Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mikunde imeinua uchumi wetu, lishe na jamii yetu: Wakazi wa Makueni Kenya

Immaculate Ngei: mkulima na mfanyabiashara wa mazao ya maharagwe Makueni nchini Kenya.
UN News/Thelma Mwadzaya
Immaculate Ngei: mkulima na mfanyabiashara wa mazao ya maharagwe Makueni nchini Kenya.

Mikunde imeinua uchumi wetu, lishe na jamii yetu: Wakazi wa Makueni Kenya

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Kenya imeongeza kasi ya mradi wa mazao ya jamii ya mikunde ikiwemo maharagwe yaliyorutubishwa na madini ya Zinc na Chuma na kuwashirikisha wakulima wengi zaidi wadogo kwenye kilimo hicho. 

Soundcloud

Maharagwe aina ya Nyota, Angaza na Faida yanahitaji maji kidogo kukua na muda mfupi kukomaa huku mavuno yake yakiwa mengi. 

Harakati hizo zinaendana na malengo ya shirika la Umoja wa mataifa la chakula na kilimo FAO, liliutenga mwezi wa Februari kuwa wa kuhimiza umuhimu wa mazao ya maharagwe kadhalika 2023 kuwa mwaka wa mtama. 

Mtama na mikunde ni mimea iliyo na mchango muhimu kwenye juhudi za kupambana na mabadiliko ya tabianchi yanayosababisha ukame, kiangazi ,wadudu kuongezeka mashambani na hatimaye kusababisha uhaba wa chakula. 

Wakulima nchini Kenya wakipokea mafunzo kuhusu kilimo hifadhi.
UN News/Thelma Mwadzaya
Wakulima nchini Kenya wakipokea mafunzo kuhusu kilimo hifadhi.

Uhakika wa mavuno kila msimu  

Mazao jamii ya mikunde yana nafasi muhimu kwenye maisha ya mwanadamu. Ni chakula chenye virutubisho muhimu kwa afya na pia huimarisha mifumo ya kilimo. 

Suluhu ya uhaba wa maji kupitia kilimo inapatikana kwenye mikunde ambayo inahitaji maji kidogo kukua na muda mfupi kukomaa. 

Kwa mujibu wa FAO mikunde ina uwezo mkubwa wa kuhimili kiangazi, majanga yanayosababishwa na ukame ikilinganishwa na mimea miengine. 

Immaculate Ngei ni mkulima wa maharagwe, pojo, mbaazi na kunde kutoka Makueni na anaisifia mikunde kwani imembadilishia maisha yake kwasababu,Hakuna msimu unapita bila kuvuna.Navuna maharagwe...mbaazi, vyakula mbalimbali hata mtama.kuna chai ya mtama , keki ya mtama hata uji wa kienyeji.Nina kikundi cha kupika chakula cha kitamaduni.Nimewafunza wakulima wenzangu kulima na kuuza pamoja ili wapate bei nzuri.”  

Kilimo hifadhi na mazingira 

Kulingana na wataalam wa kilimo, mikunde ikipandwa pamoja na miti midogo inaongeza uwezo wa wakulima kwa kujikita kwenye kilimo hifadhi kinachoimarisha hali ya udongo na mazao kwa jumla.  

Gregory Kitiso ni mkulima wa eneo la Makueni la Kenya na mshauri wa kijiji anaamini kuwa kilimo hifadhi ndio suluhu ya maisha kwavile,“Kimesaidia sana kwa kuhifadhi udongo na mazingira yetu kwani hatukati ile mimea sana na tunapata hewa safi inayotoka kwa miti. Unapata pia inachangia kuleta mvua na udongo wetu hausombwi sana na maji unasalia na rutuba tu. Hivi sasa tumekuja kugundua kwamba kuna maharagwe yaliyorutubishwa. Kwa sasa hivi kuna maharagwe ambayo yanaitwa Nyota kutokea shirika la KALRO la utafiti. Maharagwe hayo yana virutubishi vya madini ya Zinc na Chuma. Madini hayo yanahitajika hata kwa watoto wadogo kwenye kukua na pia kwa wanaume.” 

Wafanyabiashara wa mazao ya maharagwe Makueni nchini Kenya.
UN News/Thelma Mwadzaya
Wafanyabiashara wa mazao ya maharagwe Makueni nchini Kenya.

Faida za kiuchumi za mikunde 

Biashara ya mikunde imewawezesha wakulima na wafanyabiashara wengine wa sekta hiyo kunufaika. 

Nchini Kenya, mradi wa maharagwe yaliyorutubishwa kwa madini ya Zinc na chuma umeleta tija kwa wakulima wa kaunti kadhaa ikiwemo Makueni. 

Lydia Kiswii ni mtaalam na mshauri wa kilimo kutoka shirika la wakulima wa nafaka na mikunde, CGA, linalowashika mkono wakulima na anafafanua umuhimu wa maharagwe haya yaliyorutubishwa kuwa ,“Ni mavuno ambayo yana umuhimu wake katika ardhi .Ni mavuno ambayo yana umuhimu wake katika kupunguza umasikini….yanachangia kuwa na uhakika wa chakula na pia lishe muhimu. Ni uhakika kwamba ukiyapanda utavuna.Yanavumilia jua. Baadhi ya maharagwe yaliyorutubishwa yaliyo na viwango vya juu vya madini ya chuma na zinc kama Nyota ndiyo tunayowahimiza wakulima kupanda kwani yana mavuno mengi na manufaa kwa familia nzima.” 

Maharagwe ni tiba na lishe bora 

Shirika la FAO, kwa kutambua umuhimu wa mazao jamii ya mikunde kwa jamii, lishe na hata kipato liliamua kutenga siku maalum ya mikunde. 

Ulimwengu unakabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi ambayo yanasababisha uhaba wa chakula, kuleta magonjwa ya mimea na wadudu kusambaa. 

Ili kupambana na changamoto hizo,mikunde imeelezwa kuwa na uwezo wa kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi kwani inachukua muda mfupi kukomaa, kuhitaji maji kidogo na pia ina virutubisho vingi. 

Kadhalika ni chakula ambacho kinaweza kuhifadhiwa kwa muda mrefu pasi na kuharibika na kinahitaji jua tu kukaushwa. 

Mikunde imefungua mianya ya kiuchumi kwa wakulima wadogo kwani faida yake ni kubwa ikilinganishwa na nafaka.  

Immaculate Ngei ni mkulimwa wa Makueni na anakiri kuwa maisha yake yamebadilika tangu akumbatie kilimo cha mikunde kwa kiasi kikubwa na,“Maharagwe ya Nyota ni tofauti kwani madini ya chuma yanawasaidia wanawake hasa kwasababu ya kipindi cha hedhi.Yanawasaidia pia watoto kukua vizuri na kuwapa wanaume nguvu za kiume.Mbaazi nazo zikiwa mbichi zina bei nzuri kabla ya kukauka.Nilipanda pojo baada ya kupata masomo maalum na kuweza kukabiliana na ndege waliokuwa wananimalizia mavuno.Nilipanda kilo 20 kwenye ardhi ya eka 5 na nikapata magunia 7.Nilishkuru na nikasema kupitia kilimo kuna kitu kwenye mchanga.”  

Mashine ya kukoboa mazao ya maharagwe inayokoa muda.
UN News/Thelma Mwadzaya
Mashine ya kukoboa mazao ya maharagwe inayokoa muda.

2023 ni mwaka wa mtama uhusiano wake na mikunde 

Shirika la Umoja wa Mataifa la FAO, limeuteua mwaka wa 2023 kuwa mwaka wa mtama kwani upo uhusiano muhimu kati ya mikunde na mtama. 

Mikunde na mtama ina mchango muhimu kwenye mfumo mzima wa kuwa na uhakika wa chakula kwani ni mimea inayokua kwenye maeneo ambayo yanastahimili ukame na mvua haba. 

Pale wakulima wanapopanda mtama na mikunde kwa pamoja au kupokezana, mazao yanaongezeka na kuimarisha mazingira na kilimo kwa jumla. 

Ili kufanikisha hayo, upo umuhimu wa kutumia mbegu zilizohalalishwa kama anavyothibitisha Moses Mwinzi ambaye ni muuzaji wa mbegu zilizohalalishwa kwani,”Mbegu ambazo zimehalalishwa na serikali kupitia mamlaka ya KEPHIS zina ubora kwani serikali imefuatilia sana ndio mkulima apate mbegu bora inayofaa na kustahili kwenye eneo lake.Kile kitu muhimu tunawafunza wakulima ni mabadiliko ya tabia ya nchi.Kiwango cga mvua kimebadilika.Watu wa zamani walikuwa wanajaribu kupima mvua lakini mambo yamebadilika.Tunawashauri walime wiki mbili kabla msimu wa mvua kwani ikinyesha inaendelea na itakapokatika ni kabisa.Tunamshauri mkulima ajiandae mapema apande. 

Mtama na mikunde kama pojo inaweza kupikwa kwenye chungu kimoja na kuwa mseto wa aina fulani ulio na virutubisho muhimu mwilini. 

Mikunde kadhalika inaongeza rutba mashambani na kufanya kazi kwa pamoja na mbolea asilia ili kuzuia athari za ukame au mafuriko.  

Julius Kinywee ni afisa wa kilimo katika serikali ya kaunti ya Makueni anaelezea hatua wanazochukua kuimarisha kilimo ambazo zinasisitiza kuwa,“Kama kaunti tumeigawanya kaunti ya Makueni kwenye maeneo 3 kulingana na mvua inavyonyesha.Hilo linawasaidia wakulima kujipanga kulingana na mvua ili wapande mazao yanayofuata hali hizo.Hapo tunawashauri wakulima ili wasikose kuvuna chochote katika kila msimu.Safari ni ndefu lakini wanaendelea kubadilika. 

Mchango wa mazao ya mikunde katika SDGs  

Mazao ya mikunde yanayojulikanana sana na kuliwa kwa wingi ni maharagwe, njugumawe na choroko. 

Hata hivyo zipo aina nyingine ambayo pia zina virutubisho na na uwezo wa kupambana na mabadiliko ya tabianchi. 

Dhamira ya malengo ya maendeleo endelevu ya Umoja wa Mataifa SDGs ni kutomuacha mtu yeyote nyuma katika fani zote za maisha hasa kupunguza umasikini, janga la ukame na kuhakikisha chakula kinatosha.  

Kutokana na hilo, FAO inasema mikunde ina nafasi muhimu ya kufanikisha malengo hayo ya maendeleo. 

 

Taarifa hii imeandaliwa na Thelma Mwadzaya, Stringer Kenya