Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ungana nasi katika juhudi za pamoja kutokomeza kabisa Malaria- WHO

Picha ya maktaba ikimwonesha mama akiwa na mwanae kwenye gari la wagonjwa huko kituo cha malazi mjini Beira, Msumbiji ambako binti yake huyo kwenye  umri wa miaka 2 anatibiwa ugonjwa wa Malaria.
© UNICEF/UN0303710/Oatway
Picha ya maktaba ikimwonesha mama akiwa na mwanae kwenye gari la wagonjwa huko kituo cha malazi mjini Beira, Msumbiji ambako binti yake huyo kwenye umri wa miaka 2 anatibiwa ugonjwa wa Malaria.

Ungana nasi katika juhudi za pamoja kutokomeza kabisa Malaria- WHO

Afya

Ikiwa leo ni siku ya Malaria duniani, shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO, kwa kushirikiana RBM Partnership ambalo ni jukwaa la kutokomeza ugonjwa wa malaria linaloundwa na wadau zaidi ya 500 kuanzia makundi ya wahudumu wa sekta ya afya na mashirika ya kimataifa linanadi kauli mbiu ya “Bila Malaria inaanza na mimi”.

 

Kampeni hiyo ni maalumu inayoanzia chini ikilenga kuiweka malaria katika nafasi ya juu ya ajenda za kisiasa, kuratibu rasilimali za ziada, na kuziwezesha jamii kumiliki mapambano ya kuizuia Malaria. 

WHO imesema, “tunafahamu kwamba kupitia uongozi wa nchi na hatua ya pamoja, tunaweza kupunguza kwa kiasi kikubwa mateso na vifo vinavyotokana na malaria. Kati ya mwaka 2000 na 2014, idadi ya vifo vinavyohusiana na malaria ilipungua kwa asilimia 40 duniani kote, kutoka katika makadirio ya vifo 743,000 hadi 446,000.”

Hata hivyo WHO imesema kuwa katika miaka ya hivi karibuni, maendeleo ya kuitokomeza malaria yamekwama. Kwa mujibu wa ripoti ya malaria ya mwaka jana 2019 iliyotolewa na shirika hilo la Umoja wa Mataifa linalosimamia afya duniani kote, hakukuwa na ongezeko kimataifa la kupunguza maambukizi mapya katika kipindi cha mwaka 2014 hadi 2018. “Na watu wengi walifariki dunia kutokana na malaria katika mwaka 2018 kama ilivyokuwa katika mwaka uliotangulia.” Imefafanua taarifa ya WHO. 

WHO inatoa wito kuwa hatua za haraka zinahitajika ili kurejea katika njia ya mapambano, na umiliki wa changamoto uko mikononi mwa nchi ambazo zimeathirika zaidi na malaria. Kampeni ya “Bila Malaria” inahusisha wanajamii wote wakiwemo viongozi wa kisiasa ambao wanaongoza maamuzi ya sera za serikali, makampuni ya sekta binafsi ambayo yatanufaika na nguvu kazi isiyo na malaria, na pia jamii ambayo imeathiriwa na malaria ambao udhibiti wa malaria ni muhimu kwa mafanikio yao. Kwa msingi huo WHO imewasihi watu wote kuungana nayo katika juhudi za pamoja za kuitokomeza malaria kufikia sifuri. Ungaa nasi katika juhudi zetu za pamoja za kufikia sifuri.

Malaria katika zama za COVID-19 hususani katika nchi za kusini mwa jangwa la Sahara. 

“Wakati COVID-19 ikiendelea kusambaa kwa haraka duniani kote, kuna uhitaji wa haraka  wa kuudhibiti ugonjwa huo mpya lakini tukihakikisha kuwa magonjwa mengine yanayoua watu wengi kama malaria hayasahauliki,” inasisitiza WHO ikiongeza kuzisihi nchi kuhakikisha mwendelezo wa huduma za malaria ilimradi kwa kuhakikisha kuwa wahudumu wa afya wanalindwa.

Wanawake wengi zaidi katika nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara wanatumia vyandarua vyenye viuatilifu ili kujikinga dhidi ya Malaria.
©UNICEF/Josh Estey
Wanawake wengi zaidi katika nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara wanatumia vyandarua vyenye viuatilifu ili kujikinga dhidi ya Malaria.

 

Mzigo wa malaria duniani

Katika mwaka 2018, ilikadiriwa kuwa kulikuwa na wagonjwa wa malaria kufikia milioni 228 katika nchi 89. WHO kanda ya Afrika ilirekodi asilimia 93 ya visa vya malaria na asilimia 94 ya vifo kote duniani katika mwaka huo wa 2018. 

Zaidi ya nusu ya wagonjwa wote wa malaria walikuwa katika nchi sita tu ambazo ni Nigera iliyokuwa na asilimia 25 ya visa vyote, Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo DRC asilimia 12, Uganda asilimia 5,  Côte d’Ivoire, Msumbiji na Niger zikiwa na asimia 4 kila moja. 

Chanjo ya malaria

Mwaka 2019, nchi tatu yaani Ghana, Kenya na Malawi, zilitambulisha chanjo ya malaria katika maeneo machache yaliyochaguliwa kupitia programu ya majaribio ya WHO. Kwa mujibu wa WHO chanjo hiyo, kupitia majaribio ya kisayansi imeonesha kupunguza visa vinne vya malaria kati ya 10 miongoni mwa watoto.

Mbu aina ya anopheles waambukizao malaria wakiwa katika maabara ya taasisi ya KEMRI/CDC nje ya mji wa Kisumu nchini Kenya
Sven Torfinn/WHO 2016
Mbu aina ya anopheles waambukizao malaria wakiwa katika maabara ya taasisi ya KEMRI/CDC nje ya mji wa Kisumu nchini Kenya