Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mpango mpya wa IFC na UNHCR wa kuongeza ushiriki wa sekta binafsi kwa wakimbizi na jamii zinazowahifadhi

Serafina, mkimbizi wa Burundi anayeishi katika makazi ya Kalobeyei nchini Kenya, alifungua kibanda cha mboga mwaka 2019 kwa kutumia mkopo wa masharti nafuu kutoka kwa washirika wa sekta binafsi wa UNHCR.
© UNHCR/Pauline Omagwa
Serafina, mkimbizi wa Burundi anayeishi katika makazi ya Kalobeyei nchini Kenya, alifungua kibanda cha mboga mwaka 2019 kwa kutumia mkopo wa masharti nafuu kutoka kwa washirika wa sekta binafsi wa UNHCR.

Mpango mpya wa IFC na UNHCR wa kuongeza ushiriki wa sekta binafsi kwa wakimbizi na jamii zinazowahifadhi

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR na Shirika la Kimataifa la Usimamizi wa Fedha (IFC) ambalo ni miongoni mwa taasisi za Benki Kuu ya Dunia leo wametangaza mpango wa pamoja wa kuunda fursa shirikishi za kiuchumi ambazo zitawanufaisha wakimbizi na jumuiya zinazowahifadhi, imeeleza taarifa iliyotolewa Ijumaa leo na UNHCR mjini Geneva, Uswisi.

Taarifa hiyo imeeleza pia kuwa miongoni mwa malengo mengine, mpango huo unalenga kuhamasisha miradi ya sekta binafsi katika kipindi cha miaka mitano ijayo ili kuonesha uwezekano wa uwekezaji katika mazingira ya kulazimishwa kuhama. 

Uhamisho wa kulazimishwa au kufurushwa ni janga ambalo linakua ambalo ni kubwa sana na tata kwa serikali na mashirika ya kibinadamu kuutatua peke yao. Kufikia katikati ya mwaka 2022, zaidi ya watu milioni 103 walilazimika kuyahama makazi yao duniani kote, huku asilimia 74 kati yao wakiwa katika nchi za kipato cha chini na cha kati. 

Mpango wa pamoja utakuza ushirikishanaji maarifa ili kuwezesha ushirikishwaji wa wadau wa sekta binafsi katika maeneo yanayohifadhi wakimbizi. Mpango huo utahusisha utaalamu wa sekta binafsi, ufadhili, na uvumbuzi ili kuboresha hali ya maisha kwa wale waliofurushwa kwa lazima na pia wenyeji wao, kupitia uundaji wa nafasi za kazi, huduma bora na za bei nafuu, miundombinu ya ufadhili, na mtaji unaohitajika sana kwa biashara ndogo na za kati. 

"Sekta binafsi ina mengi ya kutoa na mengi ya kupata katika masoko," amesema Mkurugenzi Mkuu wa IFC Makhtar Diop akiongeza kuwa, “biashara hutengeneza nafasi za kazi na kutoa ufikiaji endelevu wa bidhaa na huduma muhimu ambazo zinanufaisha wakimbizi na wenyeji wao. Uzinduzi wa Mpango huu mpya wa Pamoja wa IFC-UNHCR unawakilisha dhamira yetu ya kuongeza msaada wetu na kuunda masuluhisho endelevu ya sekta ya kibinafsi kwa baadhi ya jamii zilizo hatarini zaidi kwenye sayari.” 

Naye Kamishna Mkuu wa UNHCR Filippo Grandi amenukuliwa akisema, “Hii ni hatua muhimu kuelekea kugawana majukumu zaidi na kutafuta suluhu za kiutendaji kwa wale wanaolazimika kukimbia. Katika kukabiliwa na mizozo mingi ulimwenguni, lazima tufanye kazi karibu zaidi na sekta binafsi ili kuongeza uwezo wao na hamu yao ya kusaidia. Ninaishukuru IFC kwa uongozi wake na kujitolea kwa mustakabali mwema kwa waliofurushwa na pia wenyeji wao.” 

IFC na UNHCR wamekuwa wakifanya kazi pamoja tangu mwaka 2016 ili kuboresha maisha ya wale waliofurushwa kwa lazima na pia wenyeji wao, kutekeleza miradi nchini Brazil, Colombia, Ethiopia, Jordan, Kenya, Uganda, Iraq na Lebanon. Kwa mfano, “nchini Kenya, kazi ya pamoja ya IFC na UNHCR ilisaidia kuvutia biashara za binafsi kwenye eneo la kuhifadhi wakimbizi la Kakuma Kalobeyei, kuunda nafasi za kazi na kuimarisha upatikanaji wa huduma kwa wakimbizi na jumuiya zinazowapokea. Nchini Colombia, ushirikiano huo umewezesha upatikanaji wa bidhaa na huduma za kifedha kwa wakimbizi na wahamiaji wa Venezuela nchini humo, na kuwaruhusu kuchangia katika uchumi wa Colombia.” 

Tangazo la leo litaruhusu IFC na UNHCR kutumia rasilimali zao za kimataifa na kuongeza juhudi zao kusaidia watu waliofurushwa kwa nguvu kuishi maisha ya utu zaidi, huku wakichangia maendeleo ya uchumi wa ndani na masoko, kwa kuzingatia ari ya Mkataba wa Kimataifa wa Wakimbizi.