Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baada ya kuelimishwa, sasa wanaume nchini Uganda wapeperusha bendera ya usawa wa kijinsia

Kupitia mpango wa Spotlight Initiative, UN Women Jeshi la Polisi nchini Uganda, wanajumuisha wachuuzi wanaume katika kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na wasichana kama sehemu ya siku 16 za harakati za Polisi kutokomeza ukatili.
UN Women/Eva Sibanda
Kupitia mpango wa Spotlight Initiative, UN Women Jeshi la Polisi nchini Uganda, wanajumuisha wachuuzi wanaume katika kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na wasichana kama sehemu ya siku 16 za harakati za Polisi kutokomeza ukatili.

Baada ya kuelimishwa, sasa wanaume nchini Uganda wapeperusha bendera ya usawa wa kijinsia

Wanawake

“Kama bingwa mwanaume, ninahaha kuweka ujumuishi wa kijinsia na kupatia usawa wa kijinsia kipaumbele,” ni kauli ya Wilfred Nyeko, Afisa Maendeleo ya Jamii katika serikali ya mtaa nchini Uganda.

Kupitia makala maalum kwenye wavuti ya shirika la Umoja wa Mataifa la kushughulikia masuala ya wanawake, UN WOMEN, Bwana Nyeko anasema “kuwa bingwa mwanaume wa masuala ya jinsia inamaanisha kutoa taarifa kuhusu aina zote za unyanyasaji, kuwa mchochea mabadiliko na kujenga hamasa kwa wanaume, na kuwa mfano wa waleteo mabadiliko ya fikra.

Inamaanisha pia kuwa mchechemuzi wa haki za wanawake na wasichana, na kufanya  kazi ili wajumuishwe na waonekane kwenye jamii.

Bwana Nyeko ni miongoni mwa wanaume 15 wakazi wa wilaya ya Kitgum nchini Uganda ambao walishiriki kwenye mafunzo yaliyoandaliwa na mpango wa Spotlight Initiative mwaka 2019 na 2020, mafunzo yaliyohusu usawa wa jinsia, haki za wanawake na utokomezaji wa ukatili wa kijinsia.  Mafunzo yaliendeshwa na mshirika wa UN WOMEN nchini Uganda, LandNet Uganda. Spotlight Initiative ni ubia kati ya Umoja wa Mataifa na Muungano wa Ulaya wenye lengo la kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake ifikapo mwaka 2030.

“Nchini Uganda kuna upendeleo wa kijinsia kwenye elimu, kuna pengo la kijinsia kwenye kilimo, kwenye ujira na ukosefu wa uwakilishi wa wanawake na wasichana kwenye ngazi ya sera na ongezeko la matukio ya unyanyasaji wa kingono,” anasema Bwana Nyeko.

Ni kwa mantiki hiyo anasema akiwa bingwa mwanaume wa masuala ya jinsia, “natumia mamlaka yangu kwenye jamii kuweka utamaduni wa ujumuishi zaidi na kusongesha harakati za kupunguza ghasia kwenye jamii yangu.”

Wakati wa mafunzo, Bwana Nyeko na mabingwa wengine wanaume walijifunza kuhusu dhimay a haki za wanawake katika kupunguza ukatili wa kijinsia; umuhimu wa huduma za uzazi wa mpango kwa wanawake na jinsi ya kuhamasisha wanaume kusaka huduma hizo za uzazi wa mpango wakiwa na wake zao; mbinu chanya za malezi zinazohimiza usawa wa kijinsia; na tabia chanya za kujamiiana zinazosongesha uhuru wa mwanamke kuhusu mwili wake.

Mabingwa hao walipatiwa mbinu na stadi za kuwa watu wa mfano na waleta mabadiliko chanya kwa wanaume wengine katika jamii zao, na sasa vitendo vitendo vya ukatili vimepungua katika wilaya ambazo wanaume walishiriki mafunzo.

Ushirikishaji wa wanaume wachuuzi katika kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto wa kike nchini Uganda.
UN Women/Eva Sibanda

Wanawake husubiri waume zao waamue kuhusu umiliki wa ardhi

Kuna uhusiano dhahiri kati ya haki na umiliki wa ardhi kwa wanawake na ukatili wa kijinsia nchini Uganda. Katika wilaya ya Kitgum, asilimia 63 ya wanawake wanamiliki ardhi na asilimia 86 wana uwezo wa kutumia ardhi, lakini kwa mujibu wa sheria ya kimila ya umiliki wa ardhi nchini humo, haki hizi mara nyingi hazitambuliwi kwenye jamii ambako wanaume ndio wanatawala mfumo wa kutoa maamuzi, na wanawake wanaenguliwa kwenye mfumo wa utawala.

“Kwa kawaida, wanawake lazima wasubiri  waume zao waamue kuhusu usimamizi na utumiaji wa ardhi, na hivyo kuacha wanawake wengi wa vijiini bila umiliki wa rasilimali za uzalishaji na huduma,” anasema Evelyn Letiyo, Mtaalamu wa Masuala ya kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na wasichana katika UN Women nchini Uganda.

Bi. Letiyo anasema hiyo inamaanisha kuwa kunapotokea matukio ya ukatili majumbani, wanawake wanahisi hawana mbadala zaidi ya kusalia kwenye kaya yenye ukatili kwa sababu hawana mbinu nyingine ya kujisaidia wao au watoto wao.

Halikadhalika, takribani asilimia 50 ya wakazi wa maeneo ya kaskazini mwa Uganda, wamekabiliwa na mizozo ya ardhi—wengi wao wakiwa ni wanawake na wajane—na asilimia 72 ya mizozo hiyo ni ndani ya kaya, familia na koo. Mara nyingi mizozo hii ya ardhi husababisha ukatili wa kiuchumi na hata vipigo kwa wanawake na watoto wa kike.

Mabingwa wanaume wameleta mabadiliko

Pamoja na mafunzo ambayo mabingwa hawa wanaume wamepatiwa kuchechemua usawa wa kijinsia kwenye jamii zao, LandNet Uganda iliendesha pia mikutano ya uhamasishaji na majukwaa ikijumuisha wanajamii 2,206 ili kuongeza uelewa kuhusu haki ya ardhi kwa wanawake, kuongeza ushiriki wa wanawake kwenye utoaji wa maamuzi na uongozi na pia kusaidia wanawake kuelewa huduma gani zinapatikana pindi wakikabiliwa na unyanyasaji na ukatili.

“Tangu kufanyika kwa mikutano hiyo ya kijamii, wanawake 25 sasa wanashiriki katika utoaji maamuzi kuhusu matumizi na haki ya ardhi, na kumekuweko na taarifa nyingi zaidi kutoka kwa wanawake kuhusu masuala ya ardhi katika mamlaka sahihi. Halikadhalika wanawake wengi zaidi wameweza kupata ardhi,” anasema Bwana Nyeko.

Hata hivyo anasema jambo muhimu zaidi, ukatili wa kijinsia unaripotiwa na kushughulikiwa na polisi na mamlaka husika nyinginezo.

Stadi za usuluhishi na ushauri nasaha nazo zimewasaidia kushughulikia mizozo ya ardhi na kutoa ripoti kuhusu ukatili wa kijinsia kwa ubora zaidi kuliko hapo  awali.

Hatimaye, nataka wanaume watambue kuwa tunapaswa kuishi  kwa pamoja na kwa amani na wanawake kwenye jamii yetu,” anatamatisha Bwana Nyeko.