Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Apu ya t-bu Lite yaleta mapinduzi katika tiba dhidi ya Kifua Kikuu au TB nchini Kenya

Mashine kwa udhamini wa Global Fund ili kupambana na VVU, Kifua Kikuu na Malaria inawasaidia maafisa wa afya wa gereza la Pollsmoor Afrika Kusini kuwapima na kuwatibu wafungwa
Photo: The Global Fund/John Rae
Mashine kwa udhamini wa Global Fund ili kupambana na VVU, Kifua Kikuu na Malaria inawasaidia maafisa wa afya wa gereza la Pollsmoor Afrika Kusini kuwapima na kuwatibu wafungwa

Apu ya t-bu Lite yaleta mapinduzi katika tiba dhidi ya Kifua Kikuu au TB nchini Kenya

Afya

Kongamano la kimataifa la wataalam wa ugonjwa wa kifua kikuu au TB limefanyika mjini Nairobi Kenya kujadili mbinu mujarabu za kuimarisha ushirikiano kati ya sekta binafsi na sekta za umma kwenye mapambano dhidi ya ugonjwa huo hatari huku apu ya t-bu Lite ikitajwa kuleta mapinduzi katika tiba.

Kifua kikuu husambazwa kupitia hewa pale mtu anapovuta iliyo na bakteria aina ya Mycobacterium tuberculosis wakati wa kukohoa. 

Kwa mujibi wa shirika la Umoja wa Mataifa la afya la duniani WHO, TB ni moja ya magonjwa 10 yanayosababisha vifo vingi duniani.  

Kwa kiasi kikubwa kifua kikuu huathiri mapafu lakini sehemu nyengine mwilini pia zinaweza kuambukizwa.  

Takwimu za WHO zinaonyesha kuwa idadi kubwa zaidi ya wagonjwa wa kifua kikuu duniani ni watu wazima na wengi wao ni wanaume. 

Orodha ya mataifa 30 yaliyoathirika zaidi 

WHO imeiondoa Kenya na mataifa mengine 5 kwenye orodha ya mataifa 30 yaliyo na visa vingi vya wagonjwa wa kifua kikuu duniani. 

WHO kwenye taarifa yake ya mwaka wa 2022 imeelezea kuwa kwa mataifa mengine, hali ilikuwa mbaya zaidi ukizingatia athari za janga la corona au COVID-19.  

Mary Nzamalu ni afisa wa matibabu na msimamizi wa mpango wa kifua kikuu kwenye kaunti ya Nairobi anafafanua kuwa,”Kwa sasa wagonjwa wakija wanapimwa COVID 19 na kifua kikuu kwa pamoja maana dalili zinafanana. Idadi ya walioambukizwa imeongezeka kwasababu waliokuwa hawawezi kufika hospitalini kwasababu ya vikwazo vya corona sasa wana uhuru wa kutembea na wanapata huduma.” 

Wataalam wa WHO wakiwa hospitali ya Mater walikotembelea maabara ya kupima TB
UN/ Thelma Mwadzaya
Wataalam wa WHO wakiwa hospitali ya Mater walikotembelea maabara ya kupima TB

Juhudi zahitajika maradufu 

Kwenye taarifa yake, shirika la WHO, linasisitizia umuhimu wa kutenga fedha zaidi za kupambana na kifua kikuu haraka iwezekanavyo ukizingatia madhila ya janga la COVID 19.  

Mwaka 2021 watu milioni 10.6 waliugua kifua kikuu, idadi ambayo ni ongezeko la asilimia  4.5% kutokea mwaka ulopita wa 2020.  

Ripoti ya WHO inabainisha kuwa watu milioni 1.6 walikufa kwa  kifua kikuu au TB katika kipindi hicho. Kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka kadhaa, idadi ya wanaougua Kifua kikuu na kifua kikuu sugu imeongezeka. Kwa mujibu wa WHO idadi ya maambukizi mapya ya kifua kikuu sugu iliongezeka kati ya mwaka 2020 na 2021. 

Kwa mantiki hiyo shirika hilo la afya linasema, idadi kubwa ya walioambukizwa kifua kikuu hawakupimwa na kutibiwa.  

Mike Macharia ni Meneja wa kiufundi katika mpango wa Komesha TB nchini Kenya unaofadhiliwa na Marekani na anaelezea umuhimu wa matumizi ya teknolojia katika vita dhidi ya kifua kikuu na kusisitiza kuwa,”Apu hii  t-bu Lite inamuwezesha mhudumu wa afya kumsajili mgonjwa, kunakili maelezo yake, kuhifadhi takwimu na kumwelekeza kwenye kituo cha afya kilicho karibu naye kokote ndani ya mipaka ya Kenya. Hii ina maana hata pale anapohama sehemu bado maelezo yapo na wataalam wa afya wana uwezo wa kuarifiwa anapotokea mgonjwa wa kifua Kikuu.” 

Kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa nembo ya kutokomeza Kifua Kikuu ikiwa imewekwa.
UN News/Daniel Dickinson
Kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa nembo ya kutokomeza Kifua Kikuu ikiwa imewekwa.

Apu ya t-bu Lite

Apu ya t-bu Lite imeleta tija hasa katika kuhifadhi takwimu na ufuatiliaji wa wagonjwa wa Kifua Kikuu kokote waliko ndani ya mipaka ya Kenya.  

Takwimu zinaashiria kuwa mwaka 2021 idadi ya maambukizi ya Kifua kikuu yalipungua ila bado hayakufikia viwango vya kabla ya janga la corona kuzuka. 

Hali kwamba idadi ya walioambukizwa TB imepungua inaashiria kuwa ambao hawajapimwa na kutibiwa wameongezeka na hatimaye kusababisha ongezeko la vifo.  

Shirika la afya linasema hii ina maana kuwa baada ya muda idadi ya walioambukizwa Kifua Kikuu itaongezeka. 

Steven Shikoli aliugua Kifua Kikuu mwaka 2009 na akapona baada ya matibabu. Familia yake ilimtenga lakini aliungwa mkono na wahudumu wa afya na hali yake ikaimarika.  

Steven anasema kuwa,”Nilitengwa na familia yangu walipogundua kuwa nimeambukizwa Kifua Kikuu.Hata hivyo wahudumu wa afya walinishika mkono na nikaweza kutumia dawa inayotakikana na nikapona.Kwa sasa kuna mabadiliko mengi kwani hata tiba ya TB imekuwa na uepesi zaidi kwa wagonjwa.Awali nililazimika kutoa kikohozi mara kadhaa kupimwa ila kwa sasa ni mara moja na majibu yanatoka baada ya saa chache tu.Uhamasisho na elimu kwa jamii pia ni mambo yaliyochangia kwa umma kuuelewa ugonjwa wa TB ambao una tiba na unapona hata ukiambukizwa mara mbili.Sindano pia zile za muda mrefu hakuna tena na hilo limesaidia.” 

WHO inashikilia kuwa ripoti yake ya mwaka 2022 inaweka bayana umuhimu wa kushirikiana na kuimarisha maradufu juhudi za kupambana na kifua kikuu ili kuokoa maisha.