Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Msilazimishe wasaka hifadhi kurudi Mashariki mwa DRC: UNHCR

Familia ikiwa kwenye makazi yao huko jimboni Ituri nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC kufuatia shambulio kubwa kwenye kambi ya wakambizi mwezi Februari mwaka huu wa 2022.
© UNHCR/Hélène Caux
Familia ikiwa kwenye makazi yao huko jimboni Ituri nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC kufuatia shambulio kubwa kwenye kambi ya wakambizi mwezi Februari mwaka huu wa 2022.

Msilazimishe wasaka hifadhi kurudi Mashariki mwa DRC: UNHCR

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR limerejea wito wake kwa kupiga marufuku kulazimisha wasaka hifadhi kurudi makwao kwa nguvu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC, ikiwa ni pamoja na wasaka hifadhi ambao madai yao yamekataliwa, katika majimbo ya Kivu Kaskazini, Kivu Kusini, na Ituri.

Katika mkutano wake na waaandishi wa Habari jijini Geneva Uswisi hii leo Mkurugenzi wa Ulinzi wa kimataifa wa UNHCR Elizabeth Tan amesema wanatoa wito kwa serikali kuwashughulikia watu hao kama wakimbizi na waruhusiwe kuingia maeneo wanayoomba hifadhi kwa mujibu wa Mkataba wa OAU wa mwaka 1969 unaosimamia Masuala Maalum ya Matatizo ya Wakimbizi Barani Afrika.

Bi Tan amesema watu wengi wanaokimbia machafuko DRC wana uwezekano mkubwa wa kukidhi vigezo vya Mkataba wa mwaka 1951 wa hali ya ukimbizi.

Mataifa yana wajibu wa kisheria na kimaadili kuwaruhusu wale wanaokimbia migogoro inayoendelea kutafuta usalama, kupewa hifadhi kwa mujibu wa Mkataba wa OAU wa 1969, na kama inavyotumika, chini ya Mkataba wa Wakimbizi wa 1951, na kutowarudisha wakimbizi kwa lazima.

UNHCR wamesema ushauri huu wanaoutoa dhidi ya wasaka hifadhi kulazimishwa kurejea katika majimbo ya Kivu Kaskazini, Kivu Kusini na Ituri nchini DRC utaendelea kutumika hadi hali itakapoimarika vya kutosha kuruhusu kurudi kwa usalama na heshima.

Mashambulizi ya raia yaongezeka

UNHCR pia imeeleza wasiwasi wake kuhusu kuongezeka kwa mashambulizi dhidi ya raia, ikiwa ni pamoja na wale wanaoishi katika kambi za wakimbizi wa ndani mashariki mwa DRC.

Watoto wakicheza kwenye moja ya kambi za wakimbizi wa ndani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC
© UNICEF/Gwenn Dubourthoumi
Watoto wakicheza kwenye moja ya kambi za wakimbizi wa ndani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC

“Katika shambulio la kutisha kama lililotokea kwenye kambi ya Plaine Savo, jimboni Ituri mwezi Februari 2022, kundi lisilo la serikali liliwaua watu wasiopungua 62 na kuwajeruhi zaidi ya wengine 40.” Ameeleza Mkurugenzi huyo wa Ulinzi wa Kimataifa wa UNHCR

Ameongeza kuwa “Tangu Februari, mashambulio kama haya yamesababisha vifo vya zaidi ya 1,000 vya watu waliojificha katika kambi za wakimbizi au waliojaribu kurejea makwao. Tangu mwanzoni mwa mwaka 2022, UNHCR imerekodi kezi za ukiukwaji dhidi ya haki za raia zaidi 50,000 ikiwa ni pamoja na wakimbizi na wakimbizi wa ndani.”

Kuongezeka kwa migogoro ya silaha 

Tangu tarehe 20 Oktoba, watu 188,000 wamekimbia makazi mapya kutokana na mapigano kati ya kundi la waasi la M23 na Jeshi la Kongo. Hata kabla ya ongezeko la hivi karibuni la watu kuhama, takriban Wakongo milioni 5.6 walikuwa wakimbizi wa ndani.

Wengine milioni 1 wamepata hifadhi katika nchi 22 barani Afrika, na kuifanya kuwa moja ya majanga makubwa zaidi ya kibinadamu ulimwenguni.

Idadi kubwa ya watu, milioni 4.9, walikuwa wakimbizi wa ndani kwa sababu ya migogoro katika Kivu Kaskazini, Kivu Kusini na Ituri huku karibu 700,000 wameyahama makazi yao kutokana na hali mbaya ya hewa.