Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uokaji mikate kwangu ni zaidi ya riziki ni thibitisho, kuwa mkimbizi sio kulemaa: Shebulike

Kavugwa Shebulike Cadet, muokaji na mkimbizi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo akiwa na mkate wake mpya uliookwa katika kambi yake ya kuoka mikate katika kambi ya wakimbizi ya Nyankanda.
© UNHCR/Samuel Otieno
Kavugwa Shebulike Cadet, muokaji na mkimbizi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo akiwa na mkate wake mpya uliookwa katika kambi yake ya kuoka mikate katika kambi ya wakimbizi ya Nyankanda.

Uokaji mikate kwangu ni zaidi ya riziki ni thibitisho, kuwa mkimbizi sio kulemaa: Shebulike

Wahamiaji na Wakimbizi

Muokaji mikate mkimbi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC anawapa mkate wa kila siku wakimbizi wenzake wanaopata hifadhi nchini Burundi na wenyeji, huku akijipatia kipato kwa familia yake, na kulinda hadhi yake. Kupitia biashara ya duka la mikate au bekari aliyoifungua. 

"Mkate wangu ndio bora zaidi kambini na kwa maili  nyingi karibu na hapa!" Anasema Kavugwa Shebulike Cadet huku akitabasamu kwa fahari. "Watu wanapoonja mkate wangu, husema, sasa huu ni mkate na kila wakati hurudi kwa ajili ya kupata zaidi." 

Shebulike alikuwa akiishi Uvira, mashariki mwa DRC wakati watu wenye silaha walipovamia nyumba yake usiku mmoja.  

Anakumbuka kilichotokea akisema "Walinipiga risasi na kuniacha wakidhania kuwa nimekufa na kabla ya kuondoka walichukua pesa na vitu vyangu vyote vya thamani. Pia walimchoma kisu mke wangu kwenye mkono." 

Shambulio hilo wiki chache baadaye lithibitisha kuwa imetosha kwa Shebulike ambaye aliamua yeye na familia yake kuzipa kisogo vurugu na uvunjaji sheria  DRC na kufungasha virago na kushika njia kuelekea kwenye usalama nchi jirani ya Burundi. 

Muokoaji mkate, Kavugwa Shebulike Cadet anaandaa tanuri lake la udongo kwa ajili ya kuoka.
© UNHCR/Samuel Otieno
Muokoaji mkate, Kavugwa Shebulike Cadet anaandaa tanuri lake la udongo kwa ajili ya kuoka.

"Tulikimbia usiku wa manane na tuliweza kuvuka mpaka baada ya kutembea kwa saa kadhaa, tukiwa na hofu katika matumbo yetu, huku mikono na mifuko yetu ikiwa mitupu," anasema.  

Shebulike tangu wakati huo ameishi katika kambi ya wakimbizi ya Nyankanda, mashariki mwa Burundi,ambako ni nyumbani kwa takriban wakimbizi 12,000 wa Congo DRC. 

Miezi michache baada ya kuwasili Burundi, Shebulike alitambua kwamba alihitaji kumtunza mke wake na watoto saba kwa kujishughulisha, hivyo akarudia kazi yake ya kuoka mikate.  

"Badala ya kukaa bila kazi na kutegemea tu usaidizi tunaopokea kutoka kwa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi (UNHCR) na mashirika mengine ya kibinadamu, niliona ni muhimu kukunja shati la mikono yangu na kufanyia kazi jambo ninalolijua zaidi," anasema.  

Shebulike na wafanyakazi wake na wanafunzi wakitayarisha unga kwenye duka lake la kuoka mikate kambini.
© UNHCR/Samuel Otieno
Shebulike na wafanyakazi wake na wanafunzi wakitayarisha unga kwenye duka lake la kuoka mikate kambini.

Shebulike alikusanya akiba yake yote kiasi cha faranga 40,000 tu za Burundi, sawa na dola za Marekani 20 na kukopa dola zingine 40 kutoka kwa rafiki yake.  

Alipozikusanya pamoja, zikatosha kununua unga wa ngano, mafuta ya kupikia, maji na hamira  na hivyo kuoka mikate yake safi ya kwanza kwa kutumia unga kilo sita. 

Haikuchukua muda kupata wateja na mara sifa zake zikaenea kila kona ya kambi na nje ya kambi hiyo ya Nyankanda.  

"Tuna wateja waaminifu hadi Ruyigi, zaidi ya kilomita 10 kutoka kambini hapa," anasema. 

Hakuna kitu kinapikwa nusu nusu linapokuja swala la mikate ya Kavugwa Shebulike Cadet.
© UNHCR/Samuel Otieno
Hakuna kitu kinapikwa nusu nusu linapokuja swala la mikate ya Kavugwa Shebulike Cadet.

Na kwa msaada wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR kupitia mshirika wake RET international Shebulike akaweza kupanua biashara yake , kuajiri wanagegenzi 13 na kuongeza ushalishaji hadi kufikia kilo 50 kwa siku akitumia oveni mpya na yenye uwezo mkubwa kuoka mikate yake, vifaa bora vya kupikia na vikolombwezo vingi zaidi. 

Shebulike anasisitiza kuwa huu ni mwanzo tu wa biashara yake ya duka la kuoka na kuuza mikate. 

Anatumai kuiendeleza na kuiongeza biashara hiyo ilia pate wateja wengi zaidi , lakini ukosefu wa umeme na vikwazo vya wakimbizi kutembea huko na kule imekuwa mtihani mkubwa kwake.  

Hivi sasa UNHCR inachagiza kuunganisha makambi ya wakimbizi nchini Burundi na umeme wa gridi ya taifa na kupata nafasi ya kuongeza wigo wa fursa za biashara na kiuchumi kwa wakimbizi nje ya makambi. 

Kavugwa Shebulike Cadet, akiandaa mikate kwa ajili ya kuoka katika kambi ya wakimbizi ya Nyankanda nchini Burundi.
© UNHCR/Samuel Otieno
Kavugwa Shebulike Cadet, akiandaa mikate kwa ajili ya kuoka katika kambi ya wakimbizi ya Nyankanda nchini Burundi.

Kwa Shebulike, kuoka ni zaidi ya riziki yake ya kila siku, kunawakilisha taaluma na ujuzi, uhuru na kujitegemea.  

"Kuwa mkimbizi sio kuwa mlemavu. Sio mwisho wa dunia. Mimi ni thibitisho lililo hai kwamba unaweza kuwa mkimbizi na kutimiza mambo makubwa. Sijui mkimbizi yeyote ambaye anataka kukaa katika hali ya hatari na tegemezi kwa muda usiojulikana." Anasema  

Ziara za kanda hiyo mwaka jana za Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa kuhudumia wakimbizi, Filippo Grandi, na naibu Kamishna mkuu Kelly T. Clements, zilionyesha ufadhili mdogo wa kukabiliana na hali ya wakimbizi nchini Burundi, na kutoa wito wa kuongezwa msaada wa wafadhili kwa wakimbizi kama vile Shebulike, ambao wanahitaji usaidizi mdogo tu ili kuleta mabadiliko makubwa kwa familia zao, wakimbizi wenzao, na jamii inayowakaribisha.