Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Msaada kwa manusura wa ukatili wa kijinsia waleta raha baada ya karaha

Goretti Ondola (kulia) akizungumza na Caren Omanga wa kituo cha sheria za kijamii cha Nyando nchini Kenya
UN Women/Luke Horswell
Goretti Ondola (kulia) akizungumza na Caren Omanga wa kituo cha sheria za kijamii cha Nyando nchini Kenya

Msaada kwa manusura wa ukatili wa kijinsia waleta raha baada ya karaha

Wanawake

Mizozo, majanga ya kibinadamu na ongezeko la majanga yatokanayo na tabianchi yamesababisha viwango vya juu vya ukatili dhidi ya wanawake na wasichana, hali ambayo imshika kasi zaidi wakati wa janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19. Kitendo hicho kimechangia udharura wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake.
 

Duniani kote, takribani mwanamke 1 kati ya 3 amekumbwa na ukatili, huku majanga yakisababisha takwimu kuwa juu zaidi.
Ukatili wa kijinsia, GBV, moja ya vitendo vya ukiukwaji mkubwa zaidi wa haki za binadamu si jambo ambalo ni la kiasili au halikwepeki na linapaswa kuzuiwa.

Katika kuadhimisha siku siku 16 za harakati za kupinga ukaitli dhidi ya wanawake  shirika la Umoja wa Mataifa la kushughulikia masuala ya wanawake, UN Women linapaza sauti za manusura watatu wa ukatili. Wote hao majina yao yamebadilishwa ili kutunza utambulisho wao. Kila mmoja amekumbwa na ukatili wa kijinsia.

Ashawishiwa kuwa angaliuawa

Kutoka jimbo la Chaco nchini Argentina, Diana, mama mwenye umri wa miaka 48 amekumwa na ukatili kutoka kwa mwenza wake kwa muda wa kipindi cha miaka 28 hadi pale aliposema nimechoka! “Nilihofia kuwa angalinipiga, nilishawishika kuwa angaliniuwa,” amesema.

Mwanzo, alihofia kuripoti polisi malalamiko ya kupigwa na mwenza wake kwa hofu ya kile ambacho mwenza huyo angalifanya. Lakini baadaye alibaini kuwa kuna huduma nyingi katika kituo cha hifadhi kwenye eneo lao na hivyo angaliweza kumtoroka, kwa hiyo akaamua kupeleka malalamiko polisi.
Watoto wa Diana walipata madhara ya kisaikolojia kwa kitendo cha kuishi na baba mkatili. Hali ya kiuchumi nayo ilikuwa mbaya. 

Kuondoka nako haikuwa rahisi. Lakini kwa msaada wa wafanyakazi wa kijamii, na makazi ya hifadhi ambako kuna eneo la kuishi, Diana alipata kazi kama msaidizi kwenye ofisi ya Manispaa.

Kuchagiza usawa wa jinsia

  • Ukatili dhidi ya wanawake unaepukika.
  • Mikakati ya kina inahitajika ili kushughulikia mizizi ya tatizo hilo, kurekebisha fikra potofu kwenye jamii na kutoa huduma kwa manusura sambamba na kuondokana na ukwepaji sheria kwa wale wanaofanya vitendo hivyo.
  • Ushahidi unaonesha kwamba vikundi thabiti vya kutetea haki za wanawake ni muhiu sana katika kutokomeza ukatili dhdi ya wanawake na wasichana.
  • Jukwaa la Kizazi cha usawa  linahitaji msaada ili kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na wasichana.
Romela Islam alimtoroka ndoa yake ya kikatili baada ya kaka yake kumchukua na kumhamishia kituo cha kuhifadhi manusura wa ukatili Bangladesh
UN Women/Fahad Kaizer
Romela Islam alimtoroka ndoa yake ya kikatili baada ya kaka yake kumchukua na kumhamishia kituo cha kuhifadhi manusura wa ukatili Bangladesh

“Nakiri kuwa ni vigumu, lakini kwa msaada wa kifikra, kisheria na mafunzo ya stadi nimepona mno,” anaeleza Diana.

Huduma za msingi kwa manusura wa ukatili wa majumbani ni muokozi wa maisha.

“Sasa hivi sijioni tena kama mfungwa niliyewekwa mahali na kusalitiwa. Kuna mambo mengi yanaendelea kwa anayekumbwa na ukatili ikiwemo athari za kisaikolojia, lakini sasa natambua hilo na naweza kukamilisha chochote kile ambacho nimeamua kufanya.”

Diana ni miongoni mwa wanawake manusura 199 wanaohifadhiwa kwenye kituo cha malazi ambacho kina uhusiaon na mtandao wa vituo vya hifadhi vya Amerika, vikipatiwa msaada na UN Women kupitia mkakati wa Spotlight.

Kituo hicho pia kinatoa msaada wa kisaikolojia na kisheria kwa zaidi ya wanawake 1,057 tangu mwaka 2017.

Soma simulizi ya kina ya Diana hapa.

Manusura sasa wana hamasa na siku za usoni

Wakati huo huo, janga la COVID-19 likiendelea kukumbwa Bangladesh na kuchochea ukatili dhidi ya wanawake na wasichana, idadi kubwa ya vituo vya kuhifadhi manusura wa ukatili au kuwapatia huduma vimefungwa.

Romela ameolewa na mwanaume mkatili. “Nilipokuwa mjamzito, alinipiga kwa nguvu hadi ujauzito ukatoka… nilitaka kujiua,” amesema.

Hatimaye alitoroka pindi kaka yake alipomchukua na kumpeleka kwenye kituo cha kuhifadhi wanawake manusura wa ukatili kiitwacho Tarango kituo ambacho baada ya kuanza kuendeshwa kwa ubia na UN Women kimeweza kupanua wigo wa hudum ahai kutoa makazi ya muda, huduma za kisheria na kijamii na mafunzo ya stadi za kazi kwa wanawake manusura ili waweze kuanza upya maisha yao.

Kuishi na mwenza mkatili mara nyingi kunafifisha fursa za mwanamke kuchagua atakacho maishani. Kunafifisha pia kujiamini.

Sasa Romela amepata pahali ambako anaweza kuishi kwa usalama pamoja na binti yake mwenye umri wa miaka 4.
Kwa kuanza upya maisha yake, watu wengine walianza kumweleza jinsi ya kuvaa, wapi atembelee na jinsi ya kuishi maisha yake. “Sasa natambua mambo yote ambayo nawez akuchagua kwenye maisha yangu,” amesema Romela akiongeza kuwa “ninajiamini na maisha yangu sasa yana raha.”

Tarango inahifadhi manusura kati ya 30 hadi 35 wa ukatili na hutoa huduma saa 24 na siku 7 kwa wiki, msaada ambao unawezesha manusura kuondokana na kiwewe, na kupata tena utu wao, kujifunza stadi mpya na kupata ajira sambamba na msaada wa fedha kwa miezi miwili ili wajijengee mnepo wa kiuchumi.
“Kazi yetu ni kuhakikisha wanawake wanajisikia salama na tunawahudumia kwa heshima na utu wote,” amesema Nazlee Nipa, Mratibu wa Programu Tarango.
Bofya hapa  kusoma zaidi simulizi ya Romela

Layla Bennani baada ya machungu katika uhusiano wa kikatili aliambua kwenda polisi akiambatana na rafiki yake.
UN Women/Mohammed Bakir
Layla Bennani baada ya machungu katika uhusiano wa kikatili aliambua kwenda polisi akiambatana na rafiki yake.

Changamoto kubwa kisheria

Goretti alirejea magharibi mwa Kenya mwaka 2001 ili kumzika mumewe na kwa mujibu wa tamaduni zao, ni lazima abakie kwenye makazi ya familia.
“Lakini hawakunipa chakula. Kila kitu nilichotoka nacho Nairobi, (mji mkuu wa Kenya) ikiwemo nguo, vifaa vya nyumbani, vilichukuliwa na kugawanywa kwa wanafamilia.” Anakumbuka Goretti.
Kwa takribani miaka 20 baada ya kifo cha mume wake, Goretti amenasa katika mtego wa maisha machungu kwa wakwe zake ambao wanampiga kiasi kwamba alilazwa hospitali na kushindwa kufanya kazi.
Kwa hofu ya kwenda kuripoti kwenye vyombo vya sheria, Goretti alisaka ushauri kwa mtetezi wa haki za binadamu, ambaye alimsaidia kupata matibabu na kuripoti kisa chake kwenye mamlaka za mitaa.
Hata hivyo, aligundua kuwa wakwe zake walighushi nyaraka za polisi zinazoonesha makubaliano yake ya kuondoa kesi hiyo polisi. “Lakini siwezi hata kuandika,” amesema Goretti.

Watetezi wa haki za binadamu nchini Kenya ni wa kwanza katika kuchukua hatua dhidi ya ukatili wa kijinsia. Tangu mwaka 2019, ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, OHCRC, imekuwa ikisaidia mashirika ya mashinani kupatia mafunzo ya kisheria na kuwajengea uwezo ili yaweze kusaidia manusura.

Halikadhalika, pamoja na kuripoti visa hivyo polisi na mahakamani, mtetezi wa haki za binadamu Caren Omanga ambaye alipatiwa mafunzo na moja ya mashirika hayo pia aliwasiliana na viongozi wa kijamii.

“Ilikuwa nusura nikamatwe kwa kuwasiliana na ofisi mhusika,” anasema Bi. Omanga. Lakini kwa kutambua kuwa jamii itakuwa kinzani na Goretti nilianzisha mchakato mwingine mbadala wa kusaka suluhu huku nikisongesha kesi mahakamani,” amesema Omanga.

Hatimaye, kesi yake ilisuluhishwa mahakamani, Goretti aliapta mkataba wa kumkabidhi mali zake na hati ya ardhi ambayo alipoteza kupitia mahari. Watekelezaji wa vitendo hivyo dhidi yake walitakiwa kulipa faini ili wasiende gerezani.
“Ni sawa na kuanza upya maisha baada ya miaka 20, na mwanangu mvulana anajiona yuko salama zaidi. Nafikiria kupanda miti ili kulinda eneo langu la ardhi na kujenga banda la kufugia kuku,” amesema Goretti.
Soma kwa kina simulizi ya Gorett hapa.

Kwa manusura wengine wawili, mmoja kutoka Moldova bofya hapa na kutoka Morocco bofya hapa

Unaweza kusoma simulizi hizo kutoka wavuti wa UN Women.