Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanawake wa jamii ya asili Peru wachukua hatua kulinda misitu

Nchini Peru wanawake wa jamii ya asili ya Awajun wanapata miti kwenye vitalu ili kurejesha misitu iliyoharibiwa.
IFAD Video
Nchini Peru wanawake wa jamii ya asili ya Awajun wanapata miti kwenye vitalu ili kurejesha misitu iliyoharibiwa.

Wanawake wa jamii ya asili Peru wachukua hatua kulinda misitu

Tabianchi na mazingira

Kwa takribani wiki moja sasa tumekuwa tukimulika masuala ya tabianchi  na mazingira kwa kuzingatia kuwa hivi sasa mkutano wa 27 wa nchi wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi, COP27 unaendelea huko Sharm el-Sheikh nchini Misri na lengo ni kusongesha harakati za kukabiliana na kuhimili mabadiliko ya tabianchi ambayo kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres hali  ya sasa ni ya udharura, hatua lazima zichukuliwe.

Watu wanakutana huku tayari makundi mbalimbali ikiwemo jamii za watu wa asili yameshaanza kuchukua hatua kwa kuwa madhara yamebisha hodi kwenye makazi yao. Miongoni mwao ni wanawake wa jamii ya asili ya Awajun huko Alto Mayo nchini Peru, Amerika ya Kusini.

Katika video ya mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Maendeleo ya kilimo , IFAD unaonekana uwanda mpana wa konde la vitalu vya miti, wanawake 12 wa kabila la watu wa asili la Awajun huko nchini Peru wanatembea kwa ukakamavu wakiwa wamevalia lubega nguo zao za kitamaduni.

Vitalu hivi vya miti ni kwa ajili ya kukuza misitu iliyokumbwa na ukataji holela, sasa jamii hii imechukua hatua kulinda msitu na wakati huo huo kujipatia kipato.

Mila na tamaduni katika kupanda misitu na mitishamba

Uziela Achayap Sejekam ni Rais wa kikundi chao kiitwacho Bosque De Las Nuwas anafafanua akisema, kama mwanamke, nimejifunza mila za kitamaduni. Msimu ni makazi yangu, msitu ni nyumbani kwangu. Nimepambana kila siku ili akina mama vijana ili waweze kuwa na furs aya kuwa wajasiriamali. »

Nchini Peru, ukataji holela wa misitu na vipindi virefu vya ukame vimeharibu mfumo wa ikolojia, lakini sasa kikundi hiki chenye jumla ya wanachama 20 wanawake kutoka jamii ya asili ya Awajun kimechukua hatua ya kurejesha misitu, sio tu kwa kupanda miti pekee, bali pia mitishamba, au miti ambayo inatumika kutengenezea dawa lishe pamoja na viungo.

Dawa hizo pamoja na viungo ambavyo vinaweza kutengeneza chai, wanauza au wanatumia wenyewe kwa ajili ya matibabu.

Hata hivyo hilo upandaji wa vitalu vya miti na mitishamba umefanikishwa na msaada kupitia fedha za kuhimili mabadiliko ya tabianchi kutoka mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Maendeleo ya kilimo, IFAD na serikali ya Peru.

Maendeleo vijijini na wanawake wa jamii ya asili

Brenda Lopez Torres ni Mtaalamu wa Kiufundi wa kilimo vijijini katika Wizara ya Kilimo nchini Peru na anasema, katika eneo la Alto Mayo, madhara makubwa yatokanayo na mabadiliko ya tabianchi ni ongezeko la viwango vya joto na ukosefu wa mvua. Madhara ya ukataji misitu holela yaliwapata zaidi watu wa jamii ya asili. Imekuwa ni dalili ya onyo kwao. Ndio maana wameanzisha shughuli kama vile upandaji miti kwa ajili ya kukuza misitu.”

Sasa katika video ya IFAD, wanakikundi hawa wako kwenye konde lao la vitalu vya miti, wengine wakionekana waking’oa magugu huku wengine wakipalilia kwenye vitalu.

Vitalu vimewekewa mfumo wa umwagiliaji wa matone. Mabomba madogo yameunganishwa kwenye vitalu na hivyo kudondosha matone ya maji kwa muda unaotakiwa.

Ruth Cumbia Sejekam, mratibu wa Kamati ya Kazi ya kikundi hiki anaonesha makopo ambamo kwayo ndani kuna chai itokanayo na mitishamba waliyopanda.

Ruth anasema, “kulinda msitu kunanufaisha na kusaidia si mimi peke yangu binafsi na watu wa jamii ya awajun, bali kila mtu.”

Uziela Achayap Sejekam, ni Rais wa kikundi cha wanawake wa jamii ya asili ya AWajun nchini Peru na wanachofanya ni kupanda miti na mitishamba kama njia ya kurejesha misitu.
IFAD Video
Uziela Achayap Sejekam, ni Rais wa kikundi cha wanawake wa jamii ya asili ya AWajun nchini Peru na wanachofanya ni kupanda miti na mitishamba kama njia ya kurejesha misitu.

Wanawake wa jamii ya asili na umwagiliaji

Uziela Achayap Sejekam, Rais wa Kikundi hiki cha wanawake wa jamii ya asili wa kabila la Awajun nchini Peru anarejea tena akisema, “kama Awajun tulishaanza kufanya kazi hii ya kuloweka miti shamba na viungo na kisha kupata chai, kitu ambacho siku hizo kina mauzo makubwa. Lakini kwas asa hatuna malighafi ya kutosha ya kuweza kuendesha mradi huu kibiashara.”

Maji yanayotumika kumwagilia vitalu vya miti kwa njia ya matone yanatoka kwenye kisima cha maji ambapo Uziela anasema, “jambo muhimu kwetu sisi ni kuhakikisha hili boza la maji linakuwa limejaa maji na tuweze kumwagilia vitalu vyetu kila siku.”

Katika maeneo ambako miti na mishamba imeota, anaonekana Ruth akivinjari huku akichuma baadhi ya miti na maua yaliyochanua na anasema, “kurejesha misitu ni kwa manufaa yangu. Itafika wakati mimi sitakuwepo hapa duniani. Hatuko hapa daima. Wale ambao watabakia ndio wataendelea kufurahia mazingira, hewa na kila kitu ambacho tunawaachia.”

Wanawake hawa wa jamii ya asili ni miongoni mwa watu watakaotoa mada kwenye mkutano wa 27 wa nchi wanachama wa mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya tabianchi, COP27 unaoendelea huko Sharm el- Sheikh nchini Misri.

Ushiriki wao ni muhimu kwa kuwa katika COP26 mwaka jana huko Glasgow, Scotland walikuwa kitovu cha mjadala na azimio la mkutano huo liliahidi kutokomeza ukataji holela wa misitu ifikapo mwaka 2030.