Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hii ndio hali ya VVU na UKIMWI nchini Ukraine kwa sasa - UNAIDS 

Daktari akipima mtoto kama ana VVU nchini Ukraine.(Maktaba)
© World Bank/Yuri Mechitov
Daktari akipima mtoto kama ana VVU nchini Ukraine.(Maktaba)

Hii ndio hali ya VVU na UKIMWI nchini Ukraine kwa sasa - UNAIDS 

Afya

Vita nchini Ukraine vinaendelea kutatiza huduma za afya na minyororo ya ugavi ambayo mamia ya maelfu ya watu wanaoishi na walioathiriwa na Virusi Vya UKIMWI, VVU wanategemea kuishi.  

Shirika la Umoja wa Mataifa lakutokomeza UKIMWI, UNAIDS linashirikiana na serikali na mashirika ya kiraia ili kuhakikisha mwendelezo wa huduma za VVU na ulinzi kwa watu muhimu na watu wanaoishi na VVU walioathiriwa na vita. 

“Kabla ya vita, takribani watu 260,000 walikadiriwa kuishi na VVU nchini Ukraine, 152 000 kati yao walikuwa wakipata dawa za kuokoa maisha za kurefusha maisha.” UNAIDS inaeleza katika taarifia yake iliyoitoa leo tarehe 20 Mei 2022. 

Hadi kufikia tarehe 3 Mei 2022, maeneo 39 ya kutoa matibabu ya kurefusha maisha yalifungwa katika maeneo yanayokaliwa na ambapo uhasama au unyanyasaji unafanyika. Wakati akiba ya kutosha ya dawa za VVU nchini Ukraine imehakikishwa na washirika wengi, usambazaji wa dawa kwa watu wanaohitaji nchini humo bado ni changamoto kubwa. 

UNAIDS inaendelea kueleza kuwa upimaji wa VVU umekatizwa. Upatikanaji wa uchunguzi, ikiwa ni pamoja na kupima ukubwa kinga, CD4 na wingi wa virusi, umetatizwa kabisa huko Kharkiv, Mariupol, Donetsk, Luhansk na Slavyansk na umetatizwa kwa kiasi huko Kherson. 

Watu wachache wanagunduliwa na watu wachache wanaanza matibabu ya VVU. Kumekuwa na upungufu wa asilimia 30 wa idadi ya watu wanaoishi na VVU ambao walianza tiba ya kurefusha maisha mwaka 2022 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2021 (Jan-Mei). 

Unyanyasaji wa kijinsia unazidi kuripotiwa katika maeneo ya vita. 

Hatua na changamoto 

Shukrani kwa juhudi za pamoja za PEPFAR, Mfuko wa Kimataifa wa UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria, Kituo cha Afya ya Umma cha Ukraine, Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani, WHO, UNAIDS na mashirika ya kiraia, usambazaji wa dawa za kufubaza virusi au kurefusha maisha  nchini vinatosha, lakini changamoto za vifaa na usalama ni kubwa. 

Tiba ya kukinga kuambukizwa kwa waathiriwa wa unyanyasaji wa kijinsia inapatikana. PEP inasambazwa katika maeneo ya tiba ya kurefusha maisha, vituo vya UKIMWI na hospitali na inapatikana saa 24 kwa siku, siku saba kwa wiki. 

UNAIDS inaunga mkono wadau nchini Ukraine na kimataifa kuendeleza masuluhisho ya dharura ya kutoa msaada wa kimatibabu na kibinadamu kwa mamia ya maelfu ya raia wa ukraine. 

Mashirika ya kiraia, kwa ushirikiano na Kituo cha Afya ya Umma cha Ukraine, yanaendeleza juhudi za kishujaa kuwasilisha vifaa na huduma muhimu lakini yamezidiwa na hayana rasilimali. UNAIDS imetoa wito wa dharura kwa jumuiya ya kimataifa kwa ziada ya dola za Marekani milioni 2.42 kusaidia mashirika ya kiraia yanayotoa huduma za VVU nchini Ukraine na katika nchi zinazopokea wakimbizi. 

Usaidizi kwa wakimbizi katika nchi jirani 

Takriban watu 30,000 wanaoishi na VVU wanakadiriwa kuikimbia nchi na ingawa idadi ya watu wanaovuka mipaka kutoka Ukraine na kuingia nchi jirani bado ni kubwa, hali hiyo ya kuhama inapungua. 

Idadi ya watu ambao wametuma maombi ya matibabu ya kurefusha maisha katika nchi zinazowapokea ilikuwa takriban 3000 kufikia katikati ya mwezi wa Aprili na imeanza kuongezeka huku watu wakikosa dawa walizobeba kutoka Ukraine. Maombi zaidi yanatarajiwa katika wiki zijazo. 

UNAIDS inahamasisha ofisi za nchi na mitandao ya watu wanaoishi na VVU katika kanda ili kutoa msaada katika kuhakikisha mwendelezo wa upatikanaji wa tiba ya kurefusha maisha na huduma za VVU. 

Afya ya akili na msaada wa kisaikolojia 

Huduma za afya ya akili na msaada wa kisaikolojia ni miongoni mwa mahitaji yaliyoripotiwa zaidi. Takriban asilimia 50 ya wanawake na wanaume walioshiriki katika Uchambuzi wa Haraka wa Jinsia uliofanywa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Wanawake, UN Women na CARE International walionesha kuwa afya yao ya akili imeathiriwa na vita. 

Kuna ukosefu wa upatikanaji wa huduma za afya, hasa kwa waathirika wa unyanyasaji wa kijinsia pamoja na wanawake wajawazito na mama wachanga (kuna takribani wanawake wajawazito 265,000 wa Ukraine). Pia kuna hofu ya kuongezeka kwa unyanyasaji wa kijinsia, hasa katika maeneo ya vita.