2021 ikilinganishwa na ACT milioni 239 mwaka 2019. 

Tiba mseto yenye msingi wa Artemisinin (ACTs) ndiyo tiba bora zaidi 

Nchi zenye ugonjwa wa Malaria ziliwasilisha wastani wa ACT milioni 242 duniani kote mwaka 2021 ikilinganishwa na ACT milioni 239 mwaka 2019. 

Mgonjwa akimeza dawa ya Malaria nchiin Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC. Mfumo wa TRVST unatarajiwa kusambaa na kusaidia kuthibitisha ubora, viwango na ufanisi wa dawa na chanjo.
UNICEF/UN0Gwenn Dubourthoumieu
Mgonjwa akimeza dawa ya Malaria nchiin Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC. Mfumo wa TRVST unatarajiwa kusambaa na kusaidia kuthibitisha ubora, viwango na ufanisi wa dawa na chanjo.

Vitisho vinavyoathiri vita dhidi ya malaria 

“Licha ya mafanikio, juhudi zetu zinakabiliwa na changamoto nyingi, haswa katika Kanda ya Afrika, ambayo ilibeba takriban asilimia 95% ya wagonjwa na asilimia 96% ya vifo vya malaria ulimwenguni mwaka 2021.” Kwa mujibu wa ripoti. 

Imeendelea kusema kwamba usumbufu wakati wa janga la COVID-19, migogoro ya kibinadamu, changamoto za mfumo wa afya, kukosekana kwa ufadhili, kuongezeka kwa vitisho vya kibaolojia na kupungua kwa ufanisi wa zana kuu za kutokomeza magonjwa vinatishia hatua za kimataifa dhidi ya malaria. 

Dkt. Matshidiso Moeti, ambaye ni mkurugenzi wa WHO Kanda ya Afrika amesema "Licha ya hatua zilizopigwa, kanda ya Afrika inaendelea kuathirika zaidi na ugonjwa huu hatari. Zana mpya na ufadhili wa kupeleka zana hizo vinahitajika haraka ili kutusaidia kushinda ugonjwa wa malaria." 

Jumla ya ufadhili kwa ajili ya malaria mwaka 2021 kwa mujibu wa ripoti ilikuwa dola bilioni 3.5 ikiwa ni ongezeko kutoka miaka miwili iliyotangulia , lakini bado ni kiwango cha chini ya makadirio yad ola bilioni 7.3 zinazohitajika duniani kote kusilia kwenye lengo la kutokomeza malaria. 

Nchini Msumbiji, vizazi vitatu vya familia moja huketi pamoja chini ya chandarua kilichotiwa dawa.
©UNICEF/Wikus De Wet
Nchini Msumbiji, vizazi vitatu vya familia moja huketi pamoja chini ya chandarua kilichotiwa dawa.

Kupungua kwa nyenzo za kudhibiti malaria ni mtihani 

Wakati huo huo, ripoti imeonya kwamba kupungua kwa ufanisi wa zana kuu za kudhibiti malaria, hasa ITNs, kunazuia maendeleo zaidi dhidi ya malaria.  

Vitisho kwa chombo hiki muhimu cha kuzuia malaria ni pamoja na usugu wa viua wadudu, kutokuwa na fursa ya kupata dawa hizo, kutokuwa na kiwango cha kutosha cha ITNs kwa sababu ya matumizi ya kila siku na mabadiliko ya tabia ya mbu, ambao huonekana kuuma watu mapema kabla ya kwenda kulala, na wakiwa wamepumzika nje, na hivyo kukwepa kudhibitiwa na viua wadudu. 

Ripoti imeongeza kuwa hatari nyingine pia zinaongezeka, ikiwa ni pamoja na mabadiliko ya vimelea yanayoathiri utendaji wa vipimo vya haraka vya uchunguzi, kuongezeka kwa usugu wa vimelea kwa dawa zinazotumiwa kutibu malaria, na uvamizi barani Afrika wa mbu anayeishi mijini ambaye anastahimili viuawadudu vingi vinavyotumiwa hivi leo.