Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkaazi wa bilioni nane kuzaliwa duniani, je sayari yetu inaweza kukidhi mahitaji ya kila mtu: Guterres

Umoja wa Mataifa unasema ilichukua miaka 12 idadi ya watu duniani kuongezekaka kutoka bilioni 7 hadi bilioni 8, sasa itachukua miaka 15 kuongezeka kutoka bilioni 8 hadi 9.
Benki ya Dunia/Hendri Lombard
Umoja wa Mataifa unasema ilichukua miaka 12 idadi ya watu duniani kuongezekaka kutoka bilioni 7 hadi bilioni 8, sasa itachukua miaka 15 kuongezeka kutoka bilioni 8 hadi 9.

Mkaazi wa bilioni nane kuzaliwa duniani, je sayari yetu inaweza kukidhi mahitaji ya kila mtu: Guterres

Masuala ya UM

Katikati ya mwezi huu wa Novemba, dunia itashuhudia mkaazi wa bilioni nane akizaliwa. Mkaazi huyo anazaliwa kwenye sayari ambayo vita bado vinaendelea, ukosefu wa usawa unatawala, mamia ya mamilioni ya watu hawana lishe na wanakabiliwa na majanga ya mabadiliko ya tabianchi.  

Wanafunzi wakiwa darasani huko Boundiali, kaskazini mwa Côte d'Ivoire.
© UNICEF/Milequem Diarassouba
Wanafunzi wakiwa darasani huko Boundiali, kaskazini mwa Côte d'Ivoire.

Hayo yamesemwa katika makala maalum ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres kwa vyombo vya habari.  

Ndani ya Makala hiyo, mkuu wa Umoja wa Mataifa ameonyesha matumaini kwamba katika miongo ijayo, nchi zilizo na viwango vya juu zaidi vya ongezeko la watu zitakuwa injini za maendeleo endelevu na ustawi. 

"Katikati ya Novemba, idadi ya watu duniani itafikia watu bilioni nane ni ushahidi wa mafanikio ya kisayansi na uboreshaji wa lishe, afya na usafi wa mazingira," mkuu wa Umoja wa Mataifa alisema.  

Hata hivyo, amesisitiza kuwa mafanikio hayo ya idadi ya watu yamegubikwa na ukweli kwamba mabilioni ya watu wanaishi katika mazingira magumu, mamia ya mamilioni wanakabiliwa na utapiamlo na hata njaa.  

Watu wengi wanalazimika kuacha nyumba zao, ikiwa ni pamoja na kutokana na athari za vita na majanga ya mbadiliko ya tabianchi. Yote hii inaongeza ukuaji wa mivutano na migawanyiko. 

"Iwapo hatutaziba pengo lililopo kati ya matajiri na maskini, tutajitia hatiani wenyewe kusihi katika ulimwengu wa watu bilioni nane ulioghubikwa na mivutano na kutoaminiana, migogoro na vita.” Ameonya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. 

Mabilionea wachache, anasema, wanamiliki utajiri mwingi kama ilivyo nusu ya watu maskini zaidi wa ubinadamu wetu. Asilimia moja ya watu matajiri zaidi duniani wanachangia moja ya tano ya mapato ya dunia.  

Watu katika nchi tajiri zaidi wanaweza kuishi hadi miaka 30 zaidi kuliko watu katika nchi maskini zaidi.  

Wakati huo huo, ustawi wa idadi ya watu duniani kwa ujumla unavyoongezeka na matokeo ya afya yanaboreka, ukosefu wa usawa nao unaongezeka.  

Katika miongo miwili iliyopita watu bilioni 2 walipata huduma ya maji safi na salama
WHO
Katika miongo miwili iliyopita watu bilioni 2 walipata huduma ya maji safi na salama

Mizani ya usawa na mgawanyiko  

Mitindo hii ya kuongezeka kwa ukosefu wa usawa inaongezwa na athari za mabadiliko ya tabianchi na janga la COVID-19. Amesema Guterres na kuongeza kuwa " majanga kama mafuriko, dhoruba na ukame ni vyanzo vyenye uharibifu mkubwa kwa nchi ambazo hazihusiki sana na ongezeko la joto duniani,". Ameongeza kuwa vita vya Ukraine vinazidisha mzozo wa chakula, nishati na kifedha duniani. 

Aidha, leo hii nchi nyingi za Kusini mwa dunia zinakabiliwa na madeni makubwa, umaskini na njaa vinaongezeka, na madhara makubwa ya ongezeko la joto duniani. Nchi hizi hazina uwezo wa kuwekeza katika miradi endelevu ya kujikwamua baada ya janga hili, kuhamia kwenye nishati mbadala au elimu ambayo inazingatia mafanikio ya enzi hizi za dijitali. 

"Hasira na kutoridhika dhidi ya nchi zilizoendelea kunaongezeka. Migawanyiko haribifu na kutoaminiana husababisha mkwamo wa masuala muhimu kuanzia upokonyaji silaha za nyuklia na ugaidi hadi afya ya umma. Ni lazima tuache mienendo hii yenye madhara, tujenge uhusiano na kutafuta suluhisho za pamoja za matatizo yetu ya pamoja,” amehimiza Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.  

Kwa maoni yake, amesema “kwa kuanzia, lazima tutambue kwamba ukuaji wa usawa ni matokeo ya vitendo vya ufahamu, na nchi zilizoendelea zina wajibu wa kubadili hali hii.” 

Mabadiliko ya hali ya tabianchi 

Bwana Guterres amesema mkataba wa kihistoria wa mshikamano wa mabadiliko ya tabianchi unapaswa kutiwa saini katika mkutano wa COP27 unaoendelea  nchini Misri.  

Amekumbusha kuwa nchi tajiri zinapaswa kutoa msaada wa kifedha na kiufundi kwa uchumi unaoibuka wa soko, ikiwa ni pamoja na kusaidia miradi inayohusiana na kuondokana na nishati ya mafuta kisukuku.  

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amewataka viongozi wa nchi zinazohudhuria COP27 kukubaliana juu ya ramani ya barabara na mfumo wa kitaasisi wa kufidia nchi za Kusini mwa dunia kwa hasara na uharibifu unaohusiana na mabadiliko ya tabianchi ambayo tayari yanasababisha mateso makubwa. 

Msaada kwa nchi masikini 

Akizungumzia mkutano wa G20 mjini Bali, António Guterres ameelezea matumaini yake kuwa utashughulikia hali mbaya ya nchi zinazoendelea.  

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amezitaka nchi za G20 kuidhinisha kifurushi cha hatua za kichocheo kusaidia serikali za Kusini mwa dunia katika uwekezaji na kukuza msamaha na urekebishaji wa madeni. 

Mpango wa Bahari Nyeusi 

Akikumbusha kuhusu mzozo mkubwa wa chakula duniani, António Guterres amebainisha umuhimu wa mpango wa usafirishaji wa nafaka wa Bahari Nyeusi, ambao utekelezaji wake, kulingana na yeye, unachangia kuleta utulivu wa masoko na kupunguza bei ya chakula duniani. 

“Pia tunajitahidi kuhakikisha kwamba mbolea za Urusi zinafika katika masoko ya dunia ambayo yameathiriwa kwa kiasi kikubwa na vita. Mbolea ni ghali mara tatu zaidi kuliko kabla ya janga hili. Athari kubwa zaidi itakuwa katika uzalishaji wa mpunga, chakula kikuu kinachotumiwa zaidi duniani.” 

Katika hilo, amesisitiza kuwa kuondoa vikwazo vilivyosalia katika usafirishaji wa mbolea ya Urusi ni moja ya hatua muhimu katika kuhakikisha uhakika wa chakula duniani kote. 

Idara ya Uchumi na Kijamii ya UM, DESA na makadirio ya idadi ya watu duniani mwaka 2022.
UNFPA
Idara ya Uchumi na Kijamii ya UM, DESA na makadirio ya idadi ya watu duniani mwaka 2022.

Matarajio ya maendeleo ya nchi zenye ongezeko kubwa la watu 

Baada ya kuorodhesha matatizo makuu duniani, António Guterres amesema kuwa kuna habari njema. "Katika ulimwengu wetu wa watu bilioni 8, kunaweza kuwa na fursa za ajabu kwa baadhi ya nchi maskini zenye viwango vya juu zaidi vya ongezeko la watu,”.  

Mkuu wa Umoja wa Mataifa ana imani kwamba uwekezaji mdogo katika afya, elimu, usawa wa kijinsia na maendeleo endelevu unaweza kubadilisha uchumi na maisha ya watu. 

"Ndani ya miongo michache, nchi maskini zaidi za leo zinaweza kuwa injini za ukuaji endelevu, unaojali mazingira na ustawi kwa kanda nzima," Anaamini Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.  

Amesema kwamba anaamini katika mshikamano wa kibinadamu, na akakumbuka maneno ya Mahatma Gandhi, kwamba sayari yetu inaweza kukidhi mahitaji ya kila mtu, lakini si uchoyo wa kibinadamu. 

Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametoa wito kwa nchi zote "kuondokana na tofauti na kurejesha uaminifu kwa msingi wa usawa na kuzingatia uhuru wa kila mwanachama wa familia ya binadamu wote bilioni nane."