Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dunia inapaswa kushikamana kutimiza mahitaji ya watu bilioni 8 kupitia SDGs: UNFPA

UN inasema mwaka 2037 idadi ya watu duniani itafikia bilioni 9
© UNICEF/Stuart Tibaweswa
UN inasema mwaka 2037 idadi ya watu duniani itafikia bilioni 9

Dunia inapaswa kushikamana kutimiza mahitaji ya watu bilioni 8 kupitia SDGs: UNFPA

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Idadi ya watu duniani leo 15 Novemba 2022 imefikia watu bilioni 8, ikiashiria hatua kubwa zilizopigwa katika masuala ya afya ambazo zimesaidia kupunguza hatari ya vifo na kuongeza umri wa kuishi limesema shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu duniani na masuala ya afya ya uzazi UNFPA. 

Hata hivyo shirika hilo limesema huu ni wakati wa kuangalia kwa undani utu wa binadamu zaidi ya idadi ya watu na kutimiza wajibu wa pamoja wa kulinda watu na sayari tukianza na walio hatarini zaidi. 

Naye Katibnu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akiongeza sauti yake katika hili amesema “Hadi pale tutakapoziba pengo la kimataifa kati ya walionancho na wasionacho tunajiandaa kuwa na watu bilioni 8 katika dunia iliyoghubikwa mivutano, kutoaminiana, migogoro na vita.” 

Wanafunzi wakishiriki katika mpango wa elimu katika kituo cha Kashonjwa nchini Uganda
© UNICEF/ Zahara Abdul
Wanafunzi wakishiriki katika mpango wa elimu katika kituo cha Kashonjwa nchini Uganda

Ulimwengu ulio tofauti zaidi ya hapo awali 

Wakati idadi ya watu duniani itaendelea kukua hadi kufikia bilioni 10.4 katika miaka ya 2080, kiwango cha ukuaji kinapungua kwa mujibu wa UNFPA na ulimwengu umetofautiana zaidi kidemografia kuliko hapo awali, huku nchi zinakabiliwa na mwelekeo tofauti kabisa wa idadi ya watu kuanzia ukuaji hadi kupungua.  

Taarifa ya shirika hilo imeongeza kuwa “Leo, theluthi mbili ya idadi ya watu duniani wanaishi katika mazingira ya uzazi wa kiwango cha chini, ambapo uzazi ni chini ya kuzaa watoto 2.1 kwa kila mwanamke. Wakati huo huo, ongezeko la idadi ya watu linatokea zaidi miongoni mwa nchi maskini zaidi duniani, ambazo nyingi ziko katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.” 

Kutokana na hali hii, UNFPA inasema jumuiya ya kimataifa lazima ihakikishe kwamba nchi zote, bila kujali kama idadi ya watu inaongezeka au inapungua, zimeandaliwa kutoa hali nzuri ya maisha kwa wakazi wao na zinaweza kuinua na kuwawezesha watu wao waliotengwa zaidi. 

"Ulimwengu wa watu bilioni 8 ni hatua muhimu kwa ubinadamu na ni matokeo ya muda mrefu ya kuongeza umri wa maisha, kupungua kwa umaskini, na kupungua kwa vifo vya uzazi na vya watoto. Hata hivyo, kuzingatia idadi pekee hakutotuondoa kutoka kwa changamoto halisi tunayokabiliana nayo, kupata dunia ambayo maendeleo yanaweza kufurahiwa kwa usawa na kwa uendelevu,” amesema mkurugenzi mtendaji wa UNFPA Dkt. Natalia Kanem. 

Ameongeza kuwa "Hatuwezi kutegemea suluhisho mmoja kwa kila kitu katika ulimwengu ambao umri wa wastani ni miaka 41 barani Ulaya ikilinganishwa na 17 katika bara la Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara. Ili kufanikiwa, sera zote za idadi ya watu lazima ziwe na haki za uzazi katika msingi wao, ziwekeze kwa watu na sayari, na ziwe na msingi wa takwimu thabiti.” 

Kundi la watoto wakitabasamu katika kijiji cha Ismail Bhand katika wilaya ya Shaheed Benazirabad nchini Pakistani, mkoa wa Sindh.
© UNICEF/Shehzad Noorani
Kundi la watoto wakitabasamu katika kijiji cha Ismail Bhand katika wilaya ya Shaheed Benazirabad nchini Pakistani, mkoa wa Sindh.

Uhusiano tata kati ya idadi ya watu, SDGs na mabadiliko ya tabianchi 

Ingawa siku ya leo ya kutimiza idadi ya watu  bilioni 8 inawakilisha hadithi ya mafanikio kwa binadamu, pia inazua wasiwasi kuhusu uhusiano kati ya ongezeko la idadi ya watu, umaskini, mabadiliko ya tabianchi na kufikiwa kwa malengo ya maendeleo endelevu SDGs. Limesema shirika la UNFPA. 

Limeongeza kuwa “Uhusiano kati ya ukuaji wa idadi ya watu na maendeleo endelevu ni mgumu. Ongezeko la kasi la idadi ya watu hufanya kutokomeza umaskini, kupambana na njaa na utapiamlo, na kuongeza wigo wa mifumo ya afya na elimu kuwa vigumu zaidi. Kinyume chake, kufikia SDGs, hasa yale malengo yanayohusiana na afya, elimu na usawa wa kijinsia, kutachangia kupunguza kasi ya ongezeko la watu duniani.” 

Li Junhua, msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya kiuchumi na kijamii.  Amesema "Lazima tuharakishe juhudi zetu ili kufikia malengo ya mkataba wa Paris  wa mabadiliko ya tabianchi pamoja na kufikia malengo ya SDGs. Tunahitaji kuunganishwa kwa haraka kwa shughuli za kiuchumi kutoka kwenye utegemezi zaidi wa sasa wa nishati ya mafuta kisukuku, pamoja na matumizi ya rasilimali hizo, na tunahitaji kufanya mabadiliko haya kuwa ya haki na jumuishi ambayo yatasaidia wale walioachwa nyuma zaidi.” 

Tunahitaji mustakbali endelevu wenye haki na usawa 

Kwa mujibu wa UNFPA ili kuwa na ulimwengu ambao watu wote bilioni 8 wanaweza kustawi, “ni lazima tutafute suluhu zilizothibitishwa na madhubuti za kupunguza changamoto za ulimwengu wetu na kufikia malengo ya SDGs, huku tukizipa kipaumbele haki za binadamu. Ili kutafuta suluhu hizi, ongezeko la uwekezaji kutoka kwa nchi wanachama na serikali za wafadhili unahitajika katika sera na programu zinazofanya kazi kuifanya dunia kuwa salama, endelevu zaidi na shirikishi zaidi.” 

Mtoa huduma za Afya kitengo cha Mama na Mtoto katika Zahanati ya Kata ya Mkambalani Rebeca Wami akimfanyia vipimo vya ukuaji mtoto huku mama yake akishuhudia  wakati wa wiki ya unyonyeshaji.
Hamad Rashid
Mtoa huduma za Afya kitengo cha Mama na Mtoto katika Zahanati ya Kata ya Mkambalani Rebeca Wami akimfanyia vipimo vya ukuaji mtoto huku mama yake akishuhudia wakati wa wiki ya unyonyeshaji.

Mambo muhimu na takwimu  

• Ilichukua takriban miaka 12 kwa idadi ya watu duniani kukua kutoka bilioni 7 hadi 8, lakini bilioni ijayo inatarajiwa kuchukua takriban miaka 14.5 (2037), kuakisi kushuka kwa ukuaji wa kimataifa. Idadi ya watu ulimwenguni inakadiriwa kufikia kilele cha karibu watu bilioni 10.4 katika miaka ya 2080 na kubaki katika kiwango hicho hadi 2100. 

• Kwa ongezeko kutoka bilioni 7 hadi 8, karibu asilimia 70 ya watu walioongezeka walikuwa katika nchi za kipato cha chini na cha kati. Kwa ongezeko hilo kutoka bilioni 8 hadi 9, makundi haya mawili ya nchi yanatarajiwa kuchangia zaidi ya asilimia 90 ya ukuaji wa kimataifa. 

• Kati ya sasa na 2050, ongezeko la kimataifa la idadi ya watu chini ya umri wa miaka 65 litatokea katika nchi za kipato cha chini na cha kati, kwa kuwa ongezeko la watu katika nchi za kipato cha juu na za juu kati litatokea tu kati ya wale wenye umri wa miaka 65 au zaidi.