Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukame na ghasia vyalazimu watu 80,000 kukimbilia kambi ya Dadaab nchini Kenya wakitokea Somalia.

Mama huyu mdogo alitembea kwa siku 20 kutoka Diinsoor, Somalia, akiwa na watoto wake saba kuelekea kambi ya wakimbizi ya Hagadera huko Dadaab, Kenya. Baada ya mifugo ya mumewe kufariki kwa sababu ya ukame nchini Somalia, aliwatuma Dadaab kwa sababu hakuw…
Meridith Kohut
Mama huyu mdogo alitembea kwa siku 20 kutoka Diinsoor, Somalia, akiwa na watoto wake saba kuelekea kambi ya wakimbizi ya Hagadera huko Dadaab, Kenya. Baada ya mifugo ya mumewe kufariki kwa sababu ya ukame nchini Somalia, aliwatuma Dadaab kwa sababu hakuweza kuwalisha. (Maktaba)

Ukame na ghasia vyalazimu watu 80,000 kukimbilia kambi ya Dadaab nchini Kenya wakitokea Somalia.

Wahamiaji na Wakimbizi

Zaidi ya raia 80,000 wa Somalia wamewasili katika kambi ya wakimbizi ya Daadab nchini Kenya, katika kipindi cha miaka miwili iliyopita wakikimbia ukosefu wa usalama na ukame nchini mwao, na kati yao hao 24,000 wamewasili tangu mwishoni mwa mwezi Septemba mwaka huu, limesema shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi duniani, UNHCR. 

Mama akimlisha mtoto wake mwenye utapiamlo katika kliniki ya Madaktari wasiokuwa na mipaka katika kambi ya Dadaab, Kenya.
OCHA/Meridith Kohut
Mama akimlisha mtoto wake mwenye utapiamlo katika kliniki ya Madaktari wasiokuwa na mipaka katika kambi ya Dadaab, Kenya.

Wenyeji na wakimbizi waonesha ukaribu kwa wageni 

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi hii leo, Msemaji wa UNHCR Boris Cheshirkov amesema wenyeji katika eneo la Dadaab kaunti ya Garissa pamoja na wakimbizi kwenye kambi hiyo wanajitolea kwa ukaribu kuwakaribisha wageni na kugawana nao kile kidogo walicho nacho. 

Hata hivyo amesema “nafasi katika kambi inaendelea kuwa finyu na kulazimu wengi wao kuishi katika maeneo ya muda kwenye viunga vya kambi hiyo ambako huduma za maji safi na salama pamoja na huduma za kujisafi hazitoshelezi au haziko kabisa.” 

Kama hiyo haitoshi, Bwana Cheshirkov amesema mlipuko wa ugonjwa wa kipindupundu umekumba wenyeji na wakimbizi na zaidi ya wagonjwa 350 wamethibitika tangu mwezi Oktokba mwaka huu na wengi wao ni watoto. 

Kipindupindu chaongeza machungu 

Katika eneo moja ambako watendaji wa UNHCR walitembelea, ni familia moja inayohifadhi watu 28, ambapo 8 kati yao tayari wameambukizwa kipindupindu. 

“Vituo vya kutibu kipindupindu vinahitaji vifaa zaidi pamoja na watendaji ili kusaidia kukabili kusambaa zaidi kwa ugonjwa huo. Hata hivyo tunashukuru wadau wetu wa afya kwani kutokana na msaada wao maambukizi yanapungua; lakini tuna wasiwasi kuhusu hatari ya maambukizi,” amesema Bwana Cheshirkov. 

Amefafanua kuwa kutokana na changamoto hiyo, UNHCR inahakikisha katika maeneo ya viunga vya kambi ya Dadaab ambako wakimbizi wapya wanawasili, wanapatiwa huduma ya maji safi na salama na huduma za kujisafi. 

Halikadhalika huduma za ulinzi kwa makundi  yaliyo hatarini. Watoto walio na utapiamlo wanapalekwa kwenye vituo vya huduma ya tiba lishe  

“Mipango inaendelea ili kuimarisha msaada wa kutoa vifaa vya ziada vya kiutu ikiwemo vikasha vya vifaa vya kujisitiri kwa wanawake na wasichana wakati wa hedhi,” amesema msemaji huyo wa UNHCR mjini Geneva, Uswisi. 

Kundi la wanawake wa Kisomali waliokimbia makazi yao wanaoishi katika Kambi ya Wakimbizi ya Ifo 2 huko Dadaab, Kenya, ambalo linasaidiwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR).
Picha ya Umoja wa Mataifa/Evan Schneider
Kundi la wanawake wa Kisomali waliokimbia makazi yao wanaoishi katika Kambi ya Wakimbizi ya Ifo 2 huko Dadaab, Kenya, ambalo linasaidiwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR).

Mgeni njoo mwenyeji apone 

Kwa upande wa wenyeji, UNHCR inasaidia jamii wenyeji katika maeneo ya Dadaab kukarabati visima vya maji kwa kuzipatia jenereta za kusukuma maji, halikadhalika malori ya kusambaza maji safi. 

UNHCR imesema kwa upande wa wakenya, takribani wakenya milioni 4.5 kaskazini na mashariki mwa taifa hilo la Afrika MAshariki nao wanakabiliwa na madhara ya ukame wa muda mrefu na familia zinahaha kupata chakula na maji, na hali inaweza kuwa mbayá zaidi iwapo msimu wa sasa wa mvua nao hautakuweko. 

Ombi la kusaidia Kenya limejibiwa kwa asilimia 50 tu 

Mwezi uliopita, UNHCR na wadau walitoa wito wa ombi la dola milioni 472.6 kuwezesha mashirika ya kiutu kuweza kutoa msaada sasa hadi mwakani kwa kuwa madhara ya ukame yanazidi kushamiri nchini Kenya. 

UNHCR inasema msaada zaidi unahitajika siyo tu kwa Kenya bali pia Somalia na Ethiopia ambako mamilioni ya watu wanakabiliwa na mazingira magumu ya kiutu kutokana na kutonyesha kwa mvua. 

Mwezi Juni, kama sehemu ya ombi la kikanda kwa Pembe ya Afrika, UNHCR iliomba dola milioni 11.1 kusaidia zaidi ya watu  257,000 walioathiriwa na ukame Kenya, ikiwemo wakimbizi wapya 55,000. 

“Hadi sasa ni nusu tu ya fedha zinazohitajika ndio zimepatikana, hata wakati huu ambapo idadi ya watu wanaowasili ni kubwa kuliko ilivyotarajiwa,” amesema Bwana Cheshirkov. 

Amesisitiza kuwa fedha zaidi zinahitajika il ikukidhi mahitaij yanayoongezeka kila uchao yakiwemo ya msaada wa kuokoa maisha na ulinzi.