Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

COP27 yafikia tamati kwa kufanya maamuzi makubwa kuhusu ‘hasara na uharibifu’ 

COP27 yakamilisha kazi yake huko Sharm el-Sheikh, Misri kwa kufanya maamuzi makubwa.
Kiara Worth
COP27 yakamilisha kazi yake huko Sharm el-Sheikh, Misri kwa kufanya maamuzi makubwa.

COP27 yafikia tamati kwa kufanya maamuzi makubwa kuhusu ‘hasara na uharibifu’ 

Tabianchi na mazingira

Baada ya siku kadhaa za mazungumzo makali yaliyoendelea hadi Jumapili asubuhi kwa saa za Sharm el-Sheikh, Misri, nchi katika mkutano wa 27 wa nchi wanachama wa Mkataba wa mabadiliko ya tabianchi, COP27, zimefikia makubaliano kuhusu matokeo ambayo yalianzisha utaratibu wa ufadhili wa kufidia walioko katika hatari ya 'hasara na uharibifu' kutokana na majanga ya tabianchi yanayosababishwa na wanadamu.

"COP hii imechukua hatua muhimu kuelekea haki. Ninakaribisha uamuzi wa kuanzisha mfuko wa hasara na uharibifu na kuufanyia kazi katika kipindi kijacho.” Amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika ujumbe wake wa video uliooneshwa kwenye ukumbi wa mikutano nchini Misri, akisisitiza kwamba sauti za wale walio mstari wa mbele katika janga la tabianchi lazima zisikilizwe. 

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa alikuwa akirejelea kile ambacho kiliishia kuwa suala gumu zaidi katika COP hii, ikiwa ni mwendelezo wa wa Mkutano wa kila mwaka wa Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC). 

Nchi zinazoendelea zilitoa wito wenye nguvu na unaorudiwa wa kuanzishwa kwa mfuko wa hasara na uharibifu, ili kufidia nchi ambazo ziko hatarini zaidi kwa majanga ya tabianchi, lakini ambazo zimechangia kidogo katika janga la tabianchi. 

"Ni wazi kuwa hii haitatosha, lakini ni ishara ya kisiasa inayohitajika kujenga upya uaminifu uliovunjika." Amesema Bwana Guterres, akisisitiza kwamba mfumo wa Umoja wa Mataifa utaunga mkono juhudi kila hatua. 

Baada ya kushindwa kufikia muafaka  katika muda uliokuwa umepangwa Ijumaa usiku, hatimaye waliweza kufikia hitimisho juu ya vipengele vigumu zaidi vya ajenda, ikiwa ni pamoja na kituo cha hasara na uharibifu - ingawa jinsi utaratibu huu utakavyofadhiliwa bado unajadiliwa - pamoja na lengo la ufadhili baada ya mwaka 2025 na kile kinachoitwa programu ya kazi ya kupunguza kwa haraka zaidi uzalishaji wa hewa chafuzi, itachochea hatua yenye athari, na uhakikisho salama kutoka kwa nchi muhimu kwamba zitachukua hatua za haraka ili kuinua matamanio na kuuweka ulimwengu kwenye njia ya kuelekea nyuzi joto 1.5 za selsiasi. 

Hata hivyo, ingawa makubaliano ya ufadhili wa hasara na uharibifu yamekuwa mafanikio kwa walio hatarini, kulikuwa na kusogea kudogo kwa COP27 juu ya masuala mengine muhimu yanayohusiana na sababu za ongezeko la joto duniani, hasa juu ya kuondokana na nishati ya mafuta kisukuku, na lugha kali juu ya haja ya kupunguza ongezeko la joto duniani hadi nyuzi joto 1.5 za Selsiasi. 

Mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi yanaendelea 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameukumbusha ulimwengu juu ya kile ambacho kimesalia kuwa vipaumbele kuhusu hatua ya mabadiliko ya tabianchi ikiwa ni pamoja na azma ya kupunguza utoaji wa gesi chafuzi duniani na kuweka hai kikomo cha nyuzi joto 1.5 za Selsiasi cha Mkataba wa Paris, na kuvuta ubinadamu "kutoka kwenye ukingo wa tabianchi". 

"Tunahitaji kupunguza kwa kiasi kikubwa uzalishaji wa gesi chafuzi sasa - na hili ni suala ambalo COP haikushughulikia," amelalamika, akisema kwamba dunia bado inahitaji kupiga hatua kubwa juu ya matamanio ya tabianchi na kukomesha uraibu wake wa nishati ya mafuta kwa kuwekeza “kwa kiasi kikubwa” katika nishati zinazoweza kurejeshwa. 

Katibu Mkuu Guterres pia amesisitiza haja ya kutekeleza ahadi iliyocheleweshwa kwa muda mrefu ya dola bilioni 100 kwa mwaka katika ufadhili wa tabianchi kwa nchi zinazoendelea, kuweka wazi mpango wa kuaminika wa kuongeza ufadhili mara mbili wa kukabiliana na hali. 

Pia amesisitiza umuhimu wa kubadilisha mifumo ya biashara ya benki za maendeleo ya kimataifa na taasisi za fedha za kimataifa. 

Sayari yetu bado iko kwenye chumba cha dharura. 

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesema kwamba wakati mfuko wa hasara na uharibifu ni muhimu, sio jibu ikiwa janga la tabianchi litaondoa kisiwa kidogo kwenye ramani - au kugeuza nchi nzima ya Afrika kuwa jangwa. 

Amerejelea wito wake wa ushirikiano wa mpito wa nishati ili kuharakisha uondoaji wa makaa ya mawe na kuongeza vitu vinavyoweza kurejeshwa na akasisitiza wito alioutoa kwenye hotuba yake ya ufunguzi katika COP27: mkataba wa mshikamano wa hali ya hewa. 

"Mkataba ambao nchi zote zinafanya juhudi za ziada kupunguza utoaji wa hewa chafuzi katika muongo huu kulingana na lengo la nyuzi joto1.5. Na Mkataba wa kuhamasisha, pamoja na taasisi za fedha za kimataifa na sekta ya kibinafsi – msaada wa kifedha na kiufundi kwa mataifa makubwa yanayoinukia kiuchumi ili kuharakisha mpito wao wa nishati mbadala.” amefafanua, akisisitiza kwamba hii ni muhimu ili kuweka kikomo cha nyuzi joto 1.5 kufikiwa. 

Muda unayoyoma 

Katika ujumbe wake wa video, Bwana Guterres ameangazia kwamba COP27 imehitimishwa ikiwa na "kazi nyingi za kwenda kufanya nyumbani" ambazo bado zinapaswa kufanywa na kukiwa na muda mchache wa kuifanya. 

"Tayari tuko katikati ya Makubaliano ya [2015] ya Tabianchi] ya Paris na mwaka wa mwisho ni 2030. Tunahitaji ushiriki wa moja kwa moja ili kuendesha haki na matamanio.” Amesema Bwana Guterres. 

Katibu Mkuu ameongeza kuwa hii ni pamoja na nia ya kumaliza "vita ya kujitoa mhanga" dhidi ya asili ambavyo vinachochea janga la tabianchi, kusababisha viumbe kutoweka na kuharibu mifumo ya ikolojia. 

"Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Baionuai wa mwezi ujao ni wakati wa kupitisha mfumo kabambe wa bayoanuwai wa kimataifa kwa muongo ujao, unaotokana na nguvu ya ufumbuzi wa asili na jukumu muhimu la jumuiya za kiasili." Amehimiza. 

‘Niko pamoja na nanyi’ 

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa pia ametuma ujumbe kwa mashirika ya kiraia na wanaharakati ambao wamekuwa wakizungumza tangu siku ya ufunguzi wa mkutano huo: "Niko pamoja nanyi katika mafadhaiko yenu". 

Bwana Guterres amesema kwamba wachechemuzi wa tabianchi - wakiongozwa na sauti ya maadili ya vijana - wameweka ajenda katika siku za giza na lazima walindwe. 

"Chanzo cha nishati muhimu zaidi ulimwenguni ni nguvu ya watu. Ndio maana ni muhimu sana kuelewa mwelekeo wa haki za binadamu wa hatua za hali ya hewa," amesema, akiongeza kuwa vita vilivyo mbele vitakuwa vikali na kwamba" itachukua kila mmoja wetu kupigana kwenye mitaro kila siku, hatuwezi kungoja muujiza.” 

Akitoa maoni haya, mwanaharakati wa vijana wa mazingira wa Kenya Elizabeth Wathuti, alisema: “COP27 inaweza kumalizika, lakini mapambano ya mustakabali salama bado. Sasa ni jambo la dharura zaidi kuliko hapo awali kwamba viongozi wa kisiasa wafanye kazi kuafikiana makubaliano madhubuti ya kimataifa ya kulinda na kurejesha asili katika Mkutano ujao wa Baionuai ‘Global Biodiversity Summit’ huko Montreal. 

Bi. Wathuti aliongeza kusema "tatizo lililounganishwa la chakula, asili na tabianchi kwa sasa linatuathiri sote - lakini jamii zilizo mstari wa mbele kama yangu ndio zimeathirika zaidi. Ni kengele ngapi za hatari zinahitaji kupigwa kabla ya kuchukua hatua?" 

Mengine yaliyofikiwa  

COP27 ilikusanya zaidi ya watu 35,000, wakiwemo wawakilishi wa serikali, waangalizi na mashirika ya kiraia. 

Muhtasari wa mkutano huo ulijumuisha, miongoni mwa mambo mengine, kuzinduliwa kwa ripoti ya kwanza ya Kikundi cha Wataalamu wa Ngazi ya Juu kuhusu Ahadi za Uzalishaji-Sifuri wa hewa chafuzi. 

Pia wakati wa Mkutano huo, Umoja wa Mataifa ulitangaza Mpango wa Utendaji wa Utekelezaji wa Maonyo ya Mapema kwa Wote, ambao unataka uwekezaji mpya wa awali uliolengwa wa dola za kimarekani bilioni 3.1 kati ya mwaka 2023 na 2027, sawa na gharama ya senti 50 tu kwa kila mtu kwa mwaka. 

Wakati huo huo, Makamu wa Rais wa zamani wa Marekani na mwanaharakati wa tabianchi Al Gore, akiungwa mkono na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, aliwasilisha  mpya huru ya utoaji wa gesi chafuzi iliyoundwa na Muungano wa Hali ya Hewa TRACE. 

Vifaa kwa kutumia data ya satelaiti na akili bandia ili kuonesha utoaji wa hewa chafuzi wa vituo zaidi ya 70,000 duniani kote, ikiwa ni pamoja na makampuni nchini China, Marekani na India. Hii itawawezesha viongozi kutambua eneo na upeo wa utoaji wa hewa ukaa na methane inayotolewa kwenye angahewa. 

Kivutio kingine cha mkutano huo kilikuwa kile kinachoitwa mpango mkuu wa kuharakisha uondoaji kaboni au hewa ukaa katika sekta kuu tano - umeme, usafiri wa barabara, chuma, hidrojeni, na kilimo - uliowasilishwa na Urais wa COP27 wa Misri. 

Uongozi wa Misri pia ulitangaza kuzindua mpango wa Chakula na Kilimo kwa Mabadiliko Endelevu au FAST, ili kuboresha idadi na ubora wa michango ya tabianchi ili kubadilisha mifumo ya kilimo na chakula ifikapo 2030. 

Hii ilikuwa COP ya kwanza kuwa na siku maalum ya Kilimo, ambayo inachangia theluthi moja ya uzalishaji wa hewa chafu na inapaswa kuwa sehemu muhimu ya suluhisho. 

Mipango mingine iliyotangazwa katika COP27 ni pamoja na: 

• Ajenda ya Sharm El-Sheik 

• Hatua yaMpango wa Kukabiliana na Maji na Mnepo (AWARe) 

• Mpango wa Soko la Kaboni Afrika (ACMI) 

• Kampeni ya Kuongeza Kasi ya Bima 

• Muungano wa Nishati Jadidifu za Ulimwengu